November 1, 2020


 IMEFAHAMIKA kuwa, kiungo mshambuliaji wa Simba raia wa Msumbiji, Luis Miquissone, ndiye aliyetoa mapendekezo ya usajili wa kiungo mshambuliaji, Pachoio Lau Há King anayekipiga UD Songo ya nchini huko.

 

Imeelezwa kuwa, Simba imepanga kumsajili kiungo huyo wa kimataifa raia wa Msumbiji katika kukiboresha kikosi chao kinachojiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020/21.

 

Wakati Simba ikiwa katika mipango hiyo ya kumsajili nyota huyo, imepanga kuachana na kiungo wao mchezeshaji raia wa nchini Kenya, Francis Kahata ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, Simba inamtumia Luis kufanikisha usajili wa kiungo huyo wa pembeni atakayetua kuichezea timu hiyo kwenye usajili wa dirisha dogo msimu huu.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, Luis alimpendekeza jamaa huyo baada ya viongozi kumshirikisha kuhusu usajili wa kiungo wa kimataifa mwenye uwezo wa kutengeneza mabao akitokea pembeni.


Aliongeza kuwa, kwa sasa mazungumzo yanafanyika juu ya kumalizana na kiungo huyo na atatua rasmi pindi usajili wa dirisha dogo ukifunguliwa Novemba, mwaka huu.

 

“Usajili wa Pachoio unafanikishwa na Luis ambao wakati wowote utakamilika kutokana na kuwepo mazungumzo hivi sasa kati ya uongozi na mchezaji huyo.

 

“Uongozi umepanga kukiimarisha kikosi katika safu ya ushambuliaji kwa kumsajili kiungo mmoja wa kimataifa mwenye uwezo mkubwa baada ya kocha kutoa mapendekezo ya usajili katika dirisha dogo.

 

“Viongozi wanamtumia Luis kufanikisha usajili wake kwani aliwahi kucheza naye kwenye klabu ya UD Songo, hivyo anamfahamu vizuri na ndiye anayefanikisha usajili wake,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Simba, Arnold Kashembe kuzungumzia hilo, alisema: “Kama uongozi jukumu lote la usajili lipo kwa kocha ambaye ndiye anayependekeza usajili, hivyo hilo suala lipo kwa kocha.”

1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic