November 15, 2019


ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera muda wowote atajiunga na klabu moja kati ya tatu za Afrika. Kati ya klabu zinazomtaka ni Horoya ya Guinea, Buildcon FC (Zambia) au moja ya nchini Afrika Kusini zilizoonyesha nia ya kuhitaji huduma yake.

Hii imetokea ikiwa ni siku chache tangu kocha huyo asitishiwe mkataba wake wa kuendelea kukinoa kikosi hicho kabla ya Charles Boniface Mkwasa kukaimu nafasi hiyo akisaidiana na Said Maulid (SMG).

Kocha huyo wikiendi iliyopita alikabidhiwa barua ya kusitishiwa mkataba wake kabla ya kusafi ri kwenda Congo kuungana na timu yake ya taifa inayojiandaa na michezo miwili ya kirafiki.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, kocha huyo yupo kwenye mazungumzo na klabu hizo tatu na kati ya hizo mojawapo ikiwemo Horoya anayoichezea mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Heritier Makambo. Mtoa taarifa huyo alisema kati ya timu hizo, Horoya ndiyo imeonekana kumpa nafasi kubwa.

Aliongeza kuwa kocha huyo kabla ya kujiunga na timu hiyo atarejea nchini kwa ajili ya kuchukua malipo yake ya fedha ambazo ni Sh Mil. 48 za mishahara yake ya miezi mitatu kati ya hiyo miwili anayodai nyuma na ule wa mwezi mmoja wa kusitishiwa mkataba wake ambao kwa mwezi alikuwa akilipwa Sh Mil. 16.

“Zahera anaondoka Yanga akiwa na uhakika wa kupata nafasi ya kwenda kufanya kazi kwingine kwa maana ya kufundisha, ni baada ya kupata ofa zaidi ya tatu ikiwemo Horoya, Buildcon na moja kutoka Afrika Kusini.

“Hivyo, kati ya hizo mojawapo atajiunga nayo mapema mara baada ya kumaliza majukumu yake ya timu ya taifa, lakini kati ya hizo Horoya ambayo anaichezea Makambo ndiyo inaonekana kuwa karibu zaidi kumchukua,” alisema mtoa taarifa huyo.

Zahera kabla ya kuondoka nchini aliliambia Championi: “Nina ofa nyingi, ni mapema kuzitaja kwa sababu nipo kwenye mazungumzo na kama kila kitu kitakaa sawa, basi nitaweka wazi.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic