May 9, 2020






Na Saleh Ally
MECHI tano tu zinatosha kuifanya Simba kuwa mabingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo.


Tayari kunaonekana kuwa na mpango wa kuirejesha Ligi Kuu Bara kwa ajili ya kumalizia mechi 10 zilizobaki kwa kila timu, kasoro Yanga pekee ambayo ina mechi 11 mkononi.


Simba ndiyo wenye nafasi kubwa ya kubeba ubingwa kutokana na pengo kubwa ambalo wamelitengeneza la pointi 17 dhidi ya Azam FC na pointi 20 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.


Kama ligi itarejea, Simba inatakiwa kushinda mechi tano tu za mwanzo na tayari itakuwa imejihakikishia kuwa mabingwa kwa msimu wa tatu mfululizo.


Hesabu zinaonyesha kama Simba watashinda idadi hiyo, watafikisha pointi 86 ambazo Yanga pekee ndiyo wanaweza kuzifikia kama watashinda mechi zote 11.


Kwa takwimu za mwanzo tokea msimu umeanza, Yanga haikuwahi kushinda angalau mechi nane mfululizo. Jambo ambalo linaonyesha kutakuwa na ugumu kufanya hivyo.


Ikitokea Yanga ikafanya hivyo, bado safu yake ya ushambulizi inaonekana haina na makali sana ya kufunga mabao mengi katika mechi moja kwa kuwa tofauti ya mabao ya kufunga kati ya Simba na Yanga ni 32.


Yanga imefunga mabao 31 katika mechi 27, Simba imefunga 63 katika mechi 28. Unaona tofauti ni zaidi ya nusu na kwa uhalisia inaonyesha kuwa Yanga haitaweza kufunga idadi ya mabao 30 katika mechi 11 zilizobaki na ukumbuke katika mechi zake 10 zilizobaki, Simba nao wataongeza idadi ya mabao ambayo bila shaka wastani si chini ya mabao 10.


Hivyo, Yanga hata kama itafanikiwa kufikisha idadi ya pointi 86, bado ni vigumu kufikia idadi ya mabao ya kufunga ya Simba na takwimu zinaonyesha Simba ina safu bora zaidi ya ulinzi kwa kuruhusu mabao 15 ya kufungwa huku Yanga ikiwa imeruhusu 20 sawa na Azam FC.


Maana yake hizo pointi 15 za mechi tano kama Simba watafanikiwa kushinda zote, hakuna ubishi watakuwa wamemchukua mwali.


Bila shaka kama ligi itarejea lazima kuna uwezekano wa mechi kuchezwa tatu kwa wiki moja. Maana hakutakuwa na mashabiki na inawezekana zikachezwa asubuhi na kwa siku zikachezwa mechi mbili kwenye uwanja mmoja.


Mechi tano kulingana na ratiba ilivyo, Simba inaonyesha inatakiwa kurejea kwani kuivaa Polisi Tanzania, moja ya mechi ngumu na itakuwa kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi.


Baada ya hapo, Simba wanatakiwa kwenda Tanga kuwavaa Wagosi wa Kaya, Coastal Union na baada ya hapo watarudi nyumbani Dar es Salaam kucheza mechi mbili dhidi ya Alliance na Mbao FC kabla kusafiri hadi Lindi kuwafuata Namungo FC.


Unaona mechi hizi tano kwa Simba ni ngumu hasa na Simba inatakiwa kuanza ligi kwa kasi ya “greda” ili kuhakikisha inashinda mechi hizo.


Lazima ianze na ushindi Moshi, halafu iendeleze hivyo kule Tanga na kwa mechi za Dar es Salaam, kawaida wanakuwa na kasi na kama watafanikiwa kushinda zote mbili, maana yake watakwenda Lindi kama vile wanakwenda kucheza fainali.


Wakishinda hizo tano, watakuwa wamejihakikishia ubingwa lakini watakuwa na mechi nyingine tano ambazo ni dhidi ya Ndanda (ugenini), Ruvu Shooting (Dar), Prisons (ugenini), Mbeya City (ugenini) na mwisho watamaliza dhidi ya Mwadui FC jijini Dar es Salaam.



MECHI ZA SIMBA ZILIZOBAKI LIGI KUU

Polisi Tanzania         Vs Simba  Ushirika 
Coastal Union           Vs Simba Mkwakwani
Simba Vs Alliance  Uhuru
Simba Vs Mbao Uhuru
Namungo        Vs Simba Majaliwa
Ndanda        Vs Simba Nangwanda
Simba Vs Ruvu Uhuru
Prisons Vs Simba   Sokoine 
Mbeya Vs Simba        Sokoine 

Simba Vs Mwadui Uhuru

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic