Na Saleh Ally
HADITHI ya beki wa kati wa Yanga, Vicent Andrew maarufu
kama Dante imechukua sura mpya baada ya mashitaka kufika kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Dante amefungua mashitaka yake akiidai Yanga kitita cha Sh milioni 40 ikiwa ni sehemu ya malipo yake kadhaa, zikiwemo fedha za usajili.
Wakati Dante anadai, tayari alichukua uamuzi wa kususia
kuichezea Yanga hadi pale atakapolipwa fedha zake hizo
ambazo amezidai kwa zaidi ya msimu mmoja na nusu bila ya
mafanikio.
Uongozi wa Yanga kupitia msemaji wake, Hassan Bumbuli
umeeleza ulikuwa tayari kumlipa Dante na ulikubaliana naye kwamba ungeendelea kumlipa kidogokidogo au kwa mafungu.
Hata hivyo, Dante akaamua kwenda kushitaki, jambo ambalo wanaona kama limewashangaza huku wakiwa wanaamini hata TFF nayo ikipitisha alipwe, lazima itakuwa kwa mafungu.
Hakuna ubishi kweli Yanga haiko katika hali nzuri sana ya kulipa fedha zote hizo kwa wakati mmoja, hili ni jambo liko wazi na tunaamini uongozi wa Yanga utakuwa hauongopi katika hilo.
Pia, kitu kingine kizuri kabisa katika sakata hili ni kwamba,
uongozi wa Yanga haijakataa kulipa na haujakataa kama
unadaiwa. Badala yake unasema upo tayari kulipa taratibu.
Pamoja na hivyo, sote tunajua kuwa Dante ameamua kugoma baada ya uvumilivu kumshinda. Kwamba alijitahidi kuvumilia kwa muda mrefu lakini ahadi zimeendelea bila ya kutimizwa na suala la subiri limekuwa kwa muda mrefu sana.
Huenda uongozi wa sasa wa Yanga unaweza usiwe unayajua
machungu ya Dante kwa asilimia kubwa kwa kuwa wakati
akipambana na “njaa” yake, viongozi waliopo sasa hawakuwa wameingia madarakani, hivyo kwanza hawapaswi kulaumiwa kwa yale ya zamani lakini nao wanapaswa kurudi nyuma na kutazama upya alikopitia Dante.
Hakuna hata mtu mmoja anayeweza kunyoosha mkono na
kusema Dante si beki mzuri, si beki aliyeitumikia Yanga kwa
juhudi na maarifa au si mchapakazi. Lakini nani anayeweza
kuendelea kuchapa kazi bila ya kuwa na taswira ya ubora wa maisha yake ya kesho wakati ni kijana anayepambana
kutengeneza maisha yake ya baadaye.
Vizuri tukajikumbusha, wachezaji nao ni binadamu kama sisi na wanapokuwa wanazitumikia timu wanakuwa kazini na
wangependa kupata maendeleo kama tupendavyo sisi
tunapoamka na kwenda makazini au katika biashara zetu. Hivyo tusiwakandamize kwa kisingizio cha mapenzi.
Kikubwa Yanga na Dante, bado wana nafasi ya kukaa mezani na niwakumbushe, si vibaya wakaunda urafiki wa mbuzi na majani. Mmoja mfano Yanga wakubali kuwa majani na Dante au mbuzi au yeye awe mbuzi na wao wawe majani.
Mbuzi, anategemea majani kuendesha maisha yake. Lakini
baada ya kula, naye anayapa haki kwa kujisaidia na baadaye
inakuwa mbolea ya kukuza majani mengine yenye rutuba
ambayo yanakuwa msaada kwa maisha ya mbuzi hapo
baadaye.
Dante anapaswa kulishwa ili aishi Yanga baadaye akiwa
ameshiba. Ana mahitaji yake kama mwanadamu na kama
akitimizwa basi atakuwa faida kubwa au msaada sahihi kwa
kikosi cha Yanga.
Tukubaliane kuwa mwanadamu yoyote, iwe mimi au wewe,
anachoshwa na ahadi zisizotimizika. Kama mtu anakuahidi mara moja, mbili, tatu na akaendelea bila kutimiza, baadaye inaingiza fikra nyingine mfano dharau na kadhalika.
Dante amevumilia kwa muda mrefu akiendelea kuitumikia
Yanga na bado mambo hayakuwa mazuri. Hivyo alipofikia,
amechoka na aeleweke kwamba anastahili chake kwa kuwa ni haki yake. Hivyo, Yanga ianze kuonyesha mfano kwa kumlipa kwanza na si maneno.
Inawezekana, kwa kuwa hali ni mbaya lakini haki ni ya Dante, basi alipwe hata robo. Halafu Yanga iweke kauli dhabiti ambayo inaweza kuwa na ushahidi wa TFF kwa kuwa jambo hilo limeshafika huko, mwisho Dante arejee kazini kiroho safi na kuisaidia klabu yake kwa kuwa kuna maisha baada ya deni.
Ninaamini usikivu, uvumilivu na busara ya kutosha inaweza
kuwa msaada mkubwa wa kulimaliza hili suala ambalo hakika, kukiwa na nia njema, ni jepesi sana.
Hebu tujitahidi tumlipe huyo Dante kapigana sana kijana
ReplyDelete