December 17, 2020


 

NGOMA ni nzito kwa sasa ndani ya uwanja kutokana na kila timu kujipanga ili kupata matokeo uwanjani jambo ambalo linamaanisha kwamba kuna kitu cha pekee msimu huu.

Hakuna mnyonge ambaye anakubali kupata matokeo mabovu ndani ya uwanja kwa sababu mipango ipo wazi. Naona kwamba kila iitwapo leo ligi inakuwa na mabadiliko.

Pongezi kwa viongozi wa timu zote ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara pamoja na zile ambazo zinashiriki Ligi Daraja la Kwana kwa kweli mnastahili pongezi.

Weka kando za Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza usisahau kwamba kuna Ligi ya Wanawake Tanzania nayo ushindani ni mwendo uleule mwanzo mwisho.

Hii ni faida kwa walimu wote Tanzania pamoja na wale wa timu za taifa kwani wigo wa wachezaji unakuwa mkubwa. Nafasi inakuwa kubwa kwa kila mwalimu kujua anachagua nini na kwa wakati upi ikiwa atakuwa anahitaji wachezaji.

Ninapenda namna ushindani ulivyo kwa msimu wa 2020/21 ninapenda uendelee mpaka mwisho wa ligi. Kisha ukiisha hivi na msimu ujao uwe zaidi ya hapa nina amini kwamba baada ya muda tutakuwa na kitu cha kujivunia.

Ikiwa utakuwa na ligi bora na imara kila mmoja atapenda kuja kucheza na kuwekeza pia. Kwenye Ligi Kuu Bara huku kiasi fulani wadhamini wapo japo gharama za uendeshaji ni kubwa.

Kwa hao waliopo na wale ambao wanaojitokeza wanastahili pongezi kwa sababu matunda yanaokena kwa wakati huu. Wale ambao wanafikiria kudhamini ligi wasiache kusita kuna faida kubwa.

Ligi Daraja la Kwanza huku mambo ni magumu.Timu zinapambana na hali zao wenyewe hawa nao wanahitaji sapoti tusiwaache wala kuwatupa mkono wanahitaji sapoti yetu.

Wadau na wale wanaopenda kushuhudia mpira mzuri wakati ni huu. Kuna ushindani mkubwa unaendelea huku ndani ya Ligi Daraja la Kwanza mfano wake hakuna.

Nina amini kwamba ikiwa mdhamini atawekeza huku atapata faida kubwa. Kwanza atakuwa karibu na sehemu ya kiwanda cha wachezaji na atakuwa karibu na familia ya mpira.

Pongezi nyingi kwa Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) kwa namna ambavyo wanapambana kuona kwamba kila kitu kinakwenda sawa ndani ya ligi zote.

Hii inapendeza na inafurahisha yale makosa ambayo yanatia doa yafanyiwe kazi. Kila kitu nina amini kwamba kinawezekana kufanyiwa kazi na iwe hivyo.

Pia ndani ya Ligi ya Wanawake Tanzania hapa kuna ushindani mkubwa. Kila timu inapigia hesabu ubingwa na kila mchezaji anaamini anacheza kwenye timu ya mabingwa.

Yote haya yanawezekana ikiwa uwekezaji utakuwa mkubwa kwa kila timu bila ubaguzi. Sasa kinachotakiwa ni jitihada kwa wachezaji kutimiza majukumu ndani ya uwanja.

Ikiwa wachezaji watakwama kutimiza majukumu yao basi anguko linakuja. Yule ambaye hafikirii kuhusu anguko ni lazima afikirie kuhusu kufikia mafanikio kwa kuongeza juhudi.

Kwa kufanya vizuri ndani ya Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Wanawake basi nina amini wawekezaji watajitokeza.

Mbali na wawekezaji pia kutakuwa na timu bora ya taifa kwa upande wa wanawake pamoja na ile ya wanaume kwa kuwa wachezaji wanafanya jitihda ndani ya uwanja.

Bado ni mapema kwa sasa kusema nani ni bingwa ndani ya ligi kuu bara ama nani atatwaa taji la ligi ya wanawake. Hii inatokana na ushindani ambao upo ndani ya uwanja.

Kwa wale ambao wanakwenda mwendo wa kususasua wanapaswa kubadili gia. Ikiwa tatizo ni wachezaji basi wafanye usajili makini.

Hakuna ambaye anapenda kushindwa ila muhimu ni mipango makini. Nafasi ya kushinda kwa kila mmoja ipo ila inahitaji hesabu nzuri.

Jambo pekee ambalo linatoa ushindi kwa wachezaji ndani ya uwanja ni kujituma. Kuna kufuata maelekezo ya mwalimu pamoja na maandalizi mazuri.

Wakati wa kufanya vizuri ni sasa kwa kuwa ligi bado haijachanganya. Kila timu ipo sehemu salama lakini namna mwendo unavyokwenda ndivyo mambo yanavyozidi kuwa magumu.

Shukrani pia kwa Azam TV kwa kuifanya Ligi Kuu Bara ionekane dunia nzima. Watu wanafuatilia na wanapenda kile mnachokifanya mnastahili pongezi.

Kila la kheri timu zote ambazo zinapeperusha bendera kimataifa ikiwa ni Namungo na Simba. Maandalizi yanahitajika na juhudi pia ziongezwe.


Maandalizi ni muhimu hivyo kwa kuwa malalamiko kwa waamuzi yamekuwa mengi na kila mmoja anakuwa na kile ambacho anakifikiria kwenye akili zake.


Ni muhimu kuwa makini na kuepuka yale makosa ambayo yamekuwa ni ya kujirudiarudia mara kwa mara yanapunguza ubora wa ligi ambayo imeanza kwenda vizuri. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic