VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC kesho, Oktoba 20 wana kazi ya kupambana na Ihefu FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Sokoine saa 8:00 mchana.
Azam ipo nafasi ya kwanza baada ya kucheza mechi sita imeshinda zote na kujiwekea kibindoni pointi 18.Inakutana na Ihefu inayonolewa na Zubeir Katwila ikiwa nafasi ya 17 na pointi tatu.
Safu yake ya ushambuliaji inayoongozwa na Prince Dube imefunga mabao 12 huku safu ya ulinzi ikiwa imeruhusu mabao mawili ilikuwa mbele ya Kagera Sugar wakati wakishinda mabao 4-2.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabit amesema kuwa kikosi kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo na kwa sasa wameshawasili Mbeya kwa ajili ya maadalizi ya mwisho.
"Kikosi kipo Mbeya na wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mchezo wetu muhimu ambao utakuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote.
"Malengo yetu ni kuona tunapata pointi tatu muhimu kwani tuna jambo letu kwa msimu huu wa 2020/21, mashabiki waendelee kutupa sapoti," amesema.
Mchezo uliopita Azam FC ilishinda mabao 3-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Azam Complex inakutana na Ihefu ambayo imetoka kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Biashara United.
0 COMMENTS:
Post a Comment