UONGOZI wa Klabu ya Azam FC umeweka wazi kuwa, Prince Dube atarejea rasmi uwanjani kuanzia Januari 17, mwaka huu.
Dube aliyesajiliwa na Azam kutokea kikosi cha Highlanders ya nchini Zimbabwe tayari ametimiza majuma sita akiwa nje ya uwanja baada ya kuvunjika mkono kwenye mchezo dhidi ya Yanga Novemba 25,2020.
Kabla ya kupata majeraha hayo Dube alikuwa amehusika kwenye mabao kumi ya Azam akifunga mabao sita na kuasisti mara nne na kufuatia taarifa hizo ni rasmi sasa Dube anatarajiwa kuikosa michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyoanza kutimua vumbi Januari 5.
Ofisa Habari wa Azam FC, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’ amesema: “Kikosi chetu kipo tayari kwa ajili ya michuano ya kombe la Mapinduzi, tumefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mashindano haya na ni matumaini yetu tutafanya vizuri.
“Kocha Lwandamina (George) amepanga kutumia michuano hii kwa ajili ya kuwapa uzoefu nyota wetu wa kikosi cha pili pamoja na baadhi ya nyota wa kikosi cha kwanza ambao hawakupata muda mwingi wa kucheza kutokana na sababu mbalimbali.
“Kuhusu Prince Dube kwake uwezekano wa kucheza mashindano haya ni mdogo kwani madaktari wake wamemruhusu kuanza mazoezi kuanzia Januari 17, ambapo ni wazi michuano ya Mapinduzi itakuwa imeisha hivyo anaweza kusafiri na kikosi kama sehemu ya kwenda kujifunza tu na siyo kucheza,” .
0 COMMENTS:
Post a Comment