June 19, 2020

KAZI bado ipo kwa mashabiki kuendelea kufuata ule muongozo ambao umewekwa na Serikali kwa kuingia ndani ya Uwanja na barakoa pamoja na kushangilia kwa tahadhari.
Nimeona kidogo kwenye mechi hizi zilizopigwa wikiendi taratibu mfumo unanza kukaa kwenye vichwa vya mashabiki hilo linastahili pongezi ila umakini zaidi unahitajika kuongezeka.
Kwenye mechi mbili za mwanzo ambazo zilikuwa na mvuto mkubwa ikiwa ni ile liyopigwa Juni 13 ya Mwadui FC na Yanga nimeona kuna mambo ambayo yanaendelea japo sio mabaya.
Pia nimeutazama ule mchezo wa Simba na Ruvu Shooting pale Uwanja wa Taifa nimeona kwamba kuna vitu ambavyo mashabiki walivikosa sasa vimerudi nao pia wamerejea.
Kumekuwa na utaratibu wa mashabiki kuweka chini ya m domo barakoa hili si sawa kwa kuwa usalama ni muhimu ndani ya uwanja.
Ninajua kwamba mnatambua kuwa janga la Corona bado lipo ila ninakumbushia kuwa ni muhimu kuvaa barakoa na ikiwa utaiweka chini ya mdomo basi jitahidi uwe umbali wa mita moja na shabiki mwenzako.
Katika hili la mita moja pia wakati wa kushangilia nalo lipewe nafasi ili iwe rahisi maisha kuendelea kama zamani ila yote kwa yote nawapongeza kwa kujitokeza kwenu uwanjani.
Serikali imerudisha kile ambacho kilikuwa kimekosekana kwa muda mrefu kwa sasa naona mambo yanaanza kurejea kwenye mstari.
Narudi kwa wachezaji wa timu zetu za Bongo, nimeona lile tatizo ambalo awali nilikuwa ninazungumzia linawatesa kwa sasa wale ambao walikuwa wanaigiza mazoezi.
Mpira hauhitaji maigizo unahitaji umakini na utii katika kila jambo ndio maana ukaitwa mpira wenyewe unazunguka tu muda wote ndani ya uwanja.
Kwa wale ambao bado hawajaanza kucheza ni lazima wajipange sawasawa ili kuziokoa timu zao zifanikishe malengo ambayo wamejiwekea.
Kwenu waamuzi ninaona mmerudi na mabadiliko kidogo katika kumaliza zile changamoto ambazo mwanzo mlikuwa nazo hapohapo mliposhikilia endeleeni.
Naona kuna mabadiliko kidogo kwenye mechi zilizochezwa wikendi ambapo malalamiko yameyeyuka ghafla huku ikiwa ni kazi ya wachezaji wenyewe kutafuta matokeo.
Kwa sasa ndicho kinachotakiwa na sio leo tu hata kesho ni muhimu iwe hivyo kwa kuwa maisha ya soka yanategemea maamuzi bora kutoka kwa mwamuzi ambaye hajali kusemwa ilimradi anatimiza sheria 17.
Itakuwa vema ikiwa maandalizi yatakuwa makini kwenye mechi zote ambazo zimebaki kwa sasa ndani ya Ligi Kuu Bara kwenye safari ya kutafuta bingwa.
Mbali na bingwa ni safari ya kutafuta zile timu ambazo zitaaga ndani ya ligi na kuibukia Ligi Daraja la Kwanza na zile ambazo zitacheza playoff pia.
Mambo ni mazuri na mambo yanazidi kupendeza. Kwa sasa kila timu inasaka ushindi hilo ndilo ambalo linahitajika.
Mbinu ni moja tu kujiandaa vema na kutambua kile ambacho unakihitaji ndani ya uwanja na nje ya uwanja kutakupa matokeo mazuri ambayo ulikuwa unayatarajia.
Iwapo kila mmoja kwa sasa atapuuzia kufanya maandalizi inavyotakiwa kuanzia kwa wachezaji mpaka benchi la ufundi malipo yake yataonekana ndani ya dakika tisini hakuna cha kuongopa kwa sasa.
Kwa kuwa kila timu inatambua malengo iliyojiwekea ni muda sahihi wa kuona namna gani hayo malengo yatafikiwa kwa sasa ikiwa ni ngwe ya mwisho hakuna nyingine tena.
Kila timu macho yake ni kwenye pointi tatu ama moja bila kujali kwamba ni nyumbani ama ugenini kazi inapigwa mwanzo mwisho bila kuchagua.
Tazama namna Ruvu Shooting walicheza mpira mbele ya vinara wa ligi Simba, tazama namna Mwadui FC ilivyopambana mbele ya Yanga, nadhani kunapicha unaipata jinsi ligi ilivyo.
Kabla hujaenda mbali hebu jikumbushe ule mchezo wa Coastal Union na Namungo unadhani ni picha gani inakujia kichwani mwako kwa sasa?
Iwe nyumbani ama ugenini timu inapata matokeo kulingana na vile ambavyo imejipanga kikubwa mipango na mbinu sahihi.
Kwenu ambao mpo kwenye nafasi za kushuka daraja hakuna nafasi nyingine ya kujitetea zaidi ya hii kwa sasa ni wakati wenu mzuri wa kufanya uchaguzi.
Uchaguzi sahihi utawapa majibu sahihi ya kupata kile ambacho kipo kwenye vichwa vyenu na mwisho wa siku kitaonekana ndani ya uwanja.
Hakuna ambaye anapenda kuona timu yake inashuka daraja lakini kwa kuwa mpira ni ushindani lazima kila mmoja apambane kutafuta matokeo chanya.
Lengo ni moja kila mmoja apate kile anachostahili na kuvuna anachokitaka ndani ya uwanja bila ya kuwa na hofu yoyote kwamba atakuwa nyumbani ama ugenini.
Wakati mwingine sasa wa mashabiki kujipanga upya kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona kwani tunapaswa tuendelee kuchukua tahadhari kwa kuwa janga hili lipo.
Mashabiki tuendelee kujitokeza kwa kufuata  utaratibu huku tukikumbuka kwamba bado tupo vitani tusijisahau wala kupuuzia katika hili.

Tumeona Uwanja wa Jamhuri, Dodoma umezuiwa mashabiki kuingia kwa sasa kutokana na kukiuka muongozo wengine mna kazi ya kujifunza katika hili.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic