January 26, 2020


Kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael, amesema kuwa hapendi kuzungumzia uwezo wa mchezaji mmojammoja wa timu yake lakini kiwango ambacho amekionyesha kiungo mshambuliaji Mghana Bernard Morrison kimemfanya ashindwe kujizuia huku akitamka jamaa ni hatari akiamini ni tegemeo hivi sasa katika timu.

Kauli hiyo aliitoa kocha huyo mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara, juzi kwa Yanga kufanikiwa kuwafunga Singida United mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Namfua mkoani Singida huku Morrison akihusika katika mabao mawili huku moja akitengeneza asisti kwa Mnyarwanda Haruna Niyonzima.

Mshambuliaji huyo anayetumia miguu yote alikuwa mchezaji wa mwisho kusajiliwa na Yanga katika usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15, mwaka huu akivaa jezi kwa mara ya kwanza alionyesha kiwango kikubwa huku akionyesha vitu vingi mguuni ikiwemo kasi, ubunifu na msumbufu kwa mabeki.

Baada ya mchezo huo, Luc alisema kuwa amefurahishwa na aina ya uchezaji wa Morrison katika
mchezo huo huku akimtabiria nyota huyo kuifikisha katika nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ambalo ndiyo lengo.

Alisema mshambuliaji huyo hajacheza muda mrefu lakini ameonekana akicheza vizuri tofauti na matarajio yake huku akiamini akipata muda zaidi atakuwa na msaada mkubwa katika timu hiyo inayopiga hesabu kubwa ya kuwapoka ubingwa wa ligi watani wao, Simba.

Aliongeza kuwa ana aina ya wachezaji wa Morrison ambao kama angejiunga mapema na timu hiyo kabla ya usajili wa dirisha dogo kufungwa, basi angekuja nao wawili na kikosi chao kingekuwa tishio katika ligi. 

“Mara nyingi nimekuwa nisipendi kuzungumzia uwezo wa mchezaji, lakini niseme kuwa mashabiki wa Yanga watarajie mengi kutoka kwa Morrison kwani akiwa na muda mchache na timu
ameonekana akifanya makubwa katika mchezo wake wa kwanza wa ligi.

“Huu ni mwanzo mzuri kwake, hivyo wasubirie mengi mazuri kutoka kwake, anaonekana ni mchezaji atakayetoa msaada mkubwa katika timu ni baada ya leo (juzi) kuonyesha kiwango kikubwa katika mchezo huu na Singida United ambao ulikuwa mgumu kwetu.

“Ninaamini Morrison akipata muda mrefu wa kukaa na timu pamoja ataonyesha kiwango kikubwa zaidi ya hiki ambacho amekionyesha, kikubwa mashabiki waendelee kumsapoti.

“Katika usajili huu bahati mbaya nilichelewa kujiunga na timu, lakini kama ningewahi kujiunga na timu, basi ningesajili wachezaji wengine wawili wenye uwezo mkubwa kama alionao Morrison,” alisema Luc.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic