February 9, 2020

HUKO mtaani wanasema waamuzi hasa wanaochezesha mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ni janga la soka letu.
Kelele hizo zimekuja hivi karibuni baada ya kutokea kwa matukio mfululizo yaliyozua utata, makubwa zaidi ni ya kushindwa kutafsiri vema sheria ya kuotea.
Nikiri wazi kwamba, kama mwamuzi hautakuwa makini wakati unachezesha mechi, suala la kuitafsiri sheria ya kuotea itakupiga sana chenga hasa pale inapotokea wachezaji wawili wanaocheza timu tofauti wanapokuwa karibu sana huku mmoja akizidi.
Hii sheria inahitaji umakini mkubwa sana kuitafsiri ikitokea ishu kama hiyo, wapo waamuzi ambao ni makini wanaoitafsiri sheria hiyo vizuri tu, lakini wengine kwao ni changamoto.
Katika pitapita zangu huku na kule nimesikia kwamba waamuzi wana madai yao, hawajalipwa kwa muda mrefu.
Wapo wanaosema kwamba ishu hiyo ya kudai inaingiliana na hiki kinachofanywa, wapo waliofika mbali zaidi na kuhusisha na suala la rushwa, eti kuna waamuzi wanatumika na baadhi ya timu.
Sijathibitisha hilo, lakini kama lipo, basi si uungwana, naamini haiwezi kuwa hivyo kwa sababu waamuzi wamefundishwa jinsi ya kuepuka vishawishi ambavyo vitaharibu kazi yake.
Kwa haya yaliyotokea, sihitaji kuwalaumu zaidi waamuzi, lakini kikubwa ninachoomba itafutwe dawa ya kuondoa haya malalamiko ya kila kukicha.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT) pamoja na ile Kamati ya Waamuzi, kukaa chini na kutatua hili tatizo.
Inawezekana kuwafungia isiwe dawa ya moja kwa moja kwa sababu unaweza kuwafungia waamuzi wengi, mwisho wa siku ligi itakuwa na uhaba wa waamuzi, hapo pia ni tatizo.
Ligi inatakiwa kuwa na waamuzi wa kutosha kwa maana ya kwamba mwamuzi mmoja asiwe na lundo la mechi, kama ikitokea mwamuzi mmoja akachezesha mechi nyingi, nalo ni tatizo.
Huko nyuma nilishawahi kusikia watu wakisema kuna mwamuzi fulani yeye amechezesha mechi nyingi za timu fulani tu, hilo halileti picha nzuri hata kidogo.
Nimalizie kwa kuziasa timu zinazoshiriki ligi hiyo kucheza kwa umakini mkubwa hasa mzunguko huu wa pili ambao ni wa lala salama.
Ukiangalia hivi sasa Simba inaongoza ligi hiyo, inafuatiwa na Azam, kisha Yanga inashika nafasi ya tatu. Timu hizi ndizo zimeonekana kila msimu zinawania zile tatu bora kwenye msimamo.
Mzunguko wa pili siku zote unakuwa na changamoto zaidi ya ule wa kwanza kwa sababu hapa unaweza kukuta na ratiba inabana zaidi.
Tazama hivi sasa timu kama Yanga kuna mechi mbili za mzunguko wa kwanza haijacheza, hivyo mzunguko huu wa pili ina kazi ya kucheza mechi nyingi zaidi na muda mdogo.
Hivyo lazima timu hiyo itakuwa na ratiba iliyobana zaidi. Hapa kama timu haijajiandaa vizuri, kuna hatari ya kupoteza pointi kirahisi.
Kama timu inawania ubingwa, lazima icheze kwa malengo. Kwanza kuhakikisha nyumbani inashinda, kisha ugenini iambulie angalau pointi moja na si kupoteza kabisa. Ikiwezekana kuondoka nazo zote.
Pia tukumbuke kuna timu za kushuka daraja, kama hazijajipanga vizuri, tunaweza kuzishuhudia zikishuka hata kabla ya msimu kumalizika, hivyo lazima zijipange.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic