SUMU gani iliyoua dansi la Bongo? Hivyo ndivyo unaweza kujiuliza ukikumbuka miaka kadhaa iliyopita mashabiki wa burudani walivyokuwa hawaambiwi kitu na muziki wa dansi.
Katika miaka ya 2005 mpaka 2014 majina ya wanamuziki kama vile Ally Choki ‘Mzee wa Farasi, Banzastone (sasa ni marehemu) , Patchou Mwamba, Nyoshi El Saadat, Ndanda Kosovo na wengine kama hao, kama alikuwepo asiyewajua basi huyo aliitwa mshamba.
Hiyo yote ilisababishwa na mahaba makubwa ya mashabiki wa burudani kwenye muziki huo ambao kwa lugha ya kisasa unaweza kusema unapumulia mashine.
TWANGA ILIVYOTISHA
Kipindi hicho ulipoitaja bendi kama African Stars ‘Twanga Pepeta' kwa mtu hata shabiki wa kawaida kabisa wa burudani alikuwa akikutajia kikosi kizima kuanzia mpiga kinanda, Victor Mkambi, Mpigadram Abuu Semhando, Mpigatumba Mcd, waimbaji kama Ally Choki, Rogart Katapila, Chaz Baba, Saleh Kupaza, Msafiri Diouf, Saulo John ‘Fagason’.
Safu ya wanenguaji wa kike nayo ilipata ustaa mkubwa ikiwamo Lilian Internet, Fetty Kiboriloni, Mwantumu Athumani na Kiongozi wao Aisha Madinda viuno vyao vilikuwa vikitikisa jiji.
Upande wa wanenguaji wa kiume Mandela Surambaya, Wabillahi Zungu, Super Bokilo, Danger Boy na kiongozi wao Super Nyamwela walikuwa balaa.
Kikosi kilikuwa kimesheheni kila kona, unapokiona kwenye shoo ya jana haiwezi kuwa kama ya leo lazima waje na jipya. Enzi hizo ukiingia kwenye shoo ya kikosi kama hicho ilikuwa ni nyomi la watu kumsaka mtu mpaka mziki uishe.
MOTO WA AKUDO ULIVYOZIMIKA GHAFLA
Huo ulikuwa ni upande wa Wana wa Kutwanga na kupepeta. Bendi nyingine iliyotisha kipindi hicho kwa kujaza nyomi la mashabiki Akudo Impact ‘Vijana wa Masauti’ na staili yao ya Pekechapekecha iliyokuwa na ngome yake pale Msasani Beach Club.
Kipindi hicho kwa wajanja wa jiji la Dar na mikoa jirani kama hujawahi kufika kiwanja hicho kwenye bonanza lao la kupekechapekecha ilionekana sawa kukuita mshamba.
Bendi hiyo iliyokuwa chini ya Prezidaa wake, Christian Bella na msaidizi wake, Tarcis Masela huku kukiwa na waimbaji kama vile Zagreb Butamu, Papy Malay, Allain Kabasere na wengineo.
Walitamba na ngoma mbalimbali ikiwemo Yako wapi mapenzi ambacho walikuwa wakikifananisha na wimbo wa taifa kutokana na watu wengi kuyajua mashairi yake kiufasaha.
Mkali wa kupapasa kinanda, Andrew Sekedia kinanda chake kilitumika kuwachanganya akili mashabiki wa bendi hiyo na kujisikia vibaya kila walipolikosa bonaza hilo.
Kwa upande wao safu ya wanenguaji Akudo iliongozwa na wanenguaji mahiri kutoka nchi ya Congo DR akiwemo, Nancy Lohuma, Shushuu Maisha, Nadine Esalaa, Fanie Bosawa, Laisaa Sangwa na wengine ambao shughuli yao kila shabiki aliyefika kwenye shoo zao aligundua kilichowasafirisha wadada hao maili nyingi kutoka Congo DR mpaka Bongo.
Viuno vya wadada hao na jinsi walivyokuwa wakijipamba kikongomani na nywele za rasta zilizowaanguka mpaka kiunoni ziliwachagiza sana wanaume wa kibongo na kuwafanya wawe macho kodo jukwaani wakijifanya kuangalia shoo.
Hatujui mdudu gani aliuvamia muziki huu lakini mwisho wa siku leo hii hayapo tena yote hayo, imebaki stori.
HATA FM ACADEMIA WAZEE WA NGWASUMA NAO CHALI!!!
Kipindi hicho bendi zilikuwa nyingi lakini The Big Three au bendi tatu kubwa ilikuwa ni African Stars ‘Twanga Pepeta’, Akudo Impact ‘Vijana wa Masauti’ na FM Academia ‘Wazee Ngwasuma’.
Tukija FM Academia ambayo kirefu chake ni Familia Moja baada ya kuhitilafiana na kampuni iliyokuwa ikiwamiliki, sasa wanajiita CP Academia baada ya kupata kampuni mpya inayowasimamia.
Tukizungumzia enzi hizo Wazee hawa wa Ngwasuma wakiongozwa na Prezidaa wao, Nyosh El Saadat na Msaidizi wake, Patchou Mwamba, ngome yao ilikuwa New Msasani Club ambapo nao walikuwa wakipiga shoo kiwanja hicho kila Jumapili.
Ukiachana na kiwanja hicho walikuwa na kiwanja kingine walichokuwa wakijaza mafuriko ya mashabiki pale Kijiji cha Makumbusho Kijitonyama kila Jumamosi.
Safu ya Wazee wa Ngwasuma ukiachana na maprezidaa wao kilikuwa na waimbaji hatari kama vile, Muleziri Boyange ‘Mulemule’ Pablo Masai, Rodger Muzungu, Kalidjo Kitokololo, Jesus Katumbi, Jose Mara, Totoo Kalala na wengineo.
Walikuwa na wanenguaji wenye kasi kama vile Queen Suzy, Titinaa Mwinyi, Queen Aaliyah, Side Mtianga na wengineo ambao walikuwa wakipiga pamba ambazo huenda zilichangia kuwavuta mashabiki kwenye maonesho yao.
UTAMU ULIKUJA, UTAMU UKAKATA
Pamoja na utamu wote huo kila bendi ilijaza mafuriko ya mashabiki. Lakini sumu isiyojulikana imeua burudani hizo hali iliyopelekea bendi zote kuwa taabani na kuzifanya zitumbuize bure na bado zimekosa waangaliaji.
KUTOKA KIINGILIO CHA BUKU KUMI MPAKA BURE
Kutokana na ugumu wa biashara ya muziki nimewashuhudia Twanga waliokuwa wakiweka kiingilio mpaka buku kumi ikipiga bure pale Baa ya Brazil Tegeta na shoo kuwa na watazamaji kiduchu hali ilipelekea kuhama kiwanja hicho.
Si hapo tu nimeshakutana nayo Baa ya Kwetu Pazuri, Toroka Uje, BL zote za Tabata bendi hiyo ikitumbuiza kwa kiingilio kinywaji.
Akudo Impact kwasasa haipo tena baada ya waimbaji wake kusambaratika.
FM Academia ambayo kwa sasa ni CP Academia iliyokuwa ikiongoza kwa mapedeshee nao wamekuwa wakipiga kwa kiingilio cha kinywaji lakini mashabiki nao wanawapita na kwenda kunywa baa za jirani kama hawawaoni.
Mara yangu ya mwisho kwenda kwenye onesho la bendi ni kwenye Baa ya Monie iliyopo Kiwalani jijini Dar ambapo nilisikia uchungu sana baada ya kukumbuka enzi hizo na kujiuliza ni sumu gani iliyoua muziki wa dansi?
Makala imeandikwa na Richard Bukos (GPL)
Mbona umewasahau vigogo wa muziki wa bongo Msondo Ngoma Music Band pamoja na Sikinde Ngoma ya Ukae?
ReplyDelete