PONGEZI kubwa kwa mashabiki wa soka la Tanzania kwa namna
ambavyo wanajitoa kwa hali na mali kwa ajili ya kuzipa sapoti timu zao zikiwa
uwanjani.
Kwa kufanya hivyo kunaongeza lile joto kwa kila timu kuingia
ndani ya uwanja ikisaka ushindi kwa nguvu. Uwepo wa mashabiki unaongeza hamasa
na kuwafanya wachezaji wajitume zaidi.
Kila shabiki anapenda kuona timu inafanya vizuri jambo
linalomfanya aweze kufika uwanjani. Wengine ni wale ambao wanakaa nyumbani
wakitazama kupitia luniga.
Azam TV wamekuwa mabalozi wazuri wa wachezaji wetu na mpira wetu
kwa kuonyesha kila kitu moja kwa moja kuhusu mpira wetu.
Kwa kufanya hivyo nao pia wanastahili pongezi kwa sababu
wanaifanya Tanzania inazidi kujulikana kwa upande wa soka ndani na nje ya
Tanzania.
Kwenye vita ya kutafuta ushindi hapo ndipo kazi inabidi iwe
kubwa kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kufanya vizuri katika kusaka
matokeo chanya uwanjani.
Kwa kupitia yale mapungufu ambayo benchi la ufundi limeyaona
kwenye mechi zao zilizizopita. Ikiwa walishindwa kuona makosa vizuri wanaweza
kukaa kwa kutazama marudio ya picha ya Azam TV.
Kila siku mambo yanazidi kubadilika na teknolojia inakwenda
kasi. Hivyo hata mbinu pia zinapaswa zibadilike kwa sababu kinachotafutwa ndani
ya uwanja ni matokeo.
Ninapenda pia kuzikumbusha zile timu za Ligi Daraja la Kwanza
kuendelea kupambania ndoto zao ili kufikia malengo ambayo yapo kwenye mipango
kazi yao.
Ukweli ni kwamba huku kuna kiwanda kizuri cha kutengeneza
wachezaji kwa ajili ya kesho ni muhimu kila mmoja akawekeza nguvu ndani ya
uwanja kwenye kusaka matokeo.
Maandalizi mazuri yanahitajika kwa timu inayosaka matokeo
mazuri. Mambo mengine ni ya ziada kwani hakuna kinachowezekana kwenye maisha ya
mpira ikiwa hakutakuwa na maandalizi mazuri.
Kila mchezaji akitambua wajibu wake ndani ya uwanja na
akiwa nje ya uwanja kwa kufanya mambo ambayo yanaleta matokeo mazuri kwake na
timu itakuwa na matokeo mazuri hapo baadaye.
Wachezaji wanapaswa waelewe kwamba mashabiki wanajitokeza kuwapa
sapoti ii kuona matokeo mazuri. Hakuna shabiki ambaye anapenda kuona timu yake
ikifungwa hivyo hilo ni deni kwa wachezaji.
Makosa ambayo yametokea kwenye mechi zilizopita ni lazima
yafanyiwe kazi. Kwa kupata matokeo mazuri kutaongeza mashabiki wengi ndani ya
uwanja.
Wapo mashabiki ambao wamekuwa wakipenda ugomvi ndani ya
uwanja. Kwa kufanya hivyo kumekuwa kukigharimu baadhi ya timu kulipa faini kwa
kosa la mashabiki.
Jambo hili mashabiki liwekeni kando kabisa kwa mechi zijazo na
hata zile ambazo zinachezwa leo na kesho pia. Ni mbaya mashabiki kujiingiza
kwenye ugomvi.
Utani kwa mashabiki sawa, kushangilia kwa kuzomea sawa ila
kutupa chupa kwa wachezaji ama benchi la ufundi hapana.
Kurusha chupa kwa ajili ya waamuzi baada ya dakika 90 kukamilika
hapana tena hapana isiwe hivyo. Kumpiga shabiki mwenzako kisa jezi aliyovaa
hapana katika hili.
Utamaduni wa mashabiki wa Tanzania ni ustaarabu na kushangilia
hii ni asili. Basi tuna kazi ya kudumisha asili kwa wakati huu ambao tupo ili
kudumisha furaha.
Hata benchi la ufundi pia huwa linakuwa kwenye presha pale
mashabiki wanaposhangilia na timu imefungwa ama ipo nyuma kwa mabao kadhaa.
Zile kelele za mashabiki zinawafanya wapate nguvu mpya ya
kupambana kwa kuwa hawapo peke yao. Wachezaji pia hata wakiwa wamechoka bado
wanapata nguvu ya kufanya vizuri kwa sababu ya mashabiki.
Maisha ya mchezaji yanajengwa na kuwa na nidhamu ndani na nje ya
uwanja. Ikitokea akakutana na chungu ya mashabiki basi asiwe mkali awe mpole na
mtulivu.
Ikiwa mchezaji atakuwa na nidhamu ndani ya uwanja ni rahisi
kwake kufikia mafanikio ambayo anayahitaji. Ila kama itatokea hajali masuala ya
nidhamu ni rahisi kushuhudia anguko.
Hivyo ni jukumu la kila mchezaji kutazama namna bora ambayo
itamfanya aweze kupata namba kule ambako anakwenda kuanza maisha mapya ndani ya
soka.
Kwa waamuzi pia ni muhimu kuzingatia sheria 17 za soka katika
kutoa maamuzi ili wasiumie wengine kwa yale maamuzi yenu.
0 COMMENTS:
Post a Comment