March 7, 2020



HAKUNA mtu ambaye angeielewa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania  (TFF) endapo ingemfungia kiungo wa Simba, Jonas Mkude na mshambuliaji wa Yanga, Bernard Morrison kabla ya mechi ya watani wa jadi.

 Tanzania ni nchi ya Simba na Yanga. Makocha wetu wazawa wote  wamegawanyika kwa Simba na Yanga. Wabunge wote wamegawanyika, kama sio Yanga basi atakuwa Simba.

 Hata Askari wanaolinda Uwanja wa Taifa pale Temeke, wote nao wamegawanyika. Isingewezekana kabisa kwa nchi hii Jonas Mkude na Bernard Morrison wafungiwe kuelekea mechi ya watani wa jadi.

Ni ngumu kwa sababu hata wajumbe wenyewe wa Kamati ya Nidhamu nao wamegawanyika. Kundi hili liko Simba, kundi lile liko Yanga. Kwenye mechi za ligi kuu Tanzania Bara wiki chache zilizopita, Jonas Mkude na Bernard Morrison walifanya matendo Uwanjani kila mmoja kwa nyakati tofauti yaliyobeba dhana ya utovu wa nidhamu.

 Maswali ya wadau wengi wa Soka ilikuwa ni kama tafsiri ya Sheria ni msumeno kama bado ipo kwenye mpira wa Tanzania. Jibu ni hakuna.  Bado mpira wetu unaendeshwa na VichembeChembe vya kishabiki.

Kuanzia mlinzi wa getini pale Uwanja wa Taifa mpaka mwamuzi wa Kati, wote ni mashabiki wa hizi timu. Kuanzia kwa Wabunge mpaka waendesha Bodaboda, wote wanashabikia hizi timu.


Ni vigumu sana kuwaadhibu Mkude na Morrison kabla ya mechi hii. Ungekuwa kwa wenzetu Ulaya, Sheria ingechukuwa mkondo wake. Hawa wachezaji wawili kwa nyakati tofauti walionekana kufanya utovu wa nidhamu haradhani kabisa kwa kuwapiga kiwiko wapinzani wao Uwanjni lakini mpaka leo ni stori tu.



 Hakuna mwenye nia ya dhati katika hili. Pomoja na Simba kuwa na wachezaji wengi bora kwenye idara ya kiungo lakini Jonas Mkude ni mchezaji tegemeo zaidi kwenye eneo la Ulinzi wa chini. Pamoja na Yanga kuwa na mawinga wengi, Bernard Morrison ndiyo mtambo wa kutembea juu ya mpira pale Jangwani.

 Isingewezekana hata siku moja wachezaji hawa waadhibiwe kabla ya mechi ya Taifa kupigwa.

Ushabiki huu unaumiza sana wachezaji wa timu nyingine. Adhabu zinatakiwa kutolewa kwa wakati na usawa pale mtu atakapobainika. Mambo yemekuwa yakienda kombo haswa watuhumiwa wanapokuwa ni Yanga au Simba.

 Hakuna wa kuwatetea wachezaji wa Mtibwa sugar, hakuna wa kuwatetea wachezaji wa Singida United. Nchi yote iko kwa Simba na Yanga tu! Kama Mkude na Morrison watakutwa na hatia wanatakiwa kuadhibiwa. Hakukuwa na sababu za msingi kwa wachezaji hawa kutosikiliza kesi zao. Kamati ya kumfungia Jonas mkude na Bernard Morrison kuelekea mechi ya hapo kesho, nadhani iko Ulaya tu.

Kuna vitu vingi vizuri vimeanza kuimarika kwenye Mpira, mfano ni mechi hii ya Simba na Yanga ya kesho ambayo tiketi zimeana kuuzwa wiki moja kabla ya mechi. Ni hatua nzuri. Ni jambo zuri. Bado kuna mambo mengi siku ya mechi husika nayo yanapaswa kuwekwa sawa. Mtu mwenye tiketi ya V.I.P. A basi akakae V.I .P A kulikuwa na usumbufu mkubwa sana mechi ya mzunguko wa kwanza ambako watu wengi walikuwa na ticket mkononi lakini hawakupata nafasi za kukaa.

Kamati zinazosimamia mpira wetu waache kutanguliza ushabiki mbele, kwa kufanya hivyo tutajikuta tumewajenga vibaya wachezaji wa Yanga na Simba ambao kimsingi ndiyo wanaongoza kwa wingi linapokuja suala la timu ya Taifa. Morrison na Mkude kama wamekosea wanapaswa kuadhibiwa kwa wakati kama wanavyofanyiwa wachezaji wengine.

 Hakuna haja ya kubebana bebana. Sheria ni msumeno, wachezaji wote ni sawa. Hawa wachezaji wangekuwa wanacheza Soka Ulaya, hakuna kiongozi yotote wa Soka ambaye angejali ukubwa wa mechi iliyoko mbele.

 Sheria ingechukuwa nafasi yake. Wakati mwingine wachezaji kama hawa wakijua kwamba wanapofanya matendo maovu watakosa mechi kama hii, inaweza kuwasaidia wakawa na nidhamu kuliko kuendelea kuwabeba kila siku kwa sababu za Kishabiki tu.



4 COMMENTS:

  1. Nchi yetu,siasa yetu kila kitu vimeingiliwa na ugonjwa wa Corona

    ReplyDelete
  2. Ni kweli kabisa, hapa ndipo uozo wa soka letu ulipo. Kuna haja ya kuwa na mijadala huru juu ya mambo kama haya, lazima mambo kama haya yakemewevkwa nguvu zote na vilabu vingine lkn tatizo hata hao viongozi wa vilabu vingine ni wadau wa Yanga au Simba, hapo ndipo unaoochoka.

    ReplyDelete
  3. Tff hamna kitu mbovu kuliko maelezo

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic