January 7, 2020





Na Saleh Ally
KABLA sijaendelea, anayepishana na mimi kuhusiana na kwamba nyota wa mchezo katika mechi ya Simba dhidi ya Yanga alikuwa benchi, anyooshe mkono!

Ninamaanisha hivi, Kocha Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa, maarufu kama Master au Masta, ndiye alikuwa nyota wa mchezo huo ulioisha kwa sare ya mabao 2-2 na kuwashangaza wengi hasa walioamini eti Simba itashinda 5-0!

Wakati ilionekana mapema kuwa mechi hiyo ilikuwa nyepesi sana kwa Simba kutokana na mwenendo wa rekodi za mechi zilizopita za Ligi Kuu Bara, Mkwasa hakuonekana kuwa na hofu sana.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Mkwasa alisisitiza mambo mawili makubwa, kwanza waamuzi kuchezesha kwa haki lakini pili kuwa vijana wake wamejiandaa na wako tayari watapambana.

Baada ya mchezo huo, Mkwasa akasema jambo ambalo hakulisema katika mkutano kabla ya mechi. Kwamba pamoja na kujua wapinzani wao wana kikosi bora, kikubwa walijua ni dhaifu katika utimamu wao wa miili na kipindi cha pili wanaonekana wanakufa mapema. Hivyo walijiandaa.

Hapa ndiyo mchezo unaanzia na mwisho unajua kabisa kuwa Mkwasa alijiandaa na kuonyesha kitu kikubwa sana. Kwamba makocha Wazalendo kuna jambo fulani wanaliweza lakini wanashindwa kabisa kulifanyia kazi na ikiwezekana kujiachia siku moja wakaenda kufundisha nje.

Siku nne kabla ya mechi hiyo, Mkwasa aliwakimbiza wachezaji wake ile mbaya. Kwa kocha wa kigeni mfano wa Sven Van der Broeck raia wa Ubeligiji lisingewezekana lakini kwa Mkwasa, mambo yaliwezekana kwa kuwa kuna kitu alitaka kuongeza katika utimamu wa wachezaji wake na uliona, Yanga walikaba kwa dakika 90 bila ya kuchoka.

Kitaalamu, Mkwasa alikubali udhaifu wa kikosi chake, akaheshimu ubora wa Simba lakini akatafuta kwa kuuchokonoa udhaifu wa Simba ulipo, alipofanikiwa katika hili akaanza kulifanyia kazi.

Angalia alichokifanya, wakati alianza mechi akiwa na mshambuliaji mmoja tu, akatundika viungo watano ndani ya kikosi chake kwa maana ya kupunguza mshambuliaji mmoja na kuingiza kiungo, kwa hiyo alianza na 3-5-1-1 kwa maana ya mfumo na kiungo wa juu alikuwa akishuka zaidi kukaba huyu alikuwa Papy Tshishimbi.

Katika viungo hao watano, watatu ambao ni Abdulaziz Makame, Mohamed Issa ‘Banka na Haruna Niyonzima wakafanya kazi zaidi ya kukaba na wa mwisho akawa ni Mapinduzi Balama ambaye licha ya kukaba alipandisha pia mashambulizi.

Unaona, Mkwasa alijua kabisa alihitaji watu wa kukaa na mpira na watu wa kutibua mipango ya Simba ambao kama utawaachia wakapiga pasi nyingi ndani ya dakika moja, unawapa nafasi ya kukupa madhara.

Ukiangalia vizuri Yanga haikupanda kabisa katika kipindi cha kwanza, walitoa nafasi ya Simba kwenda upande wao, na wao wakapambana kuwakaba kwa nguvu na kuuchukua mpira.

Kawaida iko hivi; timu inapobaki katika zone yake, maana yake kunakuwa na wachezaji wao 11, wapinzani wanaposhambulia kama wataingiza wachezaji nane katika hiyo zone maana yake kutakuwa na wachezaji 19 katika nusu ya uwanja. Hii inafanya uchezaji unakuwa mgumu na kupunguza nafasi ya ufungaji mabao. Mkwasa aliitumia hii kuwanyima Simba kutengeneza nafasi nyingi.

Ukiwaangalia Simba namna ya uchezaji wao ni kasi na open football. Mkwasa aliiminya hiyo, aliwazuia Simba kukimbia sana na unaona, mabao mawili ya Simba yote yamepatikana kwa aina hiyo ya kushambulia kwa kasi ambayo iliwazidi nguvu Yanga.

Inaonekana wazi, vijana wa Mkwasa walikosea maelekezo na Simba hawakufanya ajizi. Hata hivyo, Mkwasa hakuwaruhusu vijana wake kurudia tena makosa hayo na unaona baada ya kuwadhibiti Simba, dakika za mwisho plani ilikuwa ni ile aliyoisema, kuwa Simba hawako fiti watachoka.

Mwisho Yanga wakashambulia zaidi na pia kukaba zaidi wakionekana wako fiti na Simba wakiwa kama wamechoka na kupunguza kasi.

Mkwasa amewahi kukutana na Simba akiwa mchezaji, mwenyewe hupenda kujisifia kuwa alishawafunga. Akakutana na Simba akiwa kocha kabla ya jana, pia aliwahi kukutana nao akiwa kiongozi, kaimu katibu mkuu. Kwake hakukuwa na jipya sana na hii ilimsaidia kuidhibiti presha.
Ingekuwa vigumu sana kwa mtu asiyejiamini au asiye na hofu na mechi hiyo kukubali kuwaacha nje Patrick Sibomana na David Molinga ambao ni tegemeo zaidi katika mechi zilizopita.

Licha ya mabao manne aliyeifungia Yanga, Mkwasa alijua watakaba zaidi na Molinga asingekuwa msaada katika hili kama Banka au Tshishimbi. Akamtuliza jukwaani kwa kuwa hakumhitaji sana siku hiyo. Kama haitoshi, Sibomana ambaye angeweza kutoa pasi za mabao, pia hakumhitaji sana hasa kipindi cha kwanza alichowaachia Simba kiwe chao na kweli mipango yake imefanikiwa kwa asilimia 95, ndiyo maana nasema mechi hiyo ya sare ya 2-2, nyota wa mchezo alikuwa ni Master Mkwasa, akiwa benchini.














5 COMMENTS:

  1. Hayo ni maoni ya akili yako? kigezo ni takwimu za mchezo ball possession, direct on target shoot, corners..Kipindi cha kwanza chote kachezewa robo uwanja..kwa sababu kabahatisha kurudisha magoli ndiyo kocha bora.Sisi tunataka mechi irudiwe tena Zanzibar tuone ubora wa Mkwasa anayeshinda kwa kubahatisha 1-0 karibuni kila mechi

    ReplyDelete
  2. Huyo jamaa anajipa raha yeye mwenyewe hafichi unazi wake kwa Yanga

    ReplyDelete
  3. Kukurukeni weee mwisho ni hapa: Yanga alisawazisha magoli mawili dhidi ya Simba. Kama kubahatisha hata Simba alibahatisha aliporudisha magoli matatu katika sare ya 3-3. Mnanuna nini, huu ndiyo mpira..

    ReplyDelete
  4. Jamani kama Yanga ingeshinda ile mechi hali ingekuwaje? Yaani Wanaojiita mabingwa wa kihistoria wanasheherekea na kujisifu kwa ushindi wa sare? Mnafahamu yakwamba Yanga ilizidiwa kila idara karibu muda wote wa mchezo? Kati ya Mkwasa na Yanga yake na kocha wa mwadui na timu yake nani Shujaa mbele ya simba?

    ReplyDelete
  5. kinachoendelea Yanga hakina tofauti na Ndanda pamoja na kocha wao walioshangilia kufungwa mbili.Yanga inapaswa kushangilia kwani walichomoa na kama hata nusu ya bao walizokoswa koswa kipindi cha kwanza zingeingia! Mkwasa sio bora ni kama Zahera tu aliyekuwa anabahatisha kwani likuwa ana
    anapata bao la kuongoza kuanzia dakika ya 70 na kuendelea..Tizama mechi na Prison halafu na ya biashara eti uniambie masta

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic