TIMU ya Gwambina imesema inafahamu kuwa itakutana na Yanga kwenya hatua inayofuata ya michuano ya Kombe la Shirikisho hivyo wamejipanga kuhakikisha wanawafunga na kutimiza malengo ya kucheza nusu fainali ya michuano hiyo.
Gwambina imefikia hatua hiyo baada ya kuwaondosha Ruvu Shooting kwa penalti 7-6 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye muda wa kawaida.
Yanga wao waliwatoa Prisons kwa mabao 2-0. Akizungumza na Championi Jumatano, Katibu Mkuu wa Gwambina, Danieli Donald amesema kuwa wanawaheshimu wapinzani wao lakini bado wana deni la kufikia malengo yao kama klabu.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu kwani ni klabu yenye mafanikio makubwa nchini na Afrika kiujumla, lakini nasi kama klabu tunayo malengo ambayo tumejiwekea tangu kuanza kwa msimu huu.
“Moja kati ya malengo hayo ni kuhakikisha tunafika angalau katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Shirikisho, hivyo tutapambana kuhakikisha tunafikia malengo hayo bila kuangalia tunacheza na nani,” alisema Donald.
0 COMMENTS:
Post a Comment