January 7, 2020





NA SALEH ALLY
NILIWAHI kuandika mara kadhaa namna ambavyo wapenda mpira wa Tanzania wengi tulivyo wanafiki na tunaovutiwa na kukurupuka katika mambo mengi tusiyoyajua.
Nimewahi pia kuelezea namna mashabiki wengi wa soka, tulivyo na tabia ya kuwa wafuata mkumbo kwa kuwahukumu watu katika makosa ambayo tumesikia, hatujachunguza wala kufanya angalau uchunguzi kidogo baada ya kusikia lakini mwisho tunahukumu.

Huenda anayesema ana jazba au anayesema ana chuki na mchezaji anayemsema, basi ilimradi tu, basi tunaingia kama bendera fuata upepo na kulishikilia bango.

Nasema hivi wazi kuwa kwa wale wanaolia leo kuwa kipa wa Simba, Aishi Manula anapaswa kuondolewa, wangependa kuona anayedaka ni Beno Kakolanya na kigezo eti kwa kuwa Manula kafungwa mabao mawili dhidi ya Yanga.

Kati ya wanaosema, hakuna anayethubutu kueleza kwa ufasaha akiyachambua yale mabao mawili kiufundi kuturidhisha kuwa kweli ni makosa makubwa ya Manula ambayo yanahitaji hukumu.
Hakuna anayelalamika kuhusiana na aliyepokonywa mpira mguuni kabla ya Mapinduzi Balama kuondoka nao, akionyesha alikuwa akitaka kupiga pasi lakini akaachia mkwaju mkali ambao hakuna aliyeutarajia kulinagana na sehemu aliyokuwepo lakini pia hata muonekano wa umbo lake.

Pamoja na hivyo, anayesema Kakolanya adake, ana uhakika angeweza kuokoa shuti hilo. Jaribu kutuliza akili, rudia mchomo huo matata wa Mapinduzi na namna Manula alivyokwenda, sema tuone kama kweli ni kosa lake.


Vizuri kufanya uchunguzi kabla ya kulalamika tu kwa jazba. Manula alifanya kazi yake vizuri, nimejiridhisha, rudia ile video uone uhalisia. Acha mihemko kwa kuwa tu umesikia na ukumbuke, Manula ni kipa na si ndege mwenye mabawa, ulipokwenda mpira ni mara chache kipa kutokea kuuokoa na inategemea aina ya mpira ulivyokwenda na position aliyopo, punguzeni lawama tu bila kusifia.

Bao la pili, Manula kafungwa na beki wake, nahodha wake Mohamed Hussein Zimbwe ambaye alikuwa anajaribu kuokoa. Kwa kuwa Mohamed Issa ‘Banka’ alimsukuma kwa nyuma ilikuwa vigumu kwake kuwa na direction nzuri ya kuupiga ule mpira.

Wakati anasukumwa, Zimbwe akawa amepoteza uelekeo. Hivyo mpira ukaenda upande wa Manula ambaye ulikuwa kama umemshitukiza, alijaribu kuuokoa ukamzidi kasi.

Unamlaumu aliyejaribu kuokoa wakati beki wake akimfunga? Ingekuwa lawama basi aliyejifunga lakini katika mpira tunaamini alikuwa akijaribu kuokoa, ni bahati mbaya, tunaocheza mpira tunasema bad lucky.

Sasa iweje aliyejaribu kufuta kosa la aliyejifunga aonekane ndiye mwenye makosa makubwa zaidi. Kama aliyejifunga mmeona ni bad lucky vipi aliyejaribu kufuta kosa la mwenzake ikashindikana ndiye anaonekana alikosea sana?

Kipa hujiandaa sana anapoona mpira uko kwa mpinzani ingawa si asilimia 100 ndio ataokoa. Lakini inapotokea mpira uko upande wao, huamini ni salama. Bila shaka Manula alijua Zimbwe anaokoa na yeye anatengeneza position ya kuangalia kama kuna mpira utakaorudi tena aokoe, lakini anashtukia tayari Zimbwe amepiga kichwa cha chini cha kushindilia, mpira unakuja kwake kwa kasi.

Inawezekana Manula akawa na makosa kama mchezaji lakini hastahili adhabu mnayotaka kumpa na mkumbuke, mlifanya hivi kwa Kaseja, mkamlazimisha kuisha, mkafanya aonekane mzee, sasa mmeanza kwa Manula.

Kawaida sisi Watanzania hatupendi kuambiana ukweli, hatupendi kuwaona watu fulani waking’ara kwa muda mrefu. Sasa Kaseja anawasuta wengi wenu ingawa mmejikausha na wengine mmekuwa mstari wa mbele kumsifia kama vile hamkushiriki kumzeesha kwa lazima.

Itakuwa vizuri mkajipambanua mapema, ili siku moja Manula akiwa shujaa wa Simba na taifa, basi tuwakumbushe kwa majina na kuwaonyesha mihemko yenu haina faida.


Makocha wa Simba wanajua wapi wanamhitaji Manula, wapi wanamhitaji Kakolanya na ndio maana leo yuko Simba. Msiwashinikize wakaifanya kazi yao kwa matakwa ya mashabiki badala ya weledi wa kazi yao, acheni mihemko, acheni kulia na msivyovijua, mkiachiwa hivi, kesho mtasema Simba imsajili Farouk Shikalo, kisa kaokoa sana dhidi ya Simba…halafu! 

4 COMMENTS:

  1. Manula ajirekebishe la sivyo ni yeye mwenyewe ndie atakae jizeesha na hata Juma kaseja alijasahau pale simba kwa kufanya kazi kwa mazoea na mwisho wake ndio hivyo tena. Simba au Yanga ni timu zenye presha na mara nyingi presha ipo kubwa zaidi kwa viongozi kuliko wachezaji. Ila la kushangaza akili za wachezaji wetu wengi wa kibongo wakishafika kwenye timu yenye maslahi kama Simba hupumzika na kujisahau baada ya kujituma zaidi na kuonesha utofauti na thamani ya kazi yao kutoka pahala walipotoka na walipo sasa. Jitihada huoneshwa na wachezaji wetu pale tu wanapowania kusajiliwa na Simba lakini wakishafika utashangaa kama ni mchezaji yule yule aliekuwa akiisumbua Simba wakati akiwa ndanda au lipuli. Yuko wapi salamba na wengine wengi wakimuacha babu kagere akipeta. Deo Kanda akizidi kuteleza,mzee wawa akisahihisha makosa ya mwanae tshbalala kula kukicha akijikongoja kukomaa. Huku Mgeni Tyrone silver asieijua Simba wala uchungu wake,kama si yeye mechi ile ya watani wa jadi basi Simba ingeibika kama ingetegemea wachezaji wenye Simba yao. Na kwanini huoni makala ikizungumzia yule Mbrazil kwenye mechi ile Jamaa alipiga mpira mkubwa mno katika backline ya simba.

    ReplyDelete
  2. washabiki wengi uelewa wao ni mdogo hakuna kosa lolote la kumwangukia Manula waliofanya makosa wanajulikana ila kwa sababu watu wamekariri au wanatafuta sababu ndio wanamgeukia manula kosa la goli la kwanza ni Mzamiru wakati la pili anayewajibika ni Mohamed Husein

    ReplyDelete
  3. tatizo la sisi watanzania tunajua sana mpira wa mdomoni kuliko uhalisia

    ReplyDelete
  4. Manula anatakiwa kuzungumza na mabeki wake kabla ya hatari kosa la shabalala ni la pili mechi tofauti. Hilo ndilo kosa lake hazungumzi kuwapanga mabeki wake.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic