MGAWANYIKO uliopo kwa sasa kwenye ulimwengu wa Ligi Kuu Bara ni makundi manne ambayo yanapambana kufikia malengo ambayo wameyaweka kulingana na hesabu zao zilivyo.
Tunaona kwamba kwa sasa tayari ile burudani ambayo ilikuwa imekosekana kwa muda mrefu imerejea huku mwitikio ukiwa ni mkubwa kwa kila mmoja kuonyesha namna alivyokuwa akikosa yale anayoamini kwamba alistahili kuyapata kwa wakati.
Kikubwa ambacho kinatakiwa kwa sasa ni kuona namna gani kila mmoja atafikia malengo yake huku lengo likiwa moja tu kutimiza yale ambayo timu na uongozi kiujumla imeweka.
Ligi Kuu Bara, ambayo kwa sasa ipo kwenye lala salama imekuwa na burudani ya aina yake huku mashabiki wakifurahia kuona kile ambacho kinatokea ndani ya uwanja.
Matokeo ambayo yanapatikana ni dakika tisini zinaamua kipi kifanyike na nani anastahili ushindi hivyo kikubwa kwa kila anayeingia ndani ya uwanja kutambua anahitaji nini na anakwenda kufanya nini uwanjani.
Muhimu sana kuona kwamba kila timu inaona namna gani ushindi unapatikana na kila mmoja anapata anachostahili.
Kwa sasa wengi wanatazama nani atakuwa nani ila haya yote ni mahesabu baada ya dakika tisini kukamilika na mwendo unaanzia ndani ya uwanja na utaishia nje ya uwanja.
Kwa kuwa tupo kwenye lala salama muda huu kuna mgawanyiko wa kundi la kwanza ambalo hili linahaha kusaka ubingwa wa ligi ikiwa ni zile timu ambazo zipo ndani ya tano bora kwa sasa.
Katika hili hapa mshindi ni yule ambaye ataweza kuchanga karata zake vizuri naamini baada ya muda kidogo kupita itaanza kufahamika nani ni nani katika hili.
Ukiachana na nafasi ya ubingwa pia kuna kundi la pili ambao hawa wanasaka kuwa ndani ya 10 bora ili kuweza kuona namna gani wanaweza kufikia malengo ambayo wamejiwekea tangu awali.
Hapa pia bado mwamuzi ni dakika tisini kwani kila timu ina mchezo wake mkononi na iwapo itachanga vizuri karata jambo lolote linaweza kutokea katika mipango yao.
Hapa cha msingi ni wachezaji kuitambua kazi yao na kutimiza kwa wakati bila kupuuzia kwa kuwa muhimu kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja.
Wakati wa maandalizi ya mwisho huwa unakuwa na mambo mengi ila kitu kimoja kinachotafutwa ni ushindi.
Tukija kwenye kundi la tatu ni lile ambalo lipo kwenye kusaka nafasi ya kucheza play off. Labda unaweza kushangaa kwamba inakuaje timu isake kucheza playoff.
Hakuna kitu ambacho kinatokea kwa bahati mbaya kila kitu ni mipango, labda wamechanga karata wamegundua kwamba kupona kushuka daraja ni ngumu basi akili zao ni playoff wakiamini watatumia uzoefu.
Hapa pia kazi ipo kwani huwezi kujua ni nani mwingine anayefikiria kutokea huko ulipo wewe jambo la msingi ni kujipanga vizuri katika kila mechi.
Kundi la nne ambalo ndilo ninapenda nilizungumzie ni lile ambalo lipo nafasi ya kusaka nafasi ya kubaki kwenye ligi ili isishuke daraja hapa ndipo balaa lipo.
Timu nne zinashuka jumlajumla ina maana kwamba ushindani utakuwa mkubwa kwenye mechi hizi za lala salama hakuna ambaye anakubali kuwa daraja.
Kitu cha muhimu ambacho kinatakiwa hapa kwa mamlaka husika za michezo kwa kila mahali kuongeza umakini mkubwa ili kuepusha ujanjaujanja ambao unaweza kutumika.
Ili timu ishinde ni lazima ifuate njia zile za mafanikio kwa kuandaa kikosi vizuri bila kufikira kupata faida ya kuwa watakuwa nyumbani ama mbinu nyingine katika hili sio sawa.
Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) wakati sahihi wa kutazama hizi mechi za lala salama kwa timu ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja kwa namna ambavyo zitakuwa zikicheza.
Kuna mtindo wa timu kuamua kuacha ule ushindani na kutengeneza mazingira magumu kwa wenyeji wao kisa ni kwamba wanahitaji matokeo kwa namna yoyote.
Hili halihitajiki kwenye zama hizi za ukweli na uwazi ni lazima kuacha mpira uchezwa na yule aliyejiandaa apate ushindi wake.
Timu zote ambazo zipo kwenye hatari ya kushuka daraja zijipange upya na kuangalia ni namna gani zinamaliza mechi zao ambazo zimebaki kabla ya ligi kuisha.
Ikiwa zitaweka mipango sawa huenda zikapata matokeo ambayo yatawashangaza wengi na hicho ndio ambacho kinatarajiwa.
Mpira kwa sasa umekuwa ni jambo la wazi na kila timu inapata matokeo kulingana na vile ambavyo imejiandaa kikubwa ni hesabu na kujua unacheza na nani.
Iwapo kutakuwa na haki katika kila mchezo itakuwa rahisi kumpata yule atakayeshuka kwa uhalali bila makelele yoyote na hicho ndicho kinachotakiwa kwenye ulimwengu wa soka.
Itakuwa ni jambo zuri yule anayeshuka yeye mwenyewe ajue kwamba alizembea na sio kufelishwa makusudi kwani iwapo atafelishwa itakuwa ni dhuluma hatupendi iwe hivyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment