UGUMU wa mambo umeanza kuonekana kwa sasa kwenye Ligi Kuu Bara pamoja na Ligi Daraja la Kwanza kutokana na kuanza kuonekana kwa ugomvi na kelele nyingi.
Imekuwa rahisi kwa sasa kuskia kwamba wachezaji wanazomewa baada ya dakika 90 na mashabiki kwa kushindwa kuonyesha kile wanachokitarajia ndani ya Uwanja.
Ukweli ni kwamba hakuna ambaye anapenda kucheza chini ya kiwango ila wakati mwingine mazingira ambayo yupo yanamfanya ashindwe kutoa kile ambacho wengi wanakifikiria.
Sio busara kwa shabiki kumzomea mchezaji hata iwe amefanya makosa kiasi gani ndani ya uwanja jambo la msingi ni kumpa moyo na kumshauri ili aweze kuonyesha uwezo wake ila mchezaji hawezi kumzuia shabiki asizomee kwa kuwa ni kawaida kwenye mpira.
Namna ambavyo shabiki unaona ni tofauti na mwalimu kwani mpaka ameamua kumpa nafasi huwezi kujua ana kitu gani cha ziada ambacho anacho ndani ya uwanja.
Kila mchezaji ana utofauti wake na wachezaji wengine jambo ambalo linaamua nani aanze ni kulingana na plan ya mwalimu kwenye mchezo huo hivyo ikiwa amepewa nafasi huenda mwalimu amegundua kuwa ili apate ushindi huyo aliyemuanzisha anahitajika.
Kwa sasa mashabiki wengi wameamua kugeukia suala la uchambuzi wa mpira na kuanza kupanga namna ambavyo wanataka kikosi kiwe hili pia linaumiza kwa kuwa ikitokea tofauti kazi kubwa inakuwa kulalamika.
Hata siku ikitokea labda mchezaji unayempenda akaanza na timu ikapoteza ama ikashindwa kupata ushindi lazima lawama ziwepo hilo ni jambo la kawaida kwa mashabiki.
Kuhitaji kupata matokeo ya aina moja ambayo ni ushindi hapo sio sawa mashabiki ni lazima kukubali kwamba mpira una matokeo matatu kushinda, kufungwa na sare.
Kwa wakati ambao tupo kwenye kumalizia lala salama ya ligi ni lazima kila shabiki awe mtulivu aache nafasi kwa benchi la ufundi lisimamie yale ambayo wanaamini kwamba yana nguvu na yatawapa matokeo.
Hakuna mwalimu ambaye anapenda kuona kikosi chake kikipoteza mchezo ndani ya dakika 90 hili halipo kinachotokea ndani ya mchezo ni mbinu ya kila mmoja kutafuta ushindi wake.
Kwenu waamuzi mlianza vizuri kwenye mwendelezo wa mechi za Juni 13 ila ghafla mambo yameanza kurudi kulekule tulikotoka.
Sitapenda kulizungumia sana kwa kuwa kuna mamlaka ambazo zinashughulikia masuala hayo ila ninapenda kuwaomba kwamba itapendeza iwapo mtachezesha mechi zote kwa kufuata sheria 17.
Ni muhimu kila mmoja ambaye ana jukumu la kuchezesha mpira azingatie kanuni za soka bila kujali anachezesha timu gani hali ya malalamiko ya mashabiki, makocha na wachezaji inaanza kurudi tena.
Hili janga tulianza kulisahahu hasa kwenye mechi zile za mwendelezo na baada ya muda tukaamini kuwa itakuwa ni historia ila mwisho wa siku mambo yameanza kurudi kulekule ambako tulikuwa.
Itapendeza iwapo waamuzi mtafanya tathimini ya kutosha na kufanya maamuzi kwa usawa kwani wakati uliopo ni mdogo kwa timu kuanza kufikira masuala ya maamuzi ilihali wamebakiwa na mechi chache tena ngumu.
Jambo la msingi ni kuona kwamba sheria hazipindishwi ila usawa na haki inapaswa uonekane katika kila hatua kwa sasa kwenye mechi ambazo zitachezwa.
Timu zinapiga hesabu kubaki ndani ya Ligi Kuu Bara nyingine zikiwa zinafikiria kutwaa ubingwa sasa mambo yanavyobadilika kutokana na maamuzi ndani ya uwanja sio sawa.
Tunapenda kuona mpira safi na maamuzi pia yawe safi ukizingatia kwamba tulikuwa tumekosa burudani hizi kwa muda mrefu tangu Machi 17 sio kitu chepesi kuanza kurudia yale maumivu ambayo tuliachana nayo.
Ipo wazi kila timu kwa sasa ina mipango yake ambayo wamejiwekea sasa pale inapotibuka kisa mwamuzi ameshindwa kusimamia haki haileti pcha nzuri kwenye ulimwengu wa michezo.
Hakuna ambaye angependa kutupiwa zigo la lawama pale ambapo anapoteza hivyo muhimu ni kuona namna gani waamuzi mnakwepa lawama za kupewa zigo la kuifelisha timu sio sawa.
Kila timu inapambana kusaka matokeo uwanjani hivyo mipango ya kufelishana hiyo sio mizuri kwani inamaliza nguvu za wachezaji na viongozi kujipanga upya.
Pata picha namna Biashara United inavyopambana ama Singida United namna inavyopambana kusaka matokeo mwisho wa siku unasema kuwa wameotea hii ni mbaya.
Iwe nyumbani ama ugenini timu inapata matokeo kulingana na vile ambavyo imejipanga kikubwa mipango na mbinu sahihi.
Kwenu ambao mpo kwenye nafasi za kushuka daraja hakuna nafasi nyingine ya kujitetea zaidi ya hii kwa sasa ni wakati wenu mzuri wa kufanya uchaguzi wa kile mnachokitaka.
Muda pekee ambao umebaki ni kuona kwamba kila mwamuzi anatimiza wajibu wake kwa wakati bila kupendelea na kwa kufanya hivyo kutasaidia timu kupata matokeo.
Hakuna asiyejua kwamba mpira ni ushindani lazima kila mmoja apambane kutafuta matokeo lakini kuna muda mwingine mazingira yanakuwa magumu na timu inashindwa kuonyesha uwezo ndani ya uwanja.
Katika hilo pia wachezaji ni muhimu kuongeza juhudi ili kufikia malengo ya timu ambayo yamewekwa kwa kila mchezaji kucheza kwa kujituma.
Ukiachana na hayo basi ninapenda kuwakumbusha mashabiki kuwa ni muhimu kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona.
Bado janga la Corona lipo tusijisahau kuwa mambo yamekuwa tayari licha ya masuala ya michezo kuanza ndani ya ardhi ya Bongo.
0 COMMENTS:
Post a Comment