October 20, 2020

 


KOCHA mpya wa Yanga, Cedric Kaze, tayari ameshaanza kazi ndani ya kikosi cha timu hiyo huku akitoa ahadi kwa mashabiki wa Yanga watarajie soka la pasi nyingi kama lile linalochezwa na Barcelona, maarufu kama Tik Tak.

 

Kaze amechukua nafasi ya Mserbia, Zlatko Krmpotic ambaye alitimuliwa Yanga baada ya kuiongoza kwenye mechi tano za ligi akishinda nne na sare moja.


Licha ya kuwa na mwenendo mzuri wa ushindi, Krmpotic alitupiwa virago kutokana na kushindwa kuifanya Yanga icheze soka la kuvutia.

 

Sasa ametua Mrundi Kaze ambaye anasifika kwa soka la pasi nyingi, na mashabiki Yanga wana matumaini makubwa kwa kuwa uzoefu wake unachagizwa na ukweli kwamba aliwahi kufanya kazi katika akademi ya Barcelona.

 

Wakati Kaze akitoa kauli hiyo tayari Simba wanatawala ligi kuu kwa kucheza soka la kuvutia lenye pasi nyingi fupi na ndefu linalosababisha washushe mvua ya mabao kwa wapinzani wao, lililopelekea kupata umaarufu wa “pira biriani”.

 


Simba kwa sasa ndiyo inayotamba kwa soka tamu maarufu kama ‘pira biriani’ huku ikiwatumia nyota wake, Mzambia, Clatous Chota Chama, Luis Miquissoine, raia wa Msumbuji na Mzambia Larry Bwalya katika eneo la kiungo kujazia minyama ya biriani katika mechi zao kwa kupata ushindi mkubwa chini ya kocha Mbelgiji, Sven Vandenbroeck.

 

Sasa Yanga wanaona jeuri ya Simba kwisha kwa kuwa Kaze anatua na mpira aina ya tik tak kama waliosifika nao Barcelona enzi zile za akina Iniesta, Xavi na Messi.

 

Kaze kwa sasa ana kazi kubwa ya kuhakikisha anaibadilisha Yanga na kucheza soka la Kibarcelona kutokana na kufanya kazi kwa muda mrefu kama kocha katika kituo cha kukuza vipaji cha Barcelona kilichopo Canada kabla ya kutua Yanga.

 

Sven, tayari ameiongoza Simba kushinda mechi nne katika mechi tano za ligi msimu huu huku wakifunga mabao mengi zaidi kwenye ligi hadi sasa (14), yaliyofungwa na wachezaji saba wa timu hiyo wakati Kaze ameichukua Yanga ikiwa imeshinda mechi nne, sawa na Simba na ikifunga mabao saba pekee yaliohusisha wachezaji sita wa kikosi hicho.

 

Timu zote zina pointi 13 kuelekea mchezo baina yao utakaopigwa Novemba 7, mwaka huu, Uwanja wa Mkapa, Dar. Kuelekea mchezo huo, wana Yanga tayari wanaamini Kaze na tik tak yake atalipoteza pira biriani la Simba.

 

Pira biriani la Simba limekuwa likisumbua katika eneo la kiungo kutokana na kutengeneza nafasi nyingi za mabao kutokea kwa viungo wake ambao ni Chama mwenye pasi za mwisho tatu wakati Luis akiwa nazo tano huku Bwalya na Mzamiru Yassin wakiwa na pasi mojamoja.

 

Kaze anayepambana kuingiza soka la tik tak ndani ya kikosi cha Yanga, ana jukumu la kuhakikisha viungo wa timu hiyo, wanapiga pasi za mwisho zenye macho ili kutengeneza mabao ya kutosha kutokana na hadi sasa kiungo Carlos Carlinhos kuwa ndiyo kinara wa pasi hizo akiwa ametoa mbili, akifuatiwa na Tuisila Kisinda, Deus Kaseke na Mukoko Tonombe ambao kila mmoja ametoa moja.

 

Kwa upande wa rekodi za makocha, wote wawili CV zao ni nzito. Kaze yeye amefanya kazi muda mrefu akiwa katika kituo cha Barcelona nchini Canada, pamoja na mwaka 2009 kuwa mchambuzi wa timu ya taifa ya vijana ya Ujerumani iliyotwaa ubingwa wa dunia ikiwa na akina Mesut Ozil, Toni Kroos, Sami Khedira, Manuel Neuer na Mats Hummels.

 

Rekodi hiyo ina mpa nguvu Kaze mwenye leseni A ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na Chama cha Soka Ujerumani (DFB).

 

Kwa upande wa Sven, yeye rekodi yake kubwa nje ya Simba ni kutwaa ubingwa wa Kombe la Afrika (Afcon) akiwa kocha msaidizi wa Cameroon mwaka 2016 na amejenga ufalme Msimbazi baada ya kuchukua ubingwa wa ligi kuu na Kombe la FA msimu uliopita pamoja na ngao ya jamii msimu huu.

 

5 COMMENTS:

  1. sasa rekodi ya kubwa ya kaze iko wapi ?
    hatujaona amefundisha timu kubwa inayoshiriki ligi kuu yyte, zaid ya academ hiyo ambayo ameondoka huenda kwa kiwango chake kibovu, sasa unataka kumfananisha sven ambae amebeba ndoo ya afcon akiwa msaidiz camerroon.
    kabeba ndoo mara 2 msimbaz na FA.
    mwandishi acha kuaibisha na kuchafua CV za watu.
    huyu kaze mfananishe na mbwana makaka au Minziro Felix.

    ReplyDelete
  2. Huyu mwandishi anazingua, anataka kulazimisha uzuri wakaze ambao Hana. Ulaya Ni tofauti na Afrika sembuse Maximo ligi ilimshinda akasepa bila kuaga.

    ReplyDelete
  3. Wewe mwandishi acha kuwatoa mapovu mikia

    ReplyDelete
    Replies
    1. Povu Nani ww kiazi, Nani bingwa wa nchi. Endelea kucheza na maandishi wanaume tunatwaa makombe.

      Delete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic