MSHAMBULIAJI nyota wa Yanga, Bernard Morrison amekiri mwenyewe kwa mara ya kwanza kwamba kulikuwa na mazungumzo kwa ajili ya kujiunga na Simba.
Morrison ameliambia Gazeti la Championi Jumatano kuwa Simba walimfuata tayari akiwa na mkataba na Yanga wakitaka ajiunge nao na mazungumzo kwa asilimia kubwa yalifanywa na wakala wake.
Raia huyo wa Ghana ambaye tangu ametua nchini ameifungia Yanga mabao matatu, amesema Simba walitumia nafasi ya kumshawishi kujiunga nao baada ya kugundua ana mkataba wa miezi sita tu na klabu hiyo inayotumia rangi za njano na kijani.
Hii ilikuwa ni baada ya kucheza mechi chache na Yanga, Simba nao wakaonekana kuvutiwa na kiungo mshambulizi huyo wa zamani wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini na AS Vita ya DR Congo, moja ya klabu kongwe na kubwa barani Afrika.
“Ni kawaida kwa klabu yoyote kutaka kumsajili mchezaji wanayemuona ni mzuri uwanjani, hivyo niliona kawaida wao kuja kwangu,” anasema Morrison katika mahojiano na Championi jijini Dar es Salaam.
“Simba waliitumia nafasi ya mimi kuwa nina mkataba wa miezi sita na Yanga, wanajua kisheria hii inaruhusiwa. Na walianza mapema kidogo kunifuata tofauti na wengi walivyodhani,” anaongeza.
Morrison anasema Simba walianza kumfuata mapema hata kabla ya mechi ya watani, wakitaka baada ya miezi sita ya Yanga, mara moja aanze kazi Msimbazi.
“Simba walianza kunifuatilia hata kabla ya mchezo wetu dhidi yao (Kariakoo Dabi) wakijaribu kunishawishi kujiunga nao.
“Mwisho suala hili niliamua kuliacha kwa wakala wangu kwa kuwa ndiyo kazi yake naye akaendelea kufanya mawasiliano na Simba lakini mwisho kama unavyoona, nimeamua kubaki Yanga na kuendelea na kazi.”
Kwenye mchezo uliochezwa Machi 8 Simba ilikubali kichapo cha bao 1-0 ambalo lilifungwa na Morrison mwenyewe.
Tayari Morrison amesaini mkataba wa miaka miwili na Yanga na kwanza amekuwa akitumia muda wake mwingi kufanya mazoezi binafsi nyumbani pamoja na ndugu zake ikiwa ni kutokana na vita dhidi ya Ugonjwa wa Corona ambao unaishambulia dunia.
0 COMMENTS:
Post a Comment