January 30, 2020


MAKOCHA wengi wa Bongo wanapenda sana kujisifia kwa kazi nzuri lakini wanakuwa wagumu kukubali pale wanapokosea. 
Hayo yapo kwa kila binadamu, wengi wetu hatutaki kukubali makosa bali tunatafuta njia ya kuhakikisha tunaliepuka na kuonekana kuwa ni la mtu mwingine tofauti kabisa.

Inapotokea kukawa na kitu cha kusifiwa basi hapo ndipo tunapenda kwelikweli, haya ndiyo maisha yetu wengi. 
Lakini hii ya kukimbia makosa inafika wakati lazima tukubali makosa ili kuweza kujifunza na kuimarika zaidi na zaidi kwenye maisha ya kila siku.

 Kocha wa Singida United, Mrundi, Ramadhan Nsanzurwimo alionyesha njia kwa makocha kwa kukiri kutenda kosa na kubebeshwa lawama baada ya kufungwa mabao 3-1 na Yanga Uwanja wa Namfua. 
Namnuku kocha huyo: “Nimekubali kubeba lawama kwa kupoteza mchezo huu kwa sababu nilikosea kupanga timu kwa maana kuna wachezaji niliwaamini, lakini hawakufanya kama vile nilivyotaka wafanye.” Mwisho wa kunukuu.

Hapo unaona kabisa kuwa yeye ndiye anayestahili lawama na amekubali kulaumiwa na kubwa zaidi ni kwamba ameamua kuwa mkweli kitu ambacho wengi wetu hatukitaki. 
Tunakwama sana kwenye mfumo wetu wa kuendesha soka kwa sababu wengi wetu tunadanganya mno na kupenda kulaumu watu pale tunapotenda kosa hasa waamuzi.

Kocha yule Mrundi hakutaka kumbebesha lawama mwamuzi wa mchezo wala uongozi, yeye akaenda moja kwa moja kuwa kosa alifanya mwenyewe kwa uzembe wake na kukubali kubeba msalaba ule wa kufungwa na Yanga mabao 3-1. 
Tunataka watu kama akina Nsanzurwimo kwenye soka letu ili watusaidie sana kwa sababu uongo sio mzuri kwenye kila jambo ingawa watu wengi wa kwenye soka la Bongo kuongopa ni kitu cha kawaida kwao.

Makocha wetu wengi wajifunze kwenye hilo, yaani kama timu zao mbovu wakubali kuwa timu zao mbovu na wamefungwa kwa udhaifu wa timu zao au kama wamefanya makosa wakubali kuwa wao makocha ndio wamekosea na sio kila mara kuwashushia lawama waamuzi. 
Maana waamuzi ndio wamekuwa watu wa kuangushiwa jumba bovu kila kukicha, hata kama timu zao zimefungwa kwa makosa ya wachezaji wao wenyewe makocha lakini watawatwishwa waamuzi.

Siku zote tunajifunza kutokana na makosa na muda ni huu na tayari kocha wa Singida United ameonyesha mfano tena ni mfano mwema kwenye maendeleo ya soka letu. 
Hiki kitu ningependa kukiona kikiendelea zaidi kwani kitawafanya hata wale makocha ambao wanakuwa wanajificha kwenye kivuli cha waamuzi kwa ubovu wa timu zao nao waone aibu na kuzungumza ukweli kama ni wachezaji walimuangusha au ni upande wa mwamuzi, iwe kweli.

Soka linachezwa kwa uwazi, mwamuzi akizingua watu wanaona na kama timu inacheza chini ya kiwango pia huonekana, hakika Nsanzurwimo ameonyesha utofauti mkubwa kwa makocha, hivyo kila mmoja sasa anapaswa kubadilika.
 Lawama kwa waamuzi zipungue na watu wapige kazi ili kuhakikisha soka letu linapiga hatua zaidi.

2 COMMENTS:

  1. Umetumwa na MOOOOOOOO!Haya nenda kapokee bahasha yako

    ReplyDelete
  2. Mwandishi waamuzi wanaboronga Sana na Tff hii inajisifu Sana kwa mafanikio makubwa .

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic