LIGI Kuu
Tanzania Bara inazidi kuchanja mbunga huku ushindani ukionekana kuwa mkubwa kwa
kila timu kupambana kupata matokeo chanya ambayo yatawafanya wafikie malengo
yao ambayo wamejiwekea kwa sasa ndani ya ligi pale itakapokamilika.
Tunaona namna
kila timu zinavyoonyesha ule ushindani wa kweli jambo ambalo linamaanisha
kwamba kuna mambo ambayo yanafanyiwa kazi kila iitwapo leo huku ligi yetu
taratibu ikizidi kukomaa licha ya kwenda mwendo wa kusuasua tunastahili kuwapongeza
wale ambao wanapambana katika hili.
Kila mmoja
anayependa mpira hesabu zake ni kuona kwamba timu yake inafanya vema na matokeo
yanapatikana ndani ya dakika tisini uwanjani hili ni jambo la muhimu kuzingatia
kwani ukweli ni kwamba matokeo yanapatikana ndani ya uwanja na sio nje ya
uwanja.
Kumekuwa na
baadhi ya timu zimekuwa zikipenda kujihusisha na masuala ambayo yanaonyesha
dalili za ushirikina hili sio sawa kwani kwa teknolojia ilivyokuwa kwa sasa
kuna mambo mengine ambayo yalikuwa yanafanywa nyuma yaachwe tu.
Tumeona
kwenye Ligi Daraja la Kwanza kuna kesi kama hii ambapo Rhino Rangers inadaiwa
walifanya vitendo hivi na kesi imepelekwa kwenye Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) hii ni kupotezeana muda tu.
Kwa timu
ambayo inatambua inahitaji nini ni lazima ijipange na kufanya maandalizi mazuri
jambo pekee ambalo linatoa ushindi kwa timu husika ambayo inasaka matokeo
uwanjani.
Kwa wale
ambao bado wapo kwenye zama zile wanapaswa washtuke na kufanya kweli kuanzia
kwenye maaandalizi na kujiamini kwamba wanaweza kufanya mambo makubwa bila
kuamini mambo ambayo hayapo kwenye mpira.
Pia masuala
ya kuanza kuwa na hofu mapema maana yake ni kwamba tayari umeshashindwa soka
kuna jambo jingine ambalo unaweza kulifanya nje ya soka kiushindani.
Ligi zote
zinapaswa ziwe na ushindani ila sio kushindana kwa masuala ya madawa na
ushirikina hapana haitakuwa ni ushindani wa kweli kwani kila mchezaji atakuwa
haonyeshi uwezo alionao.
Ni sawa na
mwanafunzi ambaye anaingia kwenye chumba cha mtihani akiingia na vile vibomu
hawezi kufanya mtihani kwa kujiamini muda wote anakuwa na mashaka huenda
atakamatwa jambo ambalo ni kosa kwa kweli.
Muda wa
maandalizi timu zinapaswa kuutumia vema kwa kujiandaa na kuachana na masuala ya
nguvu za giza ambazo zinaonekana kuwamaliza kimyakimya wale ambao hawajajiandaa
kwa umakini.
Soka letu
linakua na linapiga hatua endapo kutakuwa na mwendelezo wa vitendo hivi ni
mwendelezo wa kufeli na kushindwa kupata vipaji vya kweli kisa ushirikina.
Pia kumekuwa
na vurugu ambazo hazina msingi hasa huku kwenye Ligi Daraja la Kwanza ilitokea
kwenye mchezo kati ya Pamba na Gwambina FC hili pia nalo wadau mnapaswa
kulikemea na kukataa hali hii.
Ugomvi si
asili ya soka kwa kufanya ugomvi tunapoteza ule uhalisia wa soka na kuja na
jambo ambalo tunalitambua wenyewe huku kunapoteza muda na kumaliza nguvu za
wale ambao wanapenda burudani.
Kwenye soka
ni muda wa kutazama nani anafanya vizuri nani anafeli ili kutafuta suluhisho
kwenye mchezo unaofuata sasa ikiwa kila sehemu kitu kidogo watu mnakunjana
mashati sio sawa.
Ingekuwa
vema mashabiki muda ambao mnakunjana mashati mgekuwa bize kutafuta wadhamini
ambao watawekeza kwenye soka huku ambako kuna vipaji vya kweli ila mnashindwa
na kukimbilia ugomvi.
Imeonekana kuna shabiki amechomwa na kitu cha
ncha kali mpaka umwagaji wa damu unafanyika kwenye soka hivi vitu tulishaanza
kuvisahau kutokana na ustaarabu wa watanzania nashangaa kuona vinarudi.
Kinachotakiwa
kwa sasa ni kukaa chini na kumaliza tofauti kabla ya kufikia hatua hii naona
kwenye ligi daraja la kwanza kwani hali si shwari kwa sasa.
Kuna malalamiko kuhusu waamuzi kwenda na
matokeo yao uwajani katika hili basi suluhisho linatakiwa mapema kabla halijawa
sugu.
Waamuzi mnapaswa
mjichunguze na kazi yenu iwe moja tu kufuata sheria 17 za soka hata kama
mnachezesha Ligi Daraja la Kwanza kwa kufanya hivyo zile lawama na zile kelele
za mashabiki zitakwenda na maji jumla huku soka letu likizidi kuimarika.
Mashabiki
pia nanyi mnapaswa kutambua kwamba mwamuzi naye ni binadamu kuna wakati
anakosea kuweni na busara sio kosa la mwamuzi basi mnahamishia hasira kwa
mashabiki hili haileti afya kwenye soka.
Umakini
katika kila sehemu unahitajika ili kupata kile ambacho kila mmoja anakihitaji
endapo kila mmoja atashindwa kuwa makini matokeo yake ni kushindwa kuelewana na
kugombana bila sababu.
Pia
ukiachana na hayo mashabiki tunapaswa tukumbuke kuwa michuano ya kufuzu Afcon
kwa timu yetu ya Tanzania mchezo wake wa pili iliboronga kwa kufungwa mabao 2-1
na Libya mchezo uliochezwa nchini Tunisia.
Kufungwa
kwao sio mwisho wa safari bado kuna mechi zinaendelea ni wakati wa kuendelea
kuipa sapoti timu yetu ya Taifa kwa kuwapa moyo wachezaji.
Kwa
wachezaji nao wana deni na kazi ya kufanya kwa kujiandaa vema ili kupata
matokeo kwenye mechi zao zinazofuata kila kitu kinawezekana endapo watajiandaa
vema.
Ni suala la
muda tu kwani kwa sasa kundi J bado lipo wazi kwa kila timu bado kuna nafasi ya
kupenya na kushiriki kwa mara nyingine Afcon ili kujiongezea ujuzi na uzoefu
mara dufu.
Nina amini
tayari kocha Etienne Ndayiragije ameona mapungufu ya wachezaji yalipo pamoja na
makosa yao yanavyowamaliza jambo ambalo litaleta matokeo chanya wakati ujao.
Muda wa
maandalizi upo kwani michuano hii mikubwa ina hadhi yake kwa timu ambazo
zitatinga kwenye hatua hii ni jambo la kusubiri na kujaandaa kuweza kushiriki
kwa mara nyingine tena.
0 COMMENTS:
Post a Comment