December 28, 2019


MWAKA 2019 unamalizika. Ukiachana na leo, zimebaki siku tatu pekee kuumaliza mwaka huu ambao upande wa michezo hapa nchini umekuwa wa kihistoria.
Historia kubwa ni kitendo cha Taifa Stars kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) iliyofanyika Misri.
Ilipita takribani miaka 39 bila ya Tanzania kushiriki michuano hiyo mikubwa Afrika kwa ngazi ya timu za taifa. Unapoitaja Afcon, ni wazi michuano mikubwa hapa Afrika ambayo inahusisha timu za taifa.
Katika historia ya nchi hii, ni mara mbili pekee Tanzania imeshiriki michuano hiyo. Mara ya kwanza ilikuwa 1980 kule Nigeria, mara ya pili 2019. Kiukweli naweza kusema 2019 ulikuwa mwaka wa mafanikio kisoka kwetu ingawa kulikuwa na changamoto za hapa na pale.
Mbali na Taifa Stars, kitendo cha Tanzania kuanza Afcon ya vijana chini ya miaka 17, nayo ni mafanikio makubwa katika nchi hii. Ni mara ya kwanza tunaandaa michuano hiyo.
Ingawa timu yetu haikufanya vizuri, lakini kitendo cha kuandaa michuano hiyo ni heshima kubwa. Nchi nyingi zilikuwa zikihitaji kuandaa, lakini bahati ikaangukia kwetu.
Kuandaa michuano hiyo ya vijana ni njia ya kuja kuandaa ile ya wakubwa. Tuombe uhai na uzima tuweze kuandaa michuano hiyo miaka michache ijayo. Nadhani tumejifunza kutokana na kile kilichotokea.
Ukiachana na hayo, timu yetu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20, ilitwaa ubingwa wa Cosafa kule Afrika Kusini, pia timu ya taifa ya vijana wa kiume chini ya miaka 20, nayo ilitwaa ubingwa wa Cecafa kule Uganda. Mwaka 2019 unamalizika kwa mafanikio hayo. Tunapaswa kujivunia nayo.
Siku zote katika mafanikio, changamoto hazikosekani, hivyo basi katika zile changamoto zilizojitokeza mwaka huu, tuzichukue kama sehemu ya kujifunzia kurekebisha mambo ili tuwe na mafanikio makubwa zaidi.
Ukiangalia ligi zetu zimekumbwa na changamoto nyingi. Si Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili hata Ligi Kuu ya Wanawake, kote huko kuna changamoto zake.
Changamoto kubwa ni viwanja kutokuwa kwenye hali nzuri, huku vikitumiwa kwa matumizi mbalimbali tofauti na soka.
Mfano mzuri Uwanja wa Sokoine uliopo Mbeya, hivi sasa umezuiwa kutumika kwa mechi za ligi kutokana na kuharibiwa vibaya sana na watu waliofanya shoo ya muziki.
Kufungiwa kwa uwanja huo ni pigo kubwa kwa timu zilizokuwa zikiutumia. Hivi sasa zitakuwa na wakati mgumu katika kutafuta viwanja vingine.
Kuna changamoto ya ratiba, imekuwa ikipanguliwa kila kukicha jambo ambalo wadau mbalimbali wamekuwa wakilipigia kelele. Naamini 2020 haya yote hayatajitokeza tena. Tunahitaji kuona soka letu likiwa na mabadiliko makubwa.
Mwisho kabisa ngoja nizungumze na klabu zetu. Kabla ya kwenda mbali zaidi, niipongeze Simba kwa hatua iliyopiga ya kutengeneza viwanja viwili vya mazoezi kule Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Klabu zingine nanyi fanyeni maendeleo ya miundombinu kwani soka la sasa linahitaji uwekezaji wa namna hii ili kupiga hatua.
KMC nimesikia wanaanza mchakato wa kujenga uwanja wao wa mechi kabisa, wakitimiza hilo, watakuwa wamefanya la maana sana kwani wataepuka kutegemea kutumia viwanja vya watu ambavyo ndivyo hivi vinatumika kwa matumizi zaidi ya soka.
Wenzao Azam wala hawana shida, mapema wamefanya maendeleo ya miundombinu, sasa wanafurahia.
Tunataka tuuanze mwaka 2020 kwa mabadiliko makubwa katika soka letu. Tuiage 2019 iende salama. Pale ilipotupatia mafanikio tuhame nayo, katika changamoto, tuzichukue kama sehemu ya kufikia malengo.
 Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) Wallace Karia kuna mengi amejifunza kupitia uongozi wake na yale magumu yatafutiwe dawa ili mwaka 2020 uwe wa hatua zaidi ya hii ya sasa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic