February 3, 2020





Na Saleh Ally
KOCHA Dean Smith wa Aston Villa, aliamua kufanya mabadiliko ya mapema katika dakika ya 58 katika mechi dhidi ya Bournemouth wakiwa nyuma kwa mabao 2-0.

Alimtoa Anwar El Ghazi raia wa Uholanzi na nafasi yake ikachukuliwa na Mwingereza, Keinan Davies ambaye kama unakumbuka katika mechi ya Carabao dhidi ya Leicester City, aliingia kuchukua nafasi ya Mtanzania, Mbwana Samatta.

Mabadiliko hayo yalikuwa msaada mkubwa kwa Villa ambao walipata bao likifungwa na Samatta baada ya kuuwahi mpira uliookolewa na beki wa Bournemouth. Hili bao limeifanya Tanzania kuwa nchi ya 99 raia wake kufunga bao katika EPL.

Pamoja na kupoteza mchezo huo kwa mabao 2-1, takwimu zinaonyesha Villa walitawala kila idara na kiungo wake mchezeshaji, Jack Grealish ndiye alikuwa mchezaji bora wa mechi. Lakini Watanzania wanalia naye kila upande kwamba alikuwa akimnyima pasi Samatta.

Grealish ni mchezaji tegemeo zaidi ya Samatta na amekuwa msaada mkubwa katika kikosi hicho na kamwe hajawahi kulalamikiwa kwa uchoyo kwa kuwa takwimu ndio uhalisia. Lakini Kibongobongo, watu wanalia hadi katika mitandao ya Klabu ya Aston Villa ambalo si jambo zuri.

Unaposema mchezaji mchoyo ni yule asiyefikisha pasi kwa wenzake. Pasi nazo zina aina nyingi, inawezekana zile kwa ajili ya kuchezesha timu, kulinda au kusaidia kutengeneza bao kwa maana ya asisti.
Katika takwimu za Ligi Kuu England, Grealish wao wanamuita “Mtoto wa nyumbani”, anaongoza kwa mabao akiwa amefunga saba akifuatiwa na Wesles mwenye matano halafu Anwar El Ghazi aliyefunga manne.

Upande wa pasi za mwisho, yaani asisti, Grealish anaongoza akiwa na tano, akifuatiwa na El Ghazi mwenye nne halafu Frederic Gulbert aliyetoa mbili. Maana yake si kweli kuwa hataki wenzake wafunge kwa kuwa yeye ndiye aliyetoa pasi nyingi zilizozaa mabao ya timu hiyo katika msimu huu wa EPL.







Kwenye pasi ambazo zimefika, Grealish anaongoza tena akiwa na 800, akifuatiwa na beki Tyrone Mings mwenye 747 na Douglas Luiz aliyepiga 572. Kama ndiye aliyetoa pasi nyingi zaidi ya wengine, vipi tuamini kuwa hataki kutoa pasi au anamnyima Samatta? Ni fikra potofu ambazo wengine tumezibeba kwa hisia za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kama angekuwa mchoyo wa pasi, basi asingekuwa na asisti nyingi, sasa anaongoza. Kama angekuwa hatoi asisti, bado asingekuwa mchoyo kwa kuwa kapiga pasi nyingi zilizofika kuliko mchezaji yeyote wa Villa.

Mfano mzuri wa pasi zilizofika ni ile maridadi aliyompa Samatta katika mechi ya Carabao Cup dhidi ya Leicester ambao sote tulikiri kuwa Samatta hakutulia, akaipoteza.

Hakuna hata mmoja amesikika akisifia ile pasi maridadi aliyopewa na Grealish ambayo inakuwa kati ya pasi 800 zilizofika za kiungo huyo. Kama Samatta angefunga, basi leo Grealish angekuwa na pasi 799 na asisti 8. Lakini bahati mbaya Samatta hakuwa ametulia na inawezekana utofauti wa soka la England akiwa mgeni kwa mara ya kwanza.

Ukiachana na hivyo, bao la Samatta la kwanza katika mechi ya kwanza ambalo limetengeneza faraja kwa Watanzania, lilianzia kwa Grealish baada ya kupokea pasi ndefu, akawalaghai mabeki wa Bournemouth na kupiga pasi safi ya chini iliyofika kwa Davies ambaye aligeuka na kupiga shuti kali lililozuiwa na mpira ukamfikia Samatta, akafanya yake.

Hakuna ubishi kadiri wanavyokwenda wanazoeana, kila mmoja atajua mwenzake anachezaje na kuanza kupeana pasi zaidi kwa kuwa mikimbio ndio namna ya kujua mchezaji mwenzako anacheza vipi.

Pamoja na hivyo, kila wanavyozidi kucheza, itakuwa rahisi wa Kocha Smith kuendelea kuwapa mipango na kupanga njia za kumfikishia mipira mingi Samatta kwa njia rahisi zaidi au inayowahadaa zaidi wapinzani.

Si kweli Grealish anaweza kumnyima mipira Samatta, hasa akijua wazi wako katika wakati mgumu na kunahitajika mtu wa kumalizia kazi zake nzuri.

Kwa wenzetu takwimu bora si mabao pekee, asisti zinakuza soko la mchezaji, pasi zilizofika zinaongeza bei yake. Hivyo Grealish kama play maker, anazihitaji na angependa kuona mabao mengi yanatokana na pasi zake nzuri zaidi.

Bila shaka, msimu ujao wa Premier League atakuwa mmoja wa wachezaji watakaotakiwa na klabu kadhaa kutokana na ubora anaouonyesha, hivyo tusianze kuwaza Ki-Ligi Kuu Tanzania Bara, hali ya wengi kuona kulaumu ndio kuuzungumzia mpira.
Kama una takwimu zinazoonyesha Grealish alimnyima Samatta pasi ngapi, onyesha kama huna achana na mawazo hayo potofu na kataa kuwa bendera fuata upepo na ikiwezekana sasa tuendane na Samatta, tuwe na mawazo ya Ki-Premier League.

Mwisho nikukumbushe, kadiri Samatta na Grealish wanavyozidi kuzoeana katika chemistry ya uchezaji, mabao mengi ya Samatta yatatokea kwa kiungo huyo mchezeshaji hatari na matata kabisa.










4 COMMENTS:

  1. Umeongea ukweli bro, hata Samatta nae amesema ilo. Tunaonekana kweli hatujui soka lilivyo

    ReplyDelete
  2. Umeongea ukweli bro, hata Samatta nae amesema ilo. Tunaonekana kweli hatujui soka lilivyo

    ReplyDelete
  3. Tatizo la uelewa mdogo wa wapenzi wa Hamida fc,na ndio maana Rage aliwaita Mambumbumbumbumbumbu

    ReplyDelete
  4. Umeongea kiufasaha kabisa, tatizo la WaTz wengi hawajui wanachokisemea,longolongo nyingi, wengi hufuata mkumbo lkn kwa uhalisia hawana maarifa ya kutosha

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic