NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta, amefunguka kuwa anaamini kikosi cha Stars kitapata matokeo mazuri kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Burundi kutokana na ubora wa wachezaji walioitwa na kocha, Etienne Ndayiragije.
Samatta ni miongoni mwa wachezaji sita wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania waliojumuishwa kwenye kikosi cha wachezaji 25, wanaotarajiwa kuivaa Burundi Oktoba 11, mwaka huu mchezo utakaopigwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutua nchini akitokea Instanbul, Uturuki, anapocheza soka la kulipwa kwenye kikosi cha Fenerbahce, Samatta alisema: “Nimewasili salama kutokea nchini Uturuki tayari kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Burundi.
“Nimeona majina ya wachezaji walioitwa na Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije kwangu nadhani wachezaji wote walioitwa wamestahili na naamini licha ya changamoto ya Virusi vya Corona iliyosababisha kusimama kwa ligi wachezaji wote wako tayari na tutapata matokeo mazuri kwenye mchezo huu.
”Wikiendi iliyopita Samatta alifanikiwa kutupia mabao mawili kwenye mchezo wake wa pili ndani ya Fenerbahce aliyojiunga nayo kwa mkopo akitokea Aston Villa ya England.
Leo Stars imeendelea kufanya mazoezi kwa ajili ya kujiadaa na mchezo huo ambao umeanza kuvuta hisia za mashabiki wengi.
0 COMMENTS:
Post a Comment