WAKATI
mwingine nyakati zinabadilika na ni muhimu pia kwa wale ambao wanaishi kwenye
nyakati kukubali mabadaliko na kwenda nayo kasi ili yasiwaache.
Nakumbuka
wakati ule nikisoma msemo wa polepole ndiyo mwendo pamoja na kawia ufike
ilikuwa inatumiwa sana na kutupa nguvu kwamba tunaweza kufanya mambo yote kwa
kuwa muda upo.
Jambo ambalo wakati mwingine lilikuwa
linatufanya tushindwe kuyatimiza majukumu yetu kwa wakati na kuhstuka kukiwa
kumepambazuka.
Haina maana
kwamba tunapaswa tufanye mambo yote kwa harakaharaka hapana kila kitu
kinahitaji umakini mkubwa ambao utatufanya tupate matokeo mazuri.
Ukweli
unabaki palepale kwenye Ligi Kuu Bara hata huko England timu ambayo ina
uwekezaji mzuri inapata matokeo bora kwa kuwa mpira wa sasa ni pesa.
Ipo wazi kwa
sasa kasi ya Singida United inazidi kuporomoka na kwa hapa walipofikia
wanapaswa waanze kujiandaa kisaikolojia namna ya kurejea tena kwenye ligi
wakati mwingine tena.
Kuna timu
ambazo zilipanda daraja na kucheza msimu mmoja ziliposhuka hazijaweza kurudi
kutokana na ushindani uliopo kwenye Ligi Daraja la Kwanza lakini kwa Singida
United ni miujiza inahitajika ili kuona inabaki ndani ya ligi.
Tangu ligi
kuanza haijawahi kuthubutu kuwa ndani ya tano bora hata mara moja pamoja na 10
bora jambo linaloonyesha kuna hatari ambayo imefika mlangoni inasubiri kuingia
ndani.
Uzuri ni
kwamba kila ambaye unamtazama aeleze sababu ya kukwama kwao hakuna ambaye
anakueleza kwa ufasaha zaidi ya sababu ambazo zinawekwa wazi na mwalimu kwamba
ni umakini mdogo wa wachezaji ambao wanao.
Suala kubwa
kwa sasa ni ukata ambao unaimaliza Singida United lakini kuna nyakati ilikuwa
inapitia kipindi cha neema wakati huo jicho la viongozi wa Singida United
lilikuwa linatazama nini mbele?
Kiongozi
yupo kwa ajili ya kutengeneza matatizo na kuyatatua kwa wakati sasa hapo ndipo
uongozi wa Singida United unapaswa ukae chini utazame wapi hesabu zilianza
kuwakataa kabla ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza.
Inawezekana
wadhamini ni tatizo lakini hakuna mdhamini anayeweza kuwekeza sehemu ambayo
hakuna ushindani timu icheze nyumbani inafungwa iwe ugenini inafungwa hili
linazidi kuongeza ukakasi.
Kupoteza
mbele ya Coastal Union na kupoteza mbele ya Tanzania Prisons kwa mechi za hivi karibuni kunaifanya Singida United kufikisha mechi 19 ambazo
zimepotea mbele wapinzani wao hili ni balaa.
Kwa zile
ambazo zimepanda msimu huu zinapaswa zitambue kwamba maisha ndani ya ligi
hayana muda mreufu iwapo hakutakuwa na mipango makini ambayo itakuwa inafanyiwa
kazi kwa vitendo.
Labda
Singida United hawajatambua kwamba msimu huu timu nne zinashuka jumlajumla
labda bado wanavuta kasi lakini kwa wakati huu wasikazane kumtafuta mchawi
wapambane kutafuta matokeo.
Kushika nafasi
ya 20 ukiwa umepoteza mechi 18 baada ya kucheza mechi 26 na kujiwekea kibindoni
pointi 12 ni hatari kwa afya ya soka la timu husika tathimini inapaswa ifanyike
kwa upesi.
Ninaona
kwamba kama maisha ndani ya ligi yamekuwa magumu namna hii endapo watashuka
daraja watatumia muda mwingi kujipanga kurudi, ni wakati wao wa kuweka wazi
kile kinachowasibu kwani timu nyingi zinapitia kipindi kigumu lakini
zinaonyesha utofauti kwa kupambana ili kupata wawekezaji.
0 COMMENTS:
Post a Comment