KILA mmoja kwa sasa anapambana kujiokoa kutoka kwenye hali isiyopendwa na wengi ambayo ni maradhi yaliyoingia kwa kasi kutokana na maambukizi yake kuongezeka kila iitwapo leo.
Hilo lipo wazi kwani sio jambo la mtu mmoja pekee bali dunia nzima kiujumla kwa sasa inapambana kuona namna gani inaweza kupata usalama na kuendelea na shughuli za maisha kama ilivyokuwa zamani.
Mzigo mzito upo kwa kila mmoja kufikiria hali ya maisha yake na namna anavyoweza kuwa salama kwa wakati huu wa mashaka ambao umezidi kuendelea kwa kila mmoja na dunia pia kiujumla.
Maradhi tupo nayo ni lazima tukubali kwamba Virusi vya Corona vipo na vinaenea kwa kasi lakini cha kujiuliza ni kwa namna gani tunachukua tahadhari ama tunaendelea kuishi leo kama tulivyoishi jana?
Siku zinakwenda kasi sana hilo lipo wazi basi na akili za kupambana kwenye vita hii ni muhimu pia kuibadili na kufanya mambo kwa kuzingatia afya zetu ambazo ni muhimu pia.
Hofu imetanda kila kona ambapo kwenye mioyo ya watu wengi wanahofia kushindwa kuendelea kupambana na Virusi vya Corona.
Pale nguvu inapoisha ni muhimu kutafuta mbinu mpya ambayo itaongeza nguvu ya kuendelea kupambana kutafuta matokeo mazuri.
Kikubwa tunachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kuona kwamba kila mmoja anajitahidi kuzungumza na mwenzake ili awe balozi mzuri.
Iwapo kila mmoja atakuwa balozi katika hili japo kwa muda mfupi itaokoa wengine ambao bado hawajatambua kuhusu uwepo wa Virusi hivi.
Kikubwa ni kila mmoja kuchukua tahadhari ajilinde yeye na wenzake jambo litakalofanya kila mtu aendelee na maisha yake kwa amani.
Bado hali haijawa shwari lakini ni muhimu kila mmoja kuchukua tahadhari ambayo itamfanya awe salama na kuendelea na maisha katika kazi za kila siku.
Kwa wachezaji ninaona kwamba wamepewa program za kufanya na wakiwa nyumbani hili sio la kupuuzia ni muhimu kuzingatia hasa kwa wachezaji ambao mpira ni kazi yao inayowapa ugali na kusongesha maisha kwenye harakati zao za kila siku kwenye sayari hii ya tatu ambayo ni dunia.
Kutokana na kusambaa kwa Virusi vya Corona imani yangu ni kwamba wengi watahofia kufanya mazoezi kutokana na kulinda afya zao ili wasijumuike na wengine.
Hilo ni sawa na nina amini wanasimamia kile ambacho wanakiamini lakini bado kuna namna ambayo wanaweza kufanya ili waendelee na mazoezi huku wakilinda uwezo wao.
Kitu pekee ambacho kinatakiwa kwa sasa ni wao wenyewe wachezaji kukubali hali halisi kwanza kisha kujipanga upya kwa ajili ya kubadili staili yao ya maisha.
Ikiwa hivyo mengi yatabadilika na kila mmoja ataishi kwenye ulimwengu ambao anaupenda licha ya kwamba kuna maambukizi ya Virusi vya Corona kwani maisha lazima yaendelee.
Wanatakiwa watambue kwamba kitakachowaokoa kwa sasa ni umakini wao pamoja na dua bila kukoma itawasiaidia kuwa kwenye ubora wao.
Wafanye mazoezi kwa tahadhari wakiwa nyumbani wao wenyewe kwa kuwa ni muhimu kuzingatia kwamba uwezo wao na kipaji chao ni muhimu kuvilinda.
Ikiwa watashindwa kufanya mazoezi itakuwa ngumu kurejea kwenye ubora wao na kuwafanya wawe kwenye uwezo wa kuendelea na maisha ya kwenye soka.
Ni muhimu kufuata utaratibu na kanuni ambazo zimewekwa na Serikali pamoja na Wizara ya afya wakati wa mazoezi itawasaidia kuwa bora.
Kila mmoja atambue kwamba wakati wa mapito sio muda wa kulala ni muda wa kuendelea kupambana kufanya kazi ili kulinda uwezo wa wachezaji.
Kila mwanafamilia ya soka anapenda kuona wachezaji wakiwa kwenye ubora na wanafanya kazi bila mashaka yoyote ndani ya uwanja pindi ligi itakaporejea.
Kila mmoja anapaswa kuwa makini na kujali afya yake pamoja na afya ya familia kiujumla kukaa nyumbani iwapo hauna shughuli ya kufanya ni bora kuliko kwenda mahali ambapo hauna shughuli ya kufanya.
0 COMMENTS:
Post a Comment