May 29, 2020



JUNI Mosi mambo yanatarajiwa kurejea kwenye ulimwengu wa soka baada ya kimya cha muda mrefu ambacho kilikuwa kina maswali mengi kwa familia ya michezo.
 Mambo mengi yalikuwa yamesimama duniani kote na kwenye upande wa soka kwa Bongo shughuli zote zilikuwa zimesimama kwenye kila pande.
Hayo yote  yalisababishwa  na Virusi vya Corona ambavyo vinaivurugavuruga dunia kwa sasa kutokana na kuenea kwa kasi jambo ambalo linayeyusha raha kwa wataalamu na wanafamilia ya michezo.
Kwa sasa tayari tunaona Serikali imeruhusu masuala ya michezo kurejea baada ya kujiridhisha kwamba maambukizi yameanza kupunguua ingawa bado Corona ipo hilo lipo wazi.
Kwa maana hiyo bado tunapaswa kuendelea kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima kwani hali sio shwari kwa kila mmoja kuwa huru sana kwa wakati huu na mapambano inabidhi yaendelee bila kukoma.
Awali tulikuwa kwenye hali ya upweke bila kushuhudia mpira ndani ya uwanja na kuona zile burudani ambazo tulikuwa tumezikosa kwa muda mrefu ila kwa sasa zipo njiani kurejea ni muhimu kujipanga.
Ni wazi kwamba kila mmoja kuna kitu ambacho anakikumbuka kwenye ulimwengu wa soka ambao ulikuwa una matukio mengi yaliyokuwa yanaendelea.
Wengine nje ya nchi tayari wameanza kucheza na ligi zao zinaendelea kwa tahadhari kubwa hivyo bado nasi pia tukiwa kwenye mchakato kuna vitu vya kujifunza pia.
Kazi iliyopo kwa sasa ni kuendelea kuchukua tahadhari katika kujilinda kama ambavyo wenzetu wanafanya kwani janga la Corona sio la kuliletea utani ni vita endelevu.
Mipango makini inabidi ipangwe na kila mmoja kwa sasa kuanzia mchezaji mmojammoja kwani ishawekwa wazi kwamba Juni Mosi mambo yanarejea uwanjani.
Kauli ya Serikali ya hivi karibuni kwamba kutakuwa na vituo viwili ambavyo ni pale Mwanza na Dar es Salaam inabidi ipokelewe kwa mikono miwili na kutazama namna ya kumaliza msimu kwa sasa.
Inabidi wapenda michezo watambue kuwa rasmali watu ipo chini ya Serikali ambayo ina jukumu ya kulinda kila mmoja aliyepo ndani ya ardhi ya Tanzania kuwa salama hivyo hatua ambazo wanazichukua ni kwa usalama wa watu wake.
Wakati huu uliopo kwa sasa ni muda wa kuanza kufanya maandalizi ili ligi ikirerejea kila mmoja awe tayari kufanya kazi yake ambayo alikuwa hajaifanya kwa muda mrefu.
Kuanzia Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili, hawa kituo chao kitakuwa Mwanza hivyo watu wa Mwanza kazi ni kwenu sasa kuangalia namna gani mtaweza kujipanga kuwapokea wageni ambao wanakuja.
 Ligi ya Wanawake pamoja na ligi nyingine bado hazijaruhusiwa kwa mujibu wa Serikali bado kuna mambo ya kutazama ili mambo yaende sawa kotekote subira inahitajika.
 Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho hawa kituo chao kitakuwa Dar hivyo kuna jukumu lingine la maandalizi kwa timu zilizo nje ya Dar kuanza kujipanga.
Mamlaka inayosimamia michezo Tanzania, Shirikisho la Soka (TFF) ni wakati mwingine wa kutazama namna bora katika kusimamia msimu huu wa 2019/20 namna utakavyokamilika.
Bado tusijisahau kwamba janga la Corona lipo na tahadhari zinatakiwa ziendelee kuchukuliwa kwani afya ni utajiri namba moja.
Mashabiki wasikasirike kwa kuwa wameambiwa kwamba hakutakuwa na ingizo kubwa la mashabiki haya ni maelekezo kitaalamu ambayo yamefanywa na watu wenye utaalamu tusipuuzie.
Pia ningependa kuzikumbusha timu kwamba uwezekano uliopo kuhusu ligi kurejea ni kuchezwa bila ya kuwepo kwa mashabiki ndani ya uwanja.
Ni maumivu makubwa ambayo wachezaji watapitia kwani hawajazoea hali hiyo ila ni lazima kukubali hali iliyopo kwa kuwa mazingira yanatulazimisha kufanya yale yaliyopo.
Kinga ni bora kuliko tiba kwa wakati uliopo kwa sasa ni muhimu kuchukua tahadhari na kuzuia ile mijumuiko isiyo ya lazima ili kulinda afya zetu.
Katika hili  ni muhimu kufuata utaratibu unaotolewa na Serikali kwa kuzingatia bila kupuuzia maagizo ambayo yanatolewa na wataalamu wetu.
Masuala ya kuvaa barakoa, kunawa mikono ni muhimu kuzingatia kwa wakati huu kwani ni mambo ambayo yanayotuhusu sisi kwa pamoja tusiache kuchukua tahadhari ni muhimu kujilinda.
Kikubwa kitakachotuvusha salama  ni kufuata utaratibu uliowekwa ili tuwe pamoja kwenye  kujali afya zetu ambazo ni mtaji namba moja.
Ugonjwa huu upo  kweli hilo tusijisahau kwa kuendelea kuishi maisha yale ambayo tuliyazoea zamani ni muda wa kubadilika na kuongeza umakini zaidi.
Ni muhimu kufuata maelekezo ya Serikali na kufuata kanuni za afya ili kujilinda sisi wenyewe hii vita tumeanza ni lazima tuimalize kwa ushindi inawezekana.
Vita ni yetu hatupo sehemu mbaya kwa sasa tupo katika kuelekea kupata ushindi hivyo ni lazima tuendelee kuchukua tahadhari ili kuishinda kabisa Corona.
Wachezaji wakati wenu wa kurejea uwanjani tayari umeshafika na nina amini kwamba kila mmoja alikuwa anatimiza majukumu yake aliyokuwa amepewa na benchi la ufundi.
Kila mchezaji asijisahau kwa kufikiri kwamba atakuwa na nafasi ya kujitetea kwa sasa hapana ni muhimu kuonyesha kwamba alikuwa anafanya kile ambacho alielezwa.
Tunaamini kwamba kwa sasa kazi kubwa itakuwa ndani ya uwanja kupambana na kutafuta matokeo kwa ajili ya timu zao ndani ya uwanja bila kuchoka.
Dakika tisini kwa sasa ndio atakuwa mwamuzi wa kile ambacho mlielekezwa kufanya mkiwa kwenye mapumziko na inapaswa iwe katika umakini mkubwa kutimiza majukumu yenu.
Kwa timu zetu za hapa Bongo ni muhimu kuona namna  gani program ambazo zilikuwa zimetolewa na kutazama namna bora ya kuanza kupiga hesabu kwa ajili ya kumaliza mechi za lala salama.
Ilikuwa ngumu kumfuatilia mchezaji mmojammoja ila kwa kuwa mazoezi yameruhisiwa basi itakuwa muda wa kufanya kwa pamoja na kutazama wapi ambapo palikuwa panatatizo kiufundi.
Mchezaji mmojammoja kwa sasa ni wakati wa kufanya tathimini yeye mwenyewe akiwa nyumbani na kuona ni namna gani ametimiza majukumu yake aliyopewa ili akirejea mazoezini awe anatambua wapi ataanzia kuboresha uwezo wake.
Wale ambao walikuwa wakionesha juhudi wanastahili pongezi kwani walitimiza majukumu yao bila kusimamwa.
Muda hautakuwa rafiki wa kuanza kujipanga tena hapana kwa wakati ambao umebaki ni kuona kwamba kila timu inamaliza mechi zake na kuanza kujipanga kwa wakati ujao.
Muda upo kwa sasa kuanza kujipanga upya na kufuta yale makosa ambayo yalifanyika awali kwa kuzembea ama kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wa mchezaji mwenyewe.
Wachezaji ambao walikuwa na nidhamu nje ya uwanja binafsi nina amini matunda yao watayaona ndani ya uwanja kwa kuonyesha uwezo wao kwa vitendo.
Uvivu na uzembe ni hasara kwa timu na mchezaji mwenyewe kwani kunarudisha nyuma maendeleo ya timu jambo ambalo halitakiwi kufanyika.
Mapambano lazima yaendelee ili kukamilisha msimu huu na imani yangu ni kwamba tutaendelea kuchukua tahadhari ili kuwa salama na kuendelea kuwa salama.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic