IBRAHIM Ajibu, Kiungo mshambuliaji wa Simba jana Uwanja wa Taifa aliiokoa Simba usiku mikononi mwa Polisi Tanzania kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara wakati Simba ikishinda mabao 2-1.
Ajibu ambaye alikuwa hana makuu ndani ya uwanja alifunga bao hilo akimalizia pasi ya Francis Kahata dakika ya 90+5.
Hili ni bao la kwanza kwa Ajibu ambaye ana jumla ya asisiti nne za Ligi Kuu Bara na alikuwa kinara msimu uliopita kwa kupiga jumla ya pasi 17 za mabao aliingia dakika ya 46 akichukua nafasi ya Sharaf Shiboub.
Polisi Tanzania ilianza kwa kasi kipindi cha kwanza na kufunga bao la kuongoza dakika ya 22 kupitia kwa Sixtus Sabilo, ambaye alisepa na kijiji cha mabeki wa Simba, Haruna Shamte na Kennedy Juma na kuachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango Beno Kakolanya.
Mpaka wanakwenda mapumziko Simba ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 na walirejea uwanjani wakianza kuliandama lango la Polisi Tanzania.
Iliwachukua Simba dakika 56, kufunga bao la kwanza kupitia kwa John Bocco akimalizia pasi ya Clatous Chama.
Ushindi huo unaifanya Simba kubaki nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 50 kibindoni na Polisi Tanzania inakuwa nafasi ya saba ikiwa imekusanya pointi 30 kibindoni na zote zimecheza mechi 19 za ligi.
Huu ni ushindi wa 16 kwa Simba ambayo inaongozwa na Sven Vanderbroeck raia wa Ubelgiji na ina sare mbili huku ikichapwa mechi moja mbele ya Mwadui FC bao 1-0.
Simba walifanya mabadiliko makubwa ya kikosi chao kutokana na ratiba kuwabana ambapo Ijumaa watachezaji na JKT Tanzania.
Leo Yanga watakuwa Uwanja wa Taifa saa moja usiku kuvaana na Lipuli kwenye mchezo mwingine mkali wa ligi hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment