MAJINA ya wachezaji wanaaowania tuzo za Afrika kwa wachezaji wa Ligi ya ndani yametoka na katika hayo hakuna hata jina moja la mchezaji kutoka Tanzania hili liwape hasira wachezaji wetu kupambana zaidi.
Tunaona wachezaji ambao wametajwa ni jirani zetu kutoka Rwanda ambapo jina la Meddie Kagere anayekipiga Simba limetajwa huku pale Uganda wao jina la Emmanuel Okwi anayekipiga Ittihad limetoka.
Kwa wachezaji wetu wa ndani ni wakati wao wa kangalia wapi wanakwama ama wanakwamisha na nini ili kutafuta majibu sahihi tunataka kuona wakati ujao wanakuwa miongoni mwa majina shiriki.
Kagere ambaye anacheza ligi ya Bongo kukosa mshindani wake si kitu cha kufurahia hata kidogo wapo ambao wanaonyesha kupambana ila kuna kitu kidogo tu huenda wanakikosa ni wakati wa kuzungumza na Kagere awaongezee maujuzi.
Kwa wachezaji wanaokipiga nje jina la nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta lipo yeye anapigana kikumbo na washkaji zake akina Mohamed Salah na Sadio Mane hawa wanakipiga Liverpool, hapa kazi ipo.
Anastahili pongezi na kuongeza juhudi zaidi ya hapo kwani kutajwa kwakwe kwenye orodha hii kunatokana na juhudi akiwa na klabu yake ya Genk ila asisahau kwamba anapaswa kuonyesha juhudi hizo pia akiwa na timu ya taifa.
Samatta anapaswa akumbuke kuwa watanzania hawakulala wakati timu yake ikicheza na Liverpool na walichokifanya waliachana na matokeo ya kufungwa kwao mabao 2-1 wakasepa na bao la kichwa maisha yakaendelea.
Anachotakiwa kufanya ni kuwapa burudani ile ambayo waliisubiri na kuiona akiwa pale Anfield akiwa uwanja wa taifa ama ugenini akifunga mabao ya aina ile ambayo yaliwafanya wasilale kwani amekuwa akionyesha kuna akina Samatta wawili.
Tunamtaka Samatta mmoja anayefunga mabao magumu sehemu ambayo hakuna anayetarajia kwa kufanya hivyo atazidi kuwa gumzo na atafikia malengo zaidi ya hapo ila kama atakuwa anachagua viwanja basi na mafanikio yatamchagulia sehemu.
Yote kwa yote watanzania tunapaswa tuendeleze umoja wetu na kushirikiana katika kila hatua pasipo kubaguana kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Tukirejea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara tunaona kwamba kwa sasa tunaelekea kwenye dirisha dogo la usajili ambalo linatarajiwa kufunguliwa Desemba 16 jambo ambalo linahitaji maandalizi.
Kwa wakati huu kabla ya kuelekea kwenye usajili ni muhimu kwa timu zote kuangalia wapi kuna mapungufu kabla ya kukimbilia kusajili wachezaji ambao wanawahitaji.
Umakini unahitajika kwenye usajili kwani kwa sasa tayari kuna timu ambazo zimeona mapungufu yao yapo wapi na wanahitaji nini kwenye timu zao jambo ambalo ni la muhimu na sio la kubeza.
Ikumbukwe kuwa timu ili ipate ushindi inatakiwa iwe na wachezaji ambao wanaweza kuipigania na kuipa ushindi kama hakuna matokeo itakuwa ngumu kuyapata.
Benchi la ufundi muda huu pia ni lazima kuwa na wale ambao wanafanya skauti kwa ajili ya wachezaji ambao wanahitajika kusajiliwa ndani ya timu.
Ripoti inayoandaliwa inapaswa ionyeshe mapungufu ya kikosi ili kutoa mwanya kwa viongozi kusajili wachezaji ambao wanahitajika ndani ya kikosi.
Kwa wale viongozi ambao hupenda kusajili kwa mhemuko waache suala la usajili mikononi mwa benchi la ufundi jambo ambalo litawapa uwanda mpana wa kutaja majina ambayo yatawapa majibu sahihi.
Ikumbukwe kuwa kuboronga kwao ndani ya ligi wao ndio wamekuwa wakiulizwa kwa nini wanakosa matokeo chanya licha ya wao kushindwa kusajili.
Mfano mzuri ni Ramadhan Nswazurimo, kocha wa Singida United alipohojiwa kwa nini timu inasuasua kupata matokeo alisema kwamba alikuta timu ina wachezaji ambao hawajui.
Ugumu upo kwa kocha kufanya kazi na wachezaji ambao hawatambui kwani anakuwa anaanza kazi upya ya kuunda kikosi na mfumo mpya jambo ambalo halipaswi lifanyike kwa kuwasajilia wachezaji.
Mashabiki wanahitaji burudani na soka la ukweli lile la kukata na shoka na hayawezi kutokea kimiujiza kama benchi la ufundi halijafanya usajili lenyewe.
0 COMMENTS:
Post a Comment