BAADA ya kupewa nafasi na Bodi ya
Ligi (TPLB) ya kujiandaa na michuano ya kimataifa timu za Simba na Namungo
zinapaswa kutumia muda huo vyema kwa ajili ya maandalizi yao kuelekea kwenye
michezo hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa
na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo ilieleza kuwa timu hizo ratiba
zao za Ligi zitasogezwa mbele ili timu hizo zipate maandalizi ya kutosha
kuelekea kwenye michezo yao ya kimataifa.
Hivyo kupitia taarifa hiyo ni vyema
muda huo ukatumika vizuri kwa timu hizi mbili ili kufanya maandalizi mazuri yatakayoweza
kuleta matokeo chanya kwenye mechi hizo za awali.
Simba ikiwa na kibarua cha
kumenyana na Plateau FC ya Nigeria kati ya Novemba 27-29 kwenye Uwanja wa New
Jos nchini Nigeria, katika michuano ya Klabu bingwa barani Afrika.
Mabingwa hawa watetezi wa Ligi Kuu
Bara wanakumbuka kwamba msimu uliopita waliboronga mwanzoni kutokana na
kujiamini kupita kiasi kwa kuwa walipata mafanikio msimu ule wa nyuma.
Wakati huu yote hayo wanapaswa
wayaweke kando na kuingia uwanjani kupambana kwa ajili ya taifa la Tanzania.
Katika michuano ya Shirikisho
barani Afrika, Namungo watawakabili Al Rabita FC ya Sudan Kusini, Novemba 28.
Namungo chini ya Kocha Mkuu Hemed
Morroco itaanza nyumbani kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar kazi ipo
kusaka ushindi.
Ikiwa ni michezo ya awali tuna imani
michezo mliyocheza kwenye ligi imewajenga kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.
Ila mnapaswa mkumbuke kwamba
michuano ya kimataifa ni tofauti na ligi ya Bongo hivyo ushindani ni mkubwa
kuliko vile mnavyfikiria.
Kwa upande wa benchi la ufundi kazi
ipo kwenye kuwaandaa wachezaji katika hali ya ushindani ili kuweza kutoa
brudani kwa mashabiki na kupata ushindi.
Wachezaji wana kazi ya kutumia
uzoefu pia kusaka ushindi kwa kuwa michuano ya kimataifa huwa inakuwa tofauti
na vile ambavyo wengi wanafikiria.
Nahodha John Bocco, kiraka Erasto
Nyoni, Clatous Chama ambaye ni kiungo bora kwa msimu uliopita wote kwa pamoja
wanapaswa kuonyesha uwezo wao wote katika kusaka ushindi.
Hakuna ambaye anaamini kwamba
mchezo utakuwa mwepesi hasa ukizingatia kwa Simba wao wanaanza ugenini kisha
kazi inakuja kumalizwa Uwanja wa Mkapa.
Kwenye mashindano haya hasa kwenye
mechi za awali ni idadi ya mabao inatazamwa hivyo ikiwa itaruhusu kufungwa
ugenini itakuwa na kazi ya kupindua matokeo nyumbani.
Kasi ya Namungo kidogo inatia
mashaka lakini haina maana kwamba hawana uwezo wa kupata matokeo hapana uwezo
wanao.
Kikubwa benchi la ufundi kwa sasa
lina kazi ya kuongeza umakini kwa safu ya ushambuliaji na ile ya ulinzi ili
kuweza kutoruhusu kufungwa mechi ya nyumbani na ile ya ushambuliaji kupambania
kombe kupata mabao.
Kuanza nyumbani kunapaswa kuwe ni
mtihani kwa wachezaji wote kupambana kufaulu kupata matokeo mazuri.
Ushindi wa mabao mengi utatoa fursa
ya kujiamini na kwenye mechi ya marudio pia itakuwa kazi nyepesi kuongeza idadi
ya mabao.
Yote haya lazima yafanyike kwa
umakini na usahihi kwenye mechi za awali.
Moja ya mambo muhimu kwenye
michuano ya kimataifa ni kuwa na wachezaji ambao wamekuwepo kwa muda mrefu
kwenye ligi na kushiriki michuano mbalimbali.
Timu hizo zinatarajiwa kuiwakilisha
Tanzania katika michuano hiyo huku tukitarajia kuona zikifanya vyema na
kuipeperusha bendera ya nchi kimataifa.
Watanzania wapo nyuma yenu kuwapa
sapoti ili kuhakikisha mnapata matokeo mazuri na kuondoa yale yaliyojitokeza
msimu uliopita kutojirudia tena.
Pia wachezaji kumbukeni hii ni
fursa kwenu katika kuhakikisha mnajitangaza kwenye nchi zingine.
Hakuna mchezaji ambaye hana ndoto
ya kucheza nje ya nchi hivyo mnapaswa kujituma kwa bidii.
Nidhamu, Bidii na kujituma ni
muhimu kwenu wachezaji ili kuweza kufikia malengo mliyojiwekea pamoja na yale
ya timu.
Aidha kwa upande wenu wachezaji
mnapaswa kufuata yale ambayo mnaelekezwa na makocha mkiwa mazoezini hata kwenye
mchezo.
Muda wa mapumziko mliopewa tuna
imani mtautendea haki katika kufanya maandalizi na mtaenda kufanya vizuri.
Makocha pia mnapaswa kuwafuatilia
wapinzani wenu katika michezo ya hivi karibuni ili kujua ni kwa namna gani
mnaweza kuwakabili.
Kuangalia vipande vya picha (video)
vitasaidia kwa kiwango kikubwa ili kujua ni timu ya aina gani mnaenda kukutana
nayo.
Mkifanya hivyo mtajua ni mbinu gani
mnaenda kuitumia pamoja na wachezaji wa aina gani watumike kwenye mchezo huo.
Endapo mtajua mbinu zao watakazo
tumia itawasaidia kwenu mchezo kuwa mwepesi kwani mtajua namna ya kuwakabili
vema.
Hatuhitaji kuona timu zikitolewa
katika hatua za awali kama ilivyokuwa msimu uliopita maandalizi ni muhimu sana
kwa upande wenu ili muweze kupata matokeo.
Kwa upande wenu Namungo ni mara ya
kwanza mnashiriki michuano hiyo lakini mnapaswa kujituma kwa bidii na kuonyesha
ni kwanini mliweza kufika katika hatua hiyo.
Ikiwa mechi za kwanza kila timu
itapata matokeo itakuwa ni sehemu ya kwanza ya kuyafikia mafanikio.
Kila kitu kinawezekana iwapo
mipango na maandalizi yatakuwa bora ndani na nje ya uwanja hakuna
kinachoshindikana, tunawaamini mnakazi ya kurejesha furaha kwa mashabiki wenu.
0 COMMENTS:
Post a Comment