BAADA ya kupita kwa siku 1,023 kwa mara nyingine Yanga wanarudi katika Uwanja wa Azam Complex na mara ya mwisho kukipiga uwanjani hapo ilikuwa ni Januari 27, 2018.
Yanga wanarudi uwanjani hapo leo Jumatano kucheza na wenyeji wao Azam FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo itapigwa saa 1 usiku.
Mechi hii ni muhimu kwa kila upande kwa sababu mshindi wake ndiye ambaye ataenda kileleni mwa msimamo wa ligi.
Mara ya mwisho Yanga wanaenda uwanjani hapo waliwarudisha baadhi ya wachezaji ambao walikulia katika hosteli za timu hiyo akiwemo beki Gadiel Michael ambaye ndiye aliyepeleka kilio kwa waajiri wake hao wa zamani.
Sasa safari hii pia ndani ya kikosi cha Yanga kuna mastaa ambao kupitia mechi hii wanarudishwa nyumbani Azam Complex kwa ajili ya kupambana na waajiri wao wa zamani kama makala haya yanavyokupa listi yao.
Farid Mussa
Jina la Farid Malik Mussa lilikuwa kwenye ubao wa matangazo wa Azam FC kwa miaka mitatu mfululizo, kuanzia 2013 hadi 2016 kabla ya kutolewa baada ya winga huyo kutimkia nchini Hispania kwenye Klabu ya Tenerife.
Winga huyu baada ya kupita miaka minne mfululizo akiwa Hispania kwa mara ya kwanza atarudi ndani ya viunga vya Azam Complex akiwa na kikosi cha Yanga kwa ajili ya kupambana na waajiri wake wa zamani Azam FC akiwa na pasi mbili za mabao.
Metacha Mnata
Kipa huyu leo ni kumbukizi yake ya kuletwa duniani jina lake linaimbwa na mashabiki wa Yanga kama mmoja wa mashujaa wao baada ya kuiongoza timu hiyo kuwa na kiwango bora kwa msimu huu wakiwa na pointi 25 baada ya mechi 11 na hawajafungwa hata mechi moja.
Ameanza kikosi cha kwanza mechi 10 amefungwa mabao matatu na ana clean sheet saba.
Kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza ndani ya Azam FC ndiko kulikomfanya Metacha kufunguliwa mlango na kutolewa kwa mkopo kwenda Mbao FC kwa msimu wa 2018/19.
Nyota huyu naye anarudi kwenye makazi yake ya zamani kwa sababu kwa msimu wa 2017/18 jina lake lilikuwa likisoma akiitumikia Azam FC.
Waziri Junior
Baada ya kusumbua ndani ya ligi akiwa na uzi wa kikosi cha Toto Africans cha Mwanza, straika Waziri aliamua kujifunga kitanzi na Azam FC Juni 5, 2017 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.
Lakini ajabu ni kuwa baada ya ‘kusinya’ mkataba huo Waziri akapoteza nafasi ndani ya Azam FC na kuwafanya mabosi wake wampeleke Biashara United kwa ajili ya kuongeza kiwango.
Straika huyu kama ilivyo kwa Metacha na Farid naye anarudi nyumbani Azam Complex ambapo alipita na kukaa miezi kadhaa kabla ya kwenda Biashara kisha Mbao FC na kutua Yanga kwa msimu huu.Kibindoni ana bao moja alifunga Uwanja wa CCM Kirumba, KMC 1-2 Yanga.
Ditram Nchimbi
Ukienda kwenye mechi ya Yanga ukisikia jina la Duma wala usishtuke sana kwani hilo ni jina la staa Ditram Nchimbi.
Straika huyu naye kwenye mechi hii anarudi nyumbani Azam Complex baada ya kuondoka hapo kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Ditram alikuwepo kwenye usajili wa Azam FC kwa msimu wa 2018/19 kabla ya kupelekwa kwa mkopo Polisi Tanzania ambapo kasi ya ufungaji ikawafanya mabosi wa Yanga wampe mkataba.
Yanga ikiwa imefunga mabao 13 ametoa pasi moja ya bao kwa Michael Sarpong kwenye ushindi wa Biashara 0-1 Yanga, Uwanja wa Karume.
Waziri Junior hata bench hayupo
ReplyDelete