March 5, 2020


MBWANA Samatta nyota wa timu ya Taifa ya Tanzania ameweka rekodi mpya kwenye ulimwengu wa soka duniani kwa kucheza mchezo wa kwanza wa Kombe la Carabao na kuonyesha maajabu yaliyojificha kwenye kichwa chake kwa muda mrefu.
Ni jambo ambalo wengi hawajaweza kutarajia kwamba kijana kutoka Mbagala angeweza kuwasumbua wazungu ambao wao wanaamini katika vile ambavyo wanavyo ila Samatta ameonyesha kwamba nasi pia tunaweza.
Kazi kubwa aliyofanya ilikuwa inatazamwa na watanzania wote kiujumla kwani dakika 90 wanaopenda mpira walikuwa kwenye luniga wakitazama mchezo wa Kombe la Carabao ambapo Manchester City ilikuwa inamenyana na Aston Villa.
Samatta alitumia dakika 41 kufunga bao la kwanza kwa kichwa akimalizia pasi ya Anwar El Ghazi na kurudisha nguvu kwa wachezaji wa Villa ambao walikuwa nyuma kwa mabao mawili.
City iliyo chini ya Pep Guardiola ilianza kutikisa nyavu za Aston Villa dakika ya 20 kupitia kwa Sergio Aguero na Rodri Hernandez alipachika bao dakika ya 30.
Kuna kitu ambacho kinapaswa kiwe vichwani mwa wachezaji wetu wa Bongo ni kutambua kwamba kazi ya kufikia mafanikio ni ngumu na njia yake si nyepesi kama ambavyo wengi wanafikiria.
Kuna mengi ya kufanya kufikia mafanikio kwani kwa wale ambao hawapendi kupitia ugumu wa njia zao inakuwa rahisi kubaki pale walipo maisha hayataki uchaguzi bali yanahitaji kujituma.
Licha ya timu yake kukosa kutwaa ubingwa ila kijana Samatta ameonyesha njia ya kupiga kazi kwa utofauti na ulimwengiu kwa sasa umetambua kuwa kuna kijana anaitwa Samatta mtaalamu wa mibichwa mikali.
Kwa hatua ambayo amefikia kumbukumbu zinaonyesha kwamba amewatungua makocha wote bora ndani ya Ligi Kuu England kwa kichwa na hana habari kijana anapambana.
Liverpool ile inayoongoza Ligi Kuu England ikiwa chini ya Jurgen Klopp ilikutana na kichwa chake hiyo ilikuwa wakati huo akikipiga timu ya Genk ya Ubelgiji kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ni mchezaji ambaye anajua thamani yake kuwa ndani ya uwanja na kufanya kazi kwa kujituma bila kukata tamaa hili liwe somo kwa wachezaji wetu wa ndani.
Kila la kheri Samatta huko uliko usiache kupambana kwa kuwa watanzania tupo tunakutazama na dua njema tunakuombea kwa kuwa umefungua nia na wengine watafuata.
Turejee  sasa Bongo nchi ambayo kila  mwezi inakuwa na jambo lake litakalokufanya usiamini kile unachokiona kutokana na matukio kuwa tofauti kila iitwapo leo.
Timu ya Tanzania ya Wanawake chini ya miaka 17, imeweza kupata ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Uganda ni hatua nzuri na inahitaji pongezi kwa hapo ambapo imefikia.
Kila jambo ambalo mnalifanya mwanzo lina manufaa hapo baadaye kwani ushindi wenu mlioupata unamaanisha kwamba mmefungua njia kuelekea kwenye mafanikio hasa kwenye mchezo wa  marudio utakaopigwa nchini Uganda.
Kushiriki Kombe la dunia sio hatua nyepesi ni kubwa na ngumu hivyo hata upatikanaji wake pia ni mkubwa na mgumu ili kuwa kwenye mazingira mazuri ni lazima muendelee kupambana kufikia malengo ambayo mmejiwekea.
Ninaona moto wenu mkiwa uwanjani mnacheza kwa kujituma licha ya kuwa na makosa madogomadogo ambayo yanajitokeza hayo benchi la ufundi linapaswa liyafanyie kazi.
Siwezi nikayazungumza yote ila ninaona kwamba benchi la ufundi lina watu makini ambao wamekuwa na timu kwa muda mrefu na wanatambua kwamba wachezaji wao wanakosea wapi na ni mbinu ipi itawarudisha kwenye ubora wao.
Kikubwa ambacho ninawaasa wachezaji wanapaswa wafuate yale maagizo kwa kuwa kushindwa kufuata maagaizo inakuwa ngumu kupata matokeo.
Kwa sasa tunaona Bakari Shime amekuwa akikijenga kikosi kiwe cha ushindani na kinaonyesha ushindani mkubwa na hili linahitaji muda wa kufanyia kazi.
Hakuna ushindi unaopatikana nje ya uwanja bali ndani ya dakika 90 hizo hubeba furaha na maumivu kwa wachezaji pamoja na mashabiki.
Ile kauli ya kuna matokeo matatu huwa inazungumzwa kwa kuwa ni sera ya mpira hauwezi kuizuia ipo muda wote na itadumu kila siku kwa kuwa ni sera.
Ila kuna umuhimu wa kuona namna gani kila mchezaji akiwa anajitoa na kutimiza majukumu yake kwa wakati ndani ya uwanja bila kuhofia jambo lolote zaidi ya kuhitaji kuona matokeo ya kile anachokitaka kikitokea.
Mashabiki wamekuwa chachu kwa  mafanikio ya timu zetu hili lipo wazi na wanamchango mkubwa kila wawapo uwanjani kwani wanafanya wachezaji wacheze kwa kujituma bila kuogopa.
Kwa mfano Uganda wao walianza kuliona lango la timu ya Taifa ya wanawake pale Uwanja wa Taifa hiyo ilikuwa dakika ya sita lakini mwisho wa dakika tisini meza ilipinduliwa kibabe na ushindi ukapatikana.
Hakutakuwa na muda mzuri wa kukumbuka matokeo mazuri mliyoyapata nyumbani iwapo mtaboronga kwenye mechi zinazofuata hili litaongeza maumivu kwa mashabiki ambao wanapenda kuona matokeo.
Nimekuwa mfuasi mkubwa wa sheria 17 uwanjani na ninapenda kuona kwamba wachezaji wote mkazifuata na kuzifuatilia kwa ukaribu kwenye kila mashindano.
Imani yangu ni kwamba kila kitu kinawezekana na mtakuwa mabalozi wazuri wa Taifa hata mkipata nafasi ya kutoka nje ya nchi mtaendelea kupambana kwa kufuata kanuni bila kuzivurunda huku mkipata matokeo chanya.
Kwa sasa ni wakati wa kuona kwamba wachezaji wa timu zote za Wanawake nao wanakuwa na morali kubwa ya kujitoa wakiwa uwanjani na kucheza kwa juhudi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic