January 29, 2020


NAMUNGO ya Lindi itakuwa na kazi ya kuendeleza ubabe wao ndani ya Ligi Kuu Bara wakiwa na kumbukumbu ya kupindua meza kibabe mbele ya Tanzania Prisons kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Samora.
Namungo iliyo chini ya Hitimana Thiery ilishinda mabao 3-2 baada ya kipindi cha kwanza Prison kuwa mbele jambo ambalo lilimuacha mdomo wazi Kocha Mkuu wa Prisons, Adolf Rishard.
Kazi kubwa, Uwanja wa Taifa leo, saa 1:00 usiku itakuwa ni kutafuta pointi tatu ili kuweka rekodi ya kumpoteza kocha mpya wa Simba, Sven Vandebroeck ambaye hajaonja uchungu wa kupoteza pointi tatu.
Mechi ya mwisho, Simba ilishinda kwa jumla ya mabao 4-1 mbele ya Alliance, Uwanja wa CCM Kirumba jambo linaloongeza  hali ya kujiamini kwa wachezaji.
Utamu wa mechi ya leo utabebwa na mambo haya yafuatayo Uwanja wa Taifa :-
Rekodi mpya kwa Sven na Hitimana
Kwenye jumla ya mechi sita ambazo amekaa benchi, Sven ameshinda tano na kulazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 na Yanga jambo ambalo linazidi kumpasua kichwa katika kuendeleza rekodi yake.
Hitimana yeye inakuwa mara ya kwanza kukutana na vigogo hawa ambao ni mabingwa watetezi. Endapo atafanikiwa kumfunga Simba leo itakuwa ni rekodi ya kwanza kwa Namungo kushinda mechi yao ya kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara mbele ya Simba.
Namungo ilipanda daraja msimu wa 2019/20 na ni mechi yake ya kwanza mbele ya Simba.
Vita ya mabao
Namungo kwenye jumla ya mechi 15 ilizocheza imejikusanyia jumla ya mabao 18 huku wapinzani wao Simba wakiwa wamefunga jumla ya mabao 35. Kwenye mechi sita alizosimamia Sven ndani ya Simba amefunga mabao 16.
Hitimana alisema kuwa anahitaji kukusanya mabao mengi zaidi kwa sasa ili kuwaongezea wachezaji wake hali ya kujiamini huku Sven alisema kuwa wachezaji wake wanashindwa kufunga mabao mengi kutokana na kutojiamini.
Makocha waliongoza mechi zao za awali wamepigwa chini
Ilikuwa ni Agosti 12,2018 na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Wakati huo Simba ilikuwa chini ya Patrick Aussems na Namungo ilikuwa chini ya Frugence Novatus.
Uwanja wa Majaliwa zilikutana mara moja ulikuwa ni mchezo wa kirafiki mpaka dakika 90 zinakamilika ngoma ilikuwa ngumu kwa pande zote mbili hakuna mbabe aliyeona lango la mpinzani.
Kila kocha ataingia akiwa ni mgeni kwa mwenzake jambo ambalo litaongeza hasira kwa makocha wote wawili kutafuta matokeo.
Tambo za makocha
Sven alisema kuwa hana cha kupoteza kwenye mechi zake za ligi kutokana na ugumu uliopo kwenye kupata matokeo.
“Ligi ni ngumu na kila timu inapambana kupata matokokeo. Sitakuwa na furaha ya kupoteza mchezo ilihali wachezaji wana uwezo wa kuonyesha kitu cha kipekee. Kikubwa ni kuwaheshimu wapinzani na kupambana kutafuta pointi tatu.
Hitimana wa Namungo alisema kuwa hana hofu na timu kubwa kwani wachezaji wake wameanza kujiamini kutokana na kushinda kwa mechi zao.
“Mechi zetu tulizoanza kutoka nje na kupata ushindi zimetuongezea hali ya kujiamini. Sina hofu kwani nina amini itakuwa ni kazi kutafuta pointi tatu.
Nafasi zao ndani ya ligi
Simba ipo nafasi ya kwanza imecheza mechi 16 ikiwa na pointi 41 itamenyana na Namungo iliyo nafasi ya 5 imecheza mechi 15 na ina pointi 28.
Ushindi wa Namungo utaipandisha kutoka nafasi ya tano jumla mpaka nafasi ya tatu huku Simba ikishinda itaendelea kujijengea ufalme wake nafasi ya kwanza.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic