MICHUANO ya
Cecafa kwa wanawake ilimalizika hivi karibunikwenye ardhi ya Bongo na bingwa kuwa Kenya baada
ya kuwafunga wenyeji Tanzania Bara mabao 2-0.
Katika
michuano hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar, ilikuwa na
msisimko mkubwa sana na timu zilizoingia fainali zilionekana kupambana hadi
kufika hapo.
Kama
unakumbuka, Tanzania Bara ambayo maarufu ni Kilimanjaro Queens na Kenya, hadi
zinafika fainali hazikuwa zimepoteza mechi yoyote. Zilishinda zote kuanzia hatua
ya makundi hadi nusu fainali.
Katika
fainali, Kenya iliposhinda ikaondoka kwenye michuano hiyo ikiwa na ushindi wa
asilimia mia moja kwa kushinda mechi zote tano za michuano hiyo. Wanapaswa
kupongezwa kwa hilo.
Kilimanjro
Queens nao licha ya kukosa ubingwa huo, nao wanapaswa kupongezwa kwani
walifanya kazi kubwa sana. Bahati haikuwa upande wao, wakajikuta wakifungwa
fainali.
Maumivu
waliyoyapata wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo, ni sawa na maumivu
waliyoyapata Watanzania wote kwa jumla kwani hakuna ambaye alitarajia kuona
timu hiyo ikilipoteza kombe hilo hapa nyumbani.
Kitu kibaya
ni kwamba, Kilimanjaro Queens imelikosa kombe hilo ikiwa bingwa mtetezi baada
ya kulitwaa mara mbili mfululizo katika nchi za Rwanda na Uganda. Kama
ingelichukua na safari hii, ingekuwa mara ya tatu mfululizo.
Wakati
tukizipongeza timu hizo, pia tuzikumbushe Zanzibar, Djibouti na Sudan Kusini
kufanya maandalizi kabambe kwenye nchi zao ili wakati mwingine zije zikiwa
imara zaidi.
Timu hizo
ndizo zilizofanya vibaya zaidi kwenye michuano hiyo na kudhihirisha wazi kwamba
hazikuwa zimejipanga.
Naweza
kusema kwamba, kilichoibeba zaidi Kilimanjaro Queens ni uwepo wa Ligi Kuu ya
Wanawake na Ligi Daraja la Kwanza Wanawake hapa Tanzania.
Ligi hizo
zimesaidia sana kuwa na timu imara ambayo ikiendelea kutunzwa, itafika mbali na
kushiriki michuano mbalimbali ya kimataifa.
Wakati
Kilimanjaro Queens wakifanya yao kwa upande huo, kaka zao, Kilimanjaro Stars
nao wanajiandaa kushiriki michuano ya Chalenji itakayoanza Desemba 7, mwaka huu
nchini Uganda.
Ni michuano
ambayo Kilimanjaro Stars inapaswa kufanya kweli na kuliletea heshima taifa kwa
kutwaa ubingwa huo.
Tayari Kocha
Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Etienne Ndayiragije ametangaza kikosi chenye jumla
ya wachezaji 32 kikiwa ni cha awali kabla ya baadaye kufanyika mchujo na kubaki
ambao watakwenda kuipeperusha bendera ya nchi kwenye michuano hiyo.
Wachezaji
ambao mmeitwa hivi sasa, tambueni kwamba mna jukumu kubwa la kufanya
kuhakikisha mnaliletea heshima taifa hili.
Kina dada
wamepambana lakini mwisho wa siku wameukosa ubingwa wa Cecafa, kaka zao nanyi
piteni njia sahihi ili mrudishe furaha ya Watanzania iliyopotea.
Watanzania
tutakuwa nanyi bega kwa bega kuhakikisha mnafanikisha malengo hayo na tayari
kuna mipango ya baadhi ya Watanzania wamepanga kwenda Uganda kuishangailia timu
hiyo.
Imani yangu
ni kwamba, wachezaji watajituma zaidi katika kusaka matokeo mazuri, lakini pia
kujitangaza kwani kitakuwa ni kipindi cha usajili wa dirisha dogo hapa nchini.
Dirisha dogo
litafunguliwa Desemba 16, mwaka huu na kufungwa Januari 15, mwakani, hivyo
wachezaji tumieni vizuri michuano hii kujitangaza zaidi.







0 COMMENTS:
Post a Comment