WIKI hii naweza kusema
ilikuwa chungu kwa viongozi wa timu ndogo na zenye uchumi duni kwenye ligi zetu
hapa nchini.
Ndio ilikuwa chungu baada
ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi kutangaza mechi chache
zilizosalia za ligi zitachezwa bila ya mashabiki, inamaana watakosa pesa za
viingilio.
Hilo ni pigo kubwa kwa hizo
timu ambazo sehemu kubwa zinategemea mapato ya mlangoni kujiendesha kama vile
kulipia kambi na safari.
Kazi ipo, tena ni kazi
kubwa mno kwa viongozi wa timu hizo ambao hivi sasa najua vichwa vinawauma na
hawajui chakufanya maana maamuzi hayo ni machungu kwao.
Wengine waliopata pigo ni
wazee wa kupiga ambao ni wazuri wa kufanya manuva ili kupiga mzigo kwenye
tiketi na mambo mengine.
Maana kuna watu tunawajua
wao wanasafiri na timu kila mkoa hasa timu za Simba na Yanga na kila sehemu
unayoenda wao wako getini tu hadi unajiuliza hivi hawa ndio mafundi wa hizo
kazi?
Safari hii najua hakuna
shida na hakutakuwa na vurugu kwenye milango mikubwa ya kuingia uwanjani hasa
kwa sisi wanahabari ambao wenye mpira wao wanatufanya kama karatasi vile, yaani
wakishatuandikia hatuna thamani tena.
Hapa sasa najua watu
watanielewa kwa nini tunasema tuna mfumo mbaya wa uendeshaji wa klabu zetu
ambao mtaji wake mkubwa ni viingilio.
Maana timu zetu hazina
mfumo sahihi wa uendeshaji na utafutaji pesa nje ya uwanja zote zinategemea
pesa za viingilio na za wadhamini basi kitu ambacho ni kibaya sana.
Wenzetu wameshatoka huko,
wako mbali zaidi na zaidi ingawa sisi bado tumeshindwa kufanya hivyo kwa sababu
hatuna watu sahihi wanaojua kuifanya hiyo kazi.
Hata hivyo viingilio vyetu
bado ni vidogo mno tofauti na wenzetu hapa Bongo ni kama shabiki anaingia bure
kuangalia mpira.
Timu inayosafiri kutoka
Mtwara hadi Katavi tena kwa basi dogo na ikifika leo kesho inacheza mechi na
baada ya mechi inaondoka unadhani itaweza kweli kuhimili vishindo vya kucheza
bila mashabiki? Hilo swali linakosa majibu.
Kwanza lazima tukiri
maamuzi ya Bodi ya Ligi na TFF ni maamuzi sahihi kabisa kutokana na hali yetu
ilivyo na wamethamini uhai wa mashabiki wa soka wa nchi hii kwa sababu ugonjwa
wa Corona ni hatari sana.
Mechi chache zimesalia
kabla ya msimu huu kumalizika na timu nyingi hivi sasa pesa zimekata maaana
wamezunguka sana na sasa nyingi zinategemea pesa za milangoni.
Hata hizo timu tunazoziita
timu kubwa lazima nazo zitayumba kiuchumi maana nazo hazina mifumo sahihi ya
kutafuta pesa nje ya uwanja na tena timu hizo ndizo zina mafundi wengi wa
kuzitafuna hizo pesa za viingilio.
Juzi kati Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Hassan Abbas aliliambia
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuwa kwenye mechi ya Yanga na Simba kuna
mianya mingi ya upotevu wa mapato na pesa nyingi zinaenda mifukoni mwa watu na
sio kwa wamiliki wa uwanja au klabu husika na hapo sasa utapata jibu jinsi watu
watakavyoumia.
Lakini hatuna jinsi
kutokana na hali ilivyo lazima timu zikubali tu na zijipange kwa msimu ujao
kama hali ikirejea kuwa shwari.
0 COMMENTS:
Post a Comment