KUELEKEA kwenye mchezo wa kilele cha mashindano ya Simba Super Cup, kesho Januari 31, Uwanja wa Mkapa Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba, Didier Gomes amesema kuwa atafanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha kwanza.
Gomes alianza kwa ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Al Hilal Uwanja wa Mkapa, Januari 27 na kesho ana kibarua cha kusaka ushindi mbele ya TP Mazembe.
TP Mazembe wanaingia uwanjani wakiwa na hasira ya kupoteza kwa kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal hivyo kesho utakuwa ni mchezo wa kisasi kwa TP Mazembe ambayo Mtanzania Thomas Ulimwengu anacheza.
Raia huyo wa Ufaransa ambaye amerithi mikoba ya Sven Vandenbroeck ambaye amebwaga manyanga Januari 7 na kwa sasa yupo zake ndani ya FAR Rabat ya Morocco amesema kuwa anataka kuwaona wachezaji wake wote wakiwa ndani ya uwanja.
"Kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya TP Mazembe ninahitaji kufanya mabadiliko kwenye kikosi cha kwanza ili kuweza kuwaona wachezaji wote wakiwa ndani ya uwanja.
"Kutakuwa na mabadiliko ya kikosi kwenye mchezo wa kesho, mashabiki wajitokeze kwa wingi kuona namna ambavyo wachezaji wakipambana ndani ya uwanja.
"Hautakuwa mchezo mwepesi ila nina amini tutafanya vizuri kwani maandalizi yapo sawa na tunahitaji kupata ushindi," .
Kwa upande wa nahodha msaidizi wa Klabu ya Simba, Mohamed Hussein, 'Tshabalala' amesema :"Kama wachezaji tumejiandaa vizuri sababu ni mchezo muhimu kwetu hivyo tunatarajia utakuwa mchezo mzuri na wenye ushindani mkubwa ndani ya uwanja," .
Kocha wa TP Mazembe Felix Mwamba amesema:“Jana tulipoteza lakini haimaanishi kwamba sisi ni wabaya. Kwenye mchezo wetu dhidi ya Simba tutabadili mfumo ili kuweza kupata matokeo chanya," .
0 COMMENTS:
Post a Comment