January 7, 2020








NA SALEH ALLY
MECHI ya Dabi ya Kariakoo ilikuwa tamu sana kutokana na kasi, idadi kubwa ya mabao, yaani manne yaliyopatikana katika mchezo mmoja na matatu katika kipindi cha pili.


Utamu ulikuwa zaidi kwa kuwa dakika 45 za kipindi cha pili zilikuwa na mabao matatu na yote yakifungwa ndani ya dakika 10 za kwanza za kipindi hicho.


Utamu zaidi wa mechi hiyo ni matokeo ya mwisho ambayo hayakutarajiwa na wengi hasa wanaoisapoti Yanga lakini kuna mambo haya kumi, huenda uliyaona lakini huyakumbuki!

1. Wageni 9 uwanjani Kariakoo Dabi
Vikosi viwili vya Simba vyenye wachezaji 22, viliundwa na wachezaji wa kigeni tisa, wenyeji Simba wakianza na wageni sita na Yanga watatu.

Wageni sita wa Simba walikuwa ni Tairone Santos, Serge Wawa, Deo Kanda, Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata na kwa upande wa Yanga wageni watatu ni Farouk Shikalo, Papy Tshishimbi na Haruna Niyonzima.


2. Tairone kiboko kwa vichwa
Beki Tairone Santos wa Simba, alipiga mipira mingi ya vichwa hasa kipindi cha pili na kumfanya kuwa mchezaji aliyepiga mipira mingi ya vichwa katika mchezo huo.

Mbrazili huyo, alipiga karibu mipira yote 16 aliyoruka juu kuokoa. Mipira 15 aliifikia na mmoja tu ndiyo aliozidiwa kupiga.


3. Viungo 5, wakata umeme 3!
Kocha Charles Boniface Mkwasa aliamua kuanza na mshambuliaji mmoja tu, Ditram Nchimbi huku akitumia viungo watano akionyesha wazi alikuwa na plani nzuri na hakupanga kushambulia katika kipindi cha kwanza.

Katika viungo hao watano ambao ni Abdulaziz Makame ‘Bui’, Mohamed Issa ‘Banka’, Mapinduzi Balama, Papy Tshishimbi na Haruna Niyonzima ‘Generali’, watatu kati yao yaani Bui, Banka na Tshishimbi walifanya kazi ya kukaa na mpira, kuchezesha lakini zaidi kukaba kwa lengo la kutibua mipango yote ya Simba mahususi kama wakata umeme.


4. Simba bila mgeni benchini
Benchi la Simba lenye wachezaji saba halikuwa na mgeni hata mmoja huku wazalendo wote saba wakiwa wamekalia ubao akiwemo nahodha John Bocco.

Yanga benchini ilikuwa na wachezaji wawili wageni ambao ni Patrick Sibomana kutoka Rwanda na Yikpe Gnamien raia wa Ivory Coast.

Waliokuwa benchi la Simba ni wazalendo Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Erasto Nyoni, Hassan Dilunga, Ibrahim Ajibu na Bocco. Wakati kwa Yanga ukiachana na Gnamieni na Sibomana, wazawa walikuwa ni Metacha Mnata, Feisal Salum, Deus Kaseke na Mrisho Ngassa.


5. Mkwasa na wapya wa dirisha dogo First Eleven
Licha ya presha kubwa katika Kariakoo Dabi, Kocha Mkwasa, aliamua kuwachezesha wachezaji wapya watatu ambao walisajiliwa wakati wa dirisha dogo lililofunguliwa mwezi uliopita. Watatu walioanza ni beki wa kushoto Adeyum Saleh, kiungo Haruna Niyonzima na mshambuliaji Ditram Nchimbi na baadaye akamuingiza Yikpe Gnamien. Kumbuka, Simba hawakutumia mchezaji hata mmoja mpya aliyesajiliwa wakati wa dirisha dogo.


6. Kagere alimalizia akaanzisha, Bocco, Nyoni wakiwa benchi
Kama unakumbuka mechi ya mwisho msimu uliopita, Simba ilishinda bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mechi ambayo bao lilifungwa na Kagere. Msimu huu, amekuwa wa kwanza kufunga na kuwa mchezaji aliyefunga mabao mawili ndani ya mechi mbili za Yanga.

Pamoja na hivyo, wachezaji wawili tegemeo wa Simba waliokuwa katika mechi hiyo ya msimu uliopita Erasto Nyoni na Bocco ambaye alitoa pasi ya bao la Kagere msimu uliopita, walianzia kwenye ubao. Bocco aliingia baadaye lakini Nyoni akamaliza dakika 90 aishuhudia mtanange ubaoni.



7. Wachezaji watatu waliokuwa katika benchi la Simba, walicheza msimu uliopita wakiwa Yanga na mechi moja au mbili dhidi ya Simba

Wachezaji hao ni Gadiel Michael na Ibrahim Ajibu ambao walicheza mechi mbili za msimu uliopita wakiwa Yanga dhidi ya Simba na mechi ya juzi wakabaki benchi hadi dakika 90 zinafikia tamati.

Mchezaji wa tatu alikuwa ni Kakolanya ambaye pia alimaliza dakika 90 akiwa benchi. Kama unakumbuka mechi ya mzunguko wa kwanza msimu uliopita alikuwa shujaa kwa kuizuia Simba kushinda akiokoa michomo mingi ya kina Kagere na kuwa shujaa wa mchezo huo.

Mzunguko wa pili, hakuwa Yanga wala Simba baada ya kutoelewana na uongozi wa Yanga kuhusiana na malipo.



8.   The best Come Back
Mabao mawili ya Yanga ya kusawazisha yalifungwa ndani ya dakika tatu tu na kuandika rekodi ya kuwa “The Best Come Back” kwa maana ya haraka zaidi.

Yanga ikiwa nyuma kwa mabao 2-0, ilipata bao safi la mkwaju matata wa Mapinduzi Balama katika dakika ya 50 lakini dakika ya 53, Mohamed Zimbwe akajifunga akiokoa krosi matata ya Adeyum. Ndani ya dakika tatu, Yanga ikawa imerejea mchezoni na kuwatoa kabisa Simba mchezoni.


9. Mkwasa imara kwa kuwaacha Molinda, Sibomana
Ujasiri wa Mkwasa kuwaacha wakali benchi, jukwaani
Kocha Mkwasa wa Yanga, alionyesha ujasiri wa hali ya juu akiamua kuwaacha wachezaji wake wawili tegemeo waliokuwa kiongozi wa mashambulizi na utengenezaji mabao katika mechi zilizopita.


Patrick Sibomana akiwa tegemeo la utengenezaji mabao lakini mfungaji, alikuwa benchi, jambo liliwashitua wengi.

Kama haitoshi, mfungaji bora wa Yanga, Mkongoman, David Molinga na mabao yake manne, alikaa jukwaani kabisa na hii huenda ingekuwa hatari sana kwake kama angepoteza mchezo huo.


10. Mataifa saba, Dabi moja ya Kariakoo
Makocha wa vikosi viwili vya Simba na Yanga, waliwatumia wachezaji 22 walioanza na 14 walio benchi kutoka katika mataifa saba.

Ukiachana na Watanzania waliokuwa wengi zaidi, wageni walitoka katika mataifa mengine sita tofauti ambao walicheza au kukaa benchi katika mechi hiyo ya Dabi ya Kariakoo.

Tanzania ndilo taifa lililotoa wenyeji wengi zaidi lakini mataifa mengine yaliyotoa wachezaji ni Kenya, Rwanda, DR Congo, Ivory Coast na Zambia na yote yakiwa ni mataifa ya Bara la Afrika na taifa moja la Amerika Kusini ambalo ni Brazil.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic