Jumamosi iliyopita kikosi cha Simba kilipambana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mbrazili, Gerson Fraga, lakini washambuliaji wa timu hiyo, John Bocco pamoja na Meddie Kagere kamwe hawatamsahau kipa wa Coastal Union, Sud Abdallah kwa kile alichowafanyia.
Kabla ya mchezo huo, Abdallah alimwambia kocha wake mkuu, Juma Mgunda kuwa atafanya kila liwezekanalo asifungwe na Kagere lakini pia Bocco ili aweze kuandika rekodi katika maisha ya kutofungwa na wachezaji hao ambao alidai kuwa ni washambuliaji wanaotisha kwa sasa katika ligi kuu.
Hata hivyo, mpango wake huo alifanikiwa kuutimiza kwani alifanya kazi kubwa ya kuzuia michomo iliyokuwa ikipigwa na washambuliaji hao jambo ambalo liliwafanya baada ya mechi hiyo kumalizika, wamfuate na kumpongeza.
Abdallah alisema kuwa anajivunia rekodi yake hiyo, lakini pia anasikitika kwa kufungwa mabao mawili na Fraga.
“Niliweka nadhiri kabla ya mechi kuwa nitahakikisha Bocco na Kagere hawanifungi na nimeweza kufanya hivyo, hakika najivunia hilo lakini nasikitika pia kufungwa na Fraga mabao mawili.
“Bao la kwanza alilofunga, nilikosea hesabu kidogo tu za kuuwahi mpira wa faulo uliokuwa umepigwa na Chama (Clatous Chama), lakini lile la pili naweza kusema kwamba mabeki wangu walikosa umakini kidogo.
“Baada ya mimi kupangua shuti la Hassan Dilunga walitakiwa kuuondoa katika eneo la hatari, lakini walichelewa na kumkaba Fraga ambaye alikuwa peke yake akafanikiwa kunifunga bao la pili, nampongeza pia kwa hilo,” alisema Abdallah.
0 COMMENTS:
Post a Comment