June 3, 2020


MTIBWA Sugar ni Klabu ya Soka Tanzania inayopatikana mkoani Morogoro ilianzishwa mwaka 1988 na kundi la wafanyakazi waliokuwa wanafanya kazi kwenye kiwanda hicho waliokuwa wakicheza pamoja.
Ilianza kucheza Ligi Kuu Bara1995 kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Thobias Kifaru  na bado inapambana ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo kwa sasa ipo nafasi ya 14 ikiwa imecheza mechi 29 na kibindoni ina pointi 33.
Msimu huu ilianza kwa kusuasua kutokana na kushindwa kufurukuta kwenye mechi zake za Ligi kwani katika mechi 29 ilizocheza ambazo ni dakika 2,610, imeshinda nane, sare tisa na kichapo mechi 12. Hatua zao zipo namna hii:-
Mafanikio
Kwa muda wa miaka 20, Klabu ya Mtibwa Sugar haijashuka daraja bado ipo ndani ya ligi ikizidi kuleta ushindani.
Mtibwa Sugar imekuwa ni chuo cha kuzalisha wachezaji ambao wamekuwa tegemeo kwenye timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara na wanafanya vizuri.
Simba kuna Hassan Dilunga ambaye ni kiungo kwa sasa ametupia mabao sita na pasi tatu za mabao huku kwa upande wa Yanga beki Juma Abdul naye anafanya vizuri kwani ni kinara wa kutengeneza pasi za mwisho akiwa nazo tano.
Hawa hapa wametusua bila presha
Nikson Kibabage ni kinda anayekipiga nchini Morroco ni zao la Mtibwa Sugar hajapitia timu kubwa ila ameibukia El Jadida amekutana na mzawa Simon Msuva.
Nassoro Mohamed naye pia ni zao la Mtibwa Sugar kwa sasa ametimkia nchini Serbia ambapo anakipiga huko na hawa wote wameingiza mkwanja mrefu pale Mtibwa Sugar.
Hakuna mchezaji waliyemsajili kwa dau kubwa
Mtibwa Sugar haina rekodi ya kusajili mchezaji kwa dau kubwa badala yake inawarudisha wale waliopotezewa muda kwenye timu zilizowachukua na kuendeleza kuwakuza, kwa sasa ipo na Abdulhaman Humud ambaye alirukaruka klabu kama Simba, KMC ila kwa sasa ametulia ndani ya Mtibwa Sugar na ametupia mabao mawili.
Uwekezaji
Mtibwa Sugar imewekeza kwa vijana wadogo wakiwa na timu za vijana ambao ni mabingwa mara mbili wa ubingwa wa kombe la vijana chini ya miaka 20, waliutwaa 2018/19 mkoani Dodoma mbele ya Stand United na msimu wa 2019/20 mbele ya Azam FC.
Jamal Baiser ni Mkurugenzi wa Mtibwa Sugar amekuwa mstari wa mbele kuwekeza kwa vijana na kutoa sapoti kubwa kwa timu hiyo.
Mataji
Kabatini ina mataji mawili ya Kombe la Ligi Kuu Bara ambapo ilitwaa mwaka 1999 na 2000 wakati huo ilikuwa chini ya Kocha Mkuu, Jonas Mkoko huku baadhi ya wachezaji wakiwa ni  Salum Mayanga kwa sasa ni Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting , Zuber Katwila kwa sasa ni Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar na Meck Maxime ambaye ni Kocha Mkuu wa Kagera Sugar na Vincent Barnaba yupo timu ya Mtibwa Sugar ya vijana.
Pia ina taji moja la Kombe la Shirikisho ililitwaa 2018 iliposhinda mabao 3-2 mbele ya Singida United, mataji mawili ya Kombe la Mapinduzi.
Miundombinu
Mtibwa Sugar ina uwanja wao na hosteli kwa ajili ya wachezaji zilizopo mkoani Morogoro. Uwanja wao unaitwa Manungu ambao upo umbali wa kilomita  mbili kutoka makazi ya watu kwa mujibu wa Kifaru kwa sasa umefungiwa kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa.
Uwanja wao wanaoutumia kwenye mechi za Ligi Kuu Bara kwa sasa ni Gairo kwa mechi  zisizo na mashabiki wengi ila zile za Simba na Yanga ni Uwanja wa Jamhuri.
Mikakati ijayo
Mtibwa Sugar ipo kwenye hesabu za kujenga uwanja mwingine mkubwa na wa kisasa ambao utakuwa na hadhi kwa kuchezea mechi za kimataifa ili kuzidi kutangaza zaidi bendera ya Tanzania kimataifa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic