Na Saleh Ally
WISSAM Ben Yedder wa AS Monaco ndiye
anaongoza kwa upachikaji mabao katika Ligue One
ya Ufaransa ambayo huonyeshwa kupitia
king’amuzi cha Startimes akifuatiwa na Moussa
Dembele wa Lyon.
Yedder amefunga mabao 11 baada ya mechi 17 na
Dembele amefunga 10 na hawa ndio wachezaji
waliofunga mabao mengi zaidi hadi sasa katika ligi
hiyo ingawa wanaowafuatia wengi hawako mbali
sana.
Unaona Mholanzi, Memphis Depay wa Lyon pia,
Victor Osimhen wa Lille na Habib Diallo wa Metz,
kila mmoja amepachika mabao tisa.
Hii ndio Tano Bora ya wafungaji wanaongoza kwa
mabao katika Ligue One na unaona hadi hapo
nyota wa PSG bado hawana nafasi.
Ingawa hawako mbali lakini inaonekana wazi kuwa
ushindani kwao umekuwa mkubwa kutokana na
idadi kubwa ya wafungaji wanaokimbizana nao au
kukimbizana wenyewe kileleni.
BEN YEDDER |
Takwimu zinaonyesha wigo wa upachikaji mabao
katika ligi hiyo kuu ya Ufaransa umeongezeka kwa
asilimi 27.4 kwa wachezaji wengi zaidi kufunga
mabao katika timu moja.
Kupia ligi hiyo ambayo huonyeshwa katika
king’amuzi cha StarTimes, wigo pia umetanuka kwa
asilimia 32.2 kwa wachezaji tofauti kufunga badala
ya walewale ambao walikuwa wanategemewa.
Hii maana yake nyota kama Mbappe au Neymar
ambao wamekuwa ndio mastaa wakubwa wa Ligue
One wanalazimika kufanya kazi ya ziada hadi
kurejea katika kiwango kitakachowarejesha katika
ushindani sahihi au waamue kuondoka na kwenda
kuanza maisha mengine katika ligi tofauti.
Gumzo la kwa nini hawako juu katika upachikaji
mabao ni kutokana na kuandamwa na majeraha
kwa muda fulani lakini mjadala umeongezeka kuwa
hata baada ya kurejea, cheche zao si zile
zilizozoeleka au zinazojulikana.
Katika uchambuzi wake, Gazeti la Michezo la
L’equipe limekuwa likisisitiza Neymar ambaye
baada ya kurejea kazini akitokea kwenye majeraha
alionyesha cheche lakini baadaye akachanganywa
na ile isu yake ya kurejea Barcelona ambayo
baadaye ilishindikana.
Inaonekana Neymar alijipanga kuondoka PSG lakini
mambo yaliposhindikana, pia ilimchanganya hivyo
alikuwa na vipindi viwili vilivyomvuruga. Mwanza
akianza na kuelekeza nguvu nyingi kwenye
kuondoka na pili kuchanganywa na kushindwa
kuondoka.
Hii pia inaonekana kwa Mbappe ambaye alikuwa na
nafasi ya kwenda Madrid ingawa pia yeye
anaonekana ana nafasi ya kurudi katika nafasi za
juu kwa kuwa ana mabao saba ya kufunga. Maana
yake ana nafasi ya kufikisha tisa na kwenda kumi
haraka.
Tatizo limekuwa moja nalo ni la kitaalamu ambalo
anatakiwa kulifanyia kazi. Kuwa na mashuti sahihi
na yanayolenga lango.
Ukiangalia anayeongoza kwa upachikaji mabao,
Ben Yedder uwezo wake wa kushuti langoni uko
juu. Amepiga mashuti 32, kati ya hayo 24
yamelenga na 11 ndio amefunga na uwezo wake
wa kulenga tango ni 75%.
DEPAY NA DEMBELE |
Mbappe mwenye mabao saba, yeye amepiga
mashuti 36, kati ya hayo 21. Uwezo wa kulenga
lango amesalia 58%. Na hiki ndicho anachotakiwa
kukiboresha kuhakikisha anarejea na kuwa mmoja
wa washindani wakubwa wa Ben Yedder, Dembele,
Diallo na Depay.
Pamoja na kuonekana kwamba Mbappe anatakiwa
kufanya kazi ya ziada, unaona ndani ya PSG, sasa
tegemeo ni Mauro Icardi. Yeye pia ana mabao
saba, akiwa amepiga mashuti 19, kati ya hayo 11
yamelenga lango.
Neymar naye anarejea, anapanda taratibu ingawa
kila kitu kinaonyesha anatakiwa kuweka gia ya
mlima ili kuukwea mpando ulio mbele yake.
Mbrazili huyo amefunga mabao sita, akiwa amepiga
mashuti 27 langoni na 20 yamelenga lango.
Wastani wake wa ubora ni 67% na wastani mzuri
wa mashuti kulenga lango. Kilichobaki ni
kujirekebisha kuhakikisha mpira unaingia wavuni.
Utaona pia anafukuzana na Dimitri Payet ambaye
ana mabao matano akiwa pia amepiga mashuti 27
lakini yaliyolenga ni 15 na amekuwa na 56% ya
ubora katika upigaji. Hii maana yake, ushindani wa
wafungaji katika Ligue One unazidi kupanda kwa
kiwango cha juu kabisa.
Changamoto hii kwa mastaa kama Neymar na
Mbappe inaifanya Ligue One kuendelea kuinuka
kwa kasi kwa kuwa wafungaji wanakuwa si
walewale kila wakati.
Ushindani unaongezeka na wachezaji wengine
wanaonekana nao kuwa hatari, wanaleta upinzani
na wanaweza kufunga mabao mengi na bora na si
wachache ambao wanajulikana hufanya hivyo mara
nyingi.
Wakati mwingine kwa nyota kama Neymar na
Mbappe, wanapopata ushindani wa namna hii,
ubora wao unaongezeka lakini ni lazima wakati
wakipambana wawekeze akili zao sehemu sahihi.
Kwa hali ilivyo, Mbappe na Neymar ndio wanaanza
kurejea katika Ligue One lakini inawezekana
Januari wakati wa usajili, akili zao “zikakimbia” tena.
Lazima Madrid na Barcelona watawavuruga kwa
mara nyingine. Lazima watataka kujiimarisha na
kama watahusika katika usajili, wanaweza kupoteza
tena uelekeo kwa kuwa ushindani wa wafungaji
umekuwa mkubwa na wenye wigo mpana zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment