HEKAHEKA za usajili wa wachezaji wapya kwa ajili ya msimu wa 2020/21 ndiyo habari ya mjini kwa sasa, tangu dirisha la usajili lifunguliwe Agosti Mosi na linatarajiwa kufungwa Agosti 31.
Tofauti na miaka ya nyuma, dirisha hili linaonekana kuwa
la moto likichagizwa na ufinyu wa muda ambao klabu zimepewa ili kukamilisha
taratibu za usajili, ikumbukwe kuwa saa 5:59 usiku wa Agosti 31, kwa saa za
Afrika Mashariki usajili utafungwa rasmi.
Siku zinavyozidi kwenda ndiyo usajili unazidi kuwa mtamu
huku ukisindikizwa na vijimisemo vya uchokozi na kutishia amani kama vile;
Tetemeko, kombora, bomu, kusimamisha nchi ili mradi tu kumfanya mtu aliyenunua
bando kufuatilia usajili ajihisi hajaibiwa.
Nazipongeza klabu zote ambazo tayari zimekamilisha na
kutangaza wachezaji wao wapya, lakini kwa namna ya pekee nazipa heko
klabu zetu tatu kubwa hapa nchini Simba, Yanga na Azam kwani inaonekana
sajili zao zimekubalika na wadau wa soka nchini.
Kama ilivyotabiriwa na kusubiriwa kwa hamu mpambano kati
ya Simba na Yanga kwenye soko la usajili umekuwa mkali kiasi cha kuwaacha
watu wakistaajabu, nani alidhani kama nyota wa zamani wa Yanga, Bernard
Morrison angesaini Simba? Vipi kuhusu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo
Mbatha ambaye naye ameibukia Jangwani?
Wakati tukiendelea kustaajabu ya Simba na Yanga, kuna
klabu moja imenishangaza kidogo, hapa nawazungumzia 'Wagosi wa Kaya' Coastal
Union chini ya kocha, Juma Mgunda.
Kwanini wananishangaza? Ni hivi Coastal mpaka sasa
imeondokewa na baadhi ya wachezaji muhimu wakiwemo, Bakari Mwamnyeto
(Yanga), Ibrahim Ame (Simba) na Ayoub Lyanga (Azam).
Kibiashara Coastal wamefanya vizuri kwa kufanikiwa kupiga
pesa ndefu, lakini wakati Simba na Yanga zikivunja benki ili kuimarisha vikosi
vyao Coastal wao wako bize na shughuli zao nyingine yaani kama vile hili
dirisha la usajili haliwahusu.
Wanaishi katika dunia yao ya tofauti, nimeona wako mtaani
wanatafuta vijana wa kuwarithi wakina Mwamnyeto, ni wazo zuri kwani hata huyo
Mwamnyeto alitokea hukohuko lakini wakumbuke katika soka la sasa hii ni sawa na
kamali.
Ni mpango huu ndiyo uliwashusha Singida United msimu huu
waliamini vijana wa mtaani na wale wa timu B wangekuwa msaada matokeo yake
ilibidi wavunje timu na kusajili rundo la wachezaji wapya kwenye dirisha dogo,
wakashindwa kuwalipa hatimaye timu ikashuka.
Nawakumbusha tu Coastal soka la sasa linahitaji mabavu
kwenye soko la usajili hivyo waache ubahiri na kusajili nyota watakaoweza kuwa
mbadala sahihi wa wale walioondoka kwani kwa kiwango kilichoonyeshwa na timu
hiyo msimu huu litakuwa jambo la hovyo kuiona Coastal ikikosa muelekeo msimu
ujao eti kwa kuwa haikufanya usajili makini.







0 COMMENTS:
Post a Comment