MCHEZO wa
watani wa jadi, Yanga na Simba siku zote huwa na matukio mbalimbali iwe ndani
au nje ya uwanja.
Kama utakuwa
umesahau, kumbuka mchezo wa mzunguko wa kwanza namna ulivyokuwa. Kulikuwa na
matukio mengi ya ndani na nje ya uwanja.
Ya nje ya
uwanja hufanywa na mashabiki na yale ya ndani ya uwanja wahusika wakuu ni
wachezaji, makocha na waamuzi.
Katika mchezo
wa kwanza, lawama nyingi zilikwenda kwa waamuzi, baadhi ya wachezaji na wasimamizi
wakuu wa ligi ambao ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi.
Mwamuzi wa
kati Jonesia Rukyaa alitupiwa lawama kutokana na baadhi ya matukio yake
kuonekana ya utata, lakini pia upande wa wachezaji, wale wa Simba wengi ndiyo
walitupiwa lawama. Upande wa Yanga walisifiwa.
Unajua kwa
nini, wale wa Yanga walisifiwa sana kutokana na kusawazisha mabao na mwisho wa
siku matokeo kuwa 2-2. Awali walifungwa 2-0 na ilionekana Simba inaweza
kuongeza mengine na kuibuka na ushindi, lakini ikakwama.
Simba
wachezaji wao, Mzamiru Yasin na Aishi Manula waliingia kwenye lawama wakitajwa
kwamba wamesababisha kupatikana kwa sare hiyo.
Kelele
zilipigwa sana hasa katika lile bao la kwanza lililofungwa na Balama Mapinduzi
ambaye alimpokonya mpira Mzamiru, kisha akaachia shuti la mbali sana
lililomshinda Manula. Hapo ndiyo Wanasimba wengi waliona kuna makosa.
Wanasahau
kwamba katika mchezo wa soka matukio ya namna hiyo yanatokea kwa bahati mbaya.
Sidhani kama kuna mchezaji yeyote wa Simba au Yanga akipewa nafasi anacheza
chini ya kiwango kwa makusudi ili tu kuigharimu timu yake. Wote wanacheza kwa
moyo mmoja kusaka ushindi.
Sasa yale
yaliyotokea tuache kama yalivyo, tuangalie mambo mengine kuelekea mchezo wa
kesho Jumapili.
Yanga safari
hii watakuwa wenyeji wa Simba katika mchezo huo wa kesho Jumapili utakaochezwa
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Niwasihi
kila mmoja kwa nafasi yake kufanya kile ambacho kitakuwa bora ili kuufanya
mchezo huu kuwa wa kuvutia zaidi.
Kwa
wachezaji, kila atakayepata nafasi acheze kwa kujituma kwa nia ya kuitafutia
timu yake matokeo mazuri.
Makocha nao wapange
vikosi vizuri, waamuzi wachezeshe kwa kuzitafsiri vema sheria 17 za soka,
lakini pia, watu wa usalama nao waifanye kazi yao vizuri kuwadhibiti wale
mashabiki wakorofi. Pia mashabiki na nyinyi kuweni wastaarabu.
Hivi unawezaje
kutoka nyumbani kwako kisha unaenda uwanjani kwa lengo la kufanya fujo tu. Huo
si uungwana hata kidogo.
Kila mmoja
wetu anatarajiwa kuona soka safi na la kuvutia, sasa asitokee mmoja kati ya hao
niliowabainisha akatibua mambo.
Kwa kiasi
kikubwa pambano la watani wa jadi linapokaribia mambo mengi ya ajabu huzuka na
kuanza kuleta presha kubwa na kuondoa ile ladha halisi ya dabi hii kubwa Afrika
Mashariki na Kati.
Vitendo vya
kishirikina vimekuwa vikitawala sana kuelekea pambano hili, pia kumekuwa na
lawama kwa timu hizi kufanyiana hujuma. Hayo yote yasipewe nafasi.
Ni imani
yetu kubwa sisi wadau wa soka tutashuhudia zaidi soka la kuvutia na siyo
vimbwanga ambavyo kwa kiasi kikubwa vitaharibu ladha ya pambano hili lenye
hadhi yake Afrika.
Kila la heri
kwenu, aliyejiandaa vizuri naamini ndiye atakayevuna matunda mazuri.
0 COMMENTS:
Post a Comment