JANGA la Virusi vya Corona bado linaendelea kuitikisa dunia tena kwa sasa ni kwa spidi kubwa huku mambo ya mbeleni yakibaki kuwa gizani sababu haifahamiki hatma yake.
Ligi kuu Bara na michezo mingine kwa ujumla hapa nchini ilisimamishwa kwa mwezi mmoja tangu Machi 17 na lengo likiwa ni kuangalia hali itakwenda vipi. Aprili 14 taarifa ilitolewa kwamba bado katazo lipo palepale.
Bado haijafamika rasmi Ligi Kuu Bara inarejea lini tena uwanjani na hii si kwa Bongo pekee mpaka Ulaya katika ligi pendwa hakuna ambayo inafahamika itarejea rasmi lini hii ni kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Kwa Tanzania mambo yanazidi kuwa magumu kwani ripoti ya maambukizi kwa sasa imekuwa ya hali ya juu mpaka sasa kuna wagonjwa zaidi ya 20.
Lakini pamoja na kutofahamu kuwa ligi itaendelea lini klabu zinaendelea kuweka mipango yake sawa hasa katika kuelekea msimu ujao wa ligi hususan masuala ya usajili.
Kila klabu kwa sasa licha ya ligi kusimama na kutojua hatma yake mipango yao ya usajili bado inabaki kuwa kipaumbele hapa Bongo na hata Ulaya sababu ndiyo kitendo muhimu zaidi kuelekea msimu ujao.
Pamoja na kwamba ni mpango muhimu kipindi kama hiki viongozi wanatakiwa kuwa makini na kufanya maamuzi sahihi na kuangalia ni kitu gani wanafanya kwa maslahi ya jamii.
Kuna wachezaji ambao wanatarajiwa kumaliza mikataba yao pale msimu unapomalizika ambao awali ulitarajiwa kumalizika Mei mwaka huu, lakini sasa bado haijafahamika itakuwa ni lini.
Viongozi na wachezaji wanatakiwa kuangalia na kujitafakati kipindi hiki wanapotoa maamuzi juu ya hatma zao pamoja na wachezaji katika klabu.
Hakuna asiyefahamu sheria kuwa unatakiwa kuzungumza na mchezaji lini na mkataba wake ukiwa umefikia hatua gani ili kuepusha migongano ya hapa na pale.
Mchezaji anaruhusiwa kuzungumza na klabu nyingine akiwa amesalia na miezi sita katika mkataba wake, lakini si sahihi kuzungumza na mchezaji akiwa bado na mkataba mrefu hapa sheria zinakuwa hazijafuatwa.
Kipindi hiki cha janga la Corona kisitumike vibaya kwani mwisho wa siku kinaweza kuja kuwagharimu baadhi ya viongozi na wachezaji wenyewe kuja kumbulia adhabu ambazo hawakuzitarajia kutokana na kukiuka sheria.
Hivyo ni vyema sheria na taratibu zikafuatwa na sio kuvunja sababu taifa sasa liko bize kupambana na maambukizi ya Virusi vya Corona na bora hilo likazingatiwa kwa umakini.
0 COMMENTS:
Post a Comment