March 20, 2020




NA SALEH ALLY
SERIKALI imefikia uamuzi wa kusimamisha michezo kwa kipindi cha siku 30 kutokana na ugonjwa wa Corona.


Ugonjwa huu umeitikisa dunia, karibu kila sehemu mambo yamekuwa magumu na unaona sehemu mbalimbali zimeyumba na hasa kibiashara lakini kijamii kwa maana ya maisha ya kawaida.


Tanzania ni kati ya nchi ambazo tayari zimekuwa na wagonjwa wa Corona, hili si jambo dogo na vizuri kujifunza kwamba hatuko kisiwani.



Wakati hakujawa na mgonjwa hata mmoja, ilikuwa inaonekana kama haiwezekani kufika hapa Tanzania. Leo kila mmoja anaona, Tanzania ni kati ya nchi zinazotajwa kuwa na wagonjwa wa Corona.

Kikubwa ambacho tunaweza kumshukuru Mungu ni kwamba tuna wagonjwa wachache na hii inatulazimu kuwa makini maradufu kuhakikisha ugonjwa huu hauenei zaidi.



Nimekuwa ninawaza tofauti kwamba baada ya muda fulani, ugonjwa huu utatulia na ufumbuzi utapatikana. Ninaamini pia haya ni matukio ya kila mwanadamu.

Jambo la msingi ni kuwa makini na kufuata masharti ya wataalamu hadi hapo itakapofikia suala hili limepata mwafaka na mambo yamekaa sawa.


Wakati tukiendelea kusubiri hayo, nina ushauri wangu kwa wanamichezo na watu wengine na zaidi ninataka kuzungumzia kutoufanya ugonjwa huu kuwa sehemu ya utani badala ya uhalisia.


Utani wa watu wengi mitandaoni wakiwemo wanamichezo, waigizaji, wasanii na kadhalika imenifanya nione kuna kila haja ya kukumbushana kuwa ugonjwa huu si utani.


Huenda kuna mtu anaweza kufanya utani kidogo kwa nia ya kufikisha ujumbe sahihi, si vibaya lakini si kuendelea kufanya mzaha tu bila ya kuwa na msaada wowote kwa jamii.

Kuna ile maana ya kioo cha jamii, huu ndio wakati mwafaka wa watu mbalimbali ambao wamekuwa na mashabiki au watu wanaowakubali kutumia nguvu zao nyingi kuzungumzia kuhusiana na ugonjwa wa Corona kwa usahihi.


Vizuri wafanye hivyo kwa kuwa hili si tatizo la Serikali pekee, hili ni tatizo letu na tunapaswa kupambana nalo kuhakikisha msaada unapatikana kwa kuwafikishia watu wengi zaidi ujumbe huku wakisisitizwa kipi hasa cha kufanya.


Tumeona kuna matumizi mabaya ya namna ya kujilinda. Watu wanapaswa kufikishiwa ujumbe na Serikali pekee haiwezi kufikisha kila sehemu. Wako nyota wengi wa soka na michezo mingine, waigizaji na wanamuziki ambao wana watu wengi mitandaoni, basi wafanye hivyo.


 Rais John Pombe Magufuli alisema kuhusiana na vyombo vya habari na waandishi kushiriki katika utoaji elimu, hili ni sahihi. Lakini wanamuziki, waigizaji, wanamichezo na wengineo nao wanapaswa kushiriki kinagaubaga.


Ungekuwa pia ni wakati mzuri sana hata kwa wanasiasa nao wakiwemo wa upinzani, pia chama tawala washiriki na kushirikiana. Si tuwe tunawaona wakati wakilalamika au kupingana pekee. Wakati wa matatizo kama sasa wanakaa kimya tu, haitakuwa sahihi.


Ninaamini katika hili hakuna upinzani wala kupigana badala yake tunaungana kwa ajili ya taifa letu na kuhakikisha tunalipigania kwa pamoja.


Tatizo hili halina mwenyewe, na si sahihi kulipuuza kama kuliona ni dogo au la kupita tu, huenda litakuwa dogo kama tutaungana kuhakikisha tunapambana nalo bila ya kulibeza.


Kwa wale wanaofanya mzaha, vizuri wakumbuke hili ni janga na kulipambania tukisaidiana na Serikali yetu ndio sahihi zaidi. Hivyo tuongeze nguvu ya kukumbushana, kutahadharishana na kuelezana mara kwa mara kuhusiana na ugonjwa huu ambao utapita tukiwa salama kama kweli tutaonyesha ushirikiana na kama haitakuwa hivyo, basi mwishoni athari zitakuwa kubwa zaidi na hasara itakuwa juu.





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic