Michuano ya mwaka huu ambayo
imeshirikisha takribani timu 16 zilizowekwa katika makundi manne, imekuwa na
ushindani wa aina yake licha ya hapo awali kuahirishwa kutokana na janga la
virusi vya Corona ambalo limekuwa tishio kwa maeneo mbalimbali duniani.
Miongoni mwa timu zilizopata
nafasi ya kushiriki michuano hiyo kwa mwaka huu ni timu ya Taifa ya Tanzania,
Taifa Stars ambayo ilishiriki michuano hiyo kwa mara ya pili baada ya kufanya
hivyo mara ya kwanza mwaka 2009.
Kwa bahati mbaya kama ilivyokuwa
mwaka 2009, katika michuano ya mwaka huu pia Stars iliishia katika hatua ya
makundi wakiwa wamejikusanyia pointi 3 tu ndani ya kundi C lililokuwa na timu
za Zambia, Namibia na Guinea.
Yapo mengi ambayo naamini timu
yetu ya Taifa imejifunza kupitia michuano hii, hasa kwa sababu kiasi kikubwa
cha nyota wengi walioitwa kwenye kikosi na kocha Ettiene Ndayiragije walikuwa
ni wapya.
Lakini miongoni mwa mambo mengi
ambayo sisi kama Watanzania tumejifunza kupitia michuano hii ni juu ya ubora wa
viwango vya waamuzi waliopata nafasi ya kuchezesha michezo hiyo.
Wengi wetu mtakubaliana na mimi
kuwa waamuzi waliochezesha CHAN ya mwaka huu, walifanikiwa kuonyesha uwezo
mkubwa wa kutafsiri zile Sheria 17 za mchezo wa soka.
Waamuzi hawa sio Malaika hivyo
hata kama walifanya makosa basi ni mara chache sana tena ni yale ambayo
tunayataja kuwa makosa ya kibinadamu, lakini pia waamuzi hawa hawajatoka sayari
nyingine bali kuna wengine wametoka hapo kwa Wanaafrika Mashariki wenzetu Taifa
la Burundi.
Nadhani hapa ndipo tunapopata
swali la kuwauliza waamuzi wetu wa Kitanzania, ni nini ambacho wamejifunza
kutoka kwa wenzao, na nini wanadhani imekuwa sababu kubwa ya kupelekea
kukosekana kwa mwamuzi hata mmoja wa Tanzania ambaye amekwenda kuchezesha
michuano hii?
Lazima tukubali kuwa bado kuna
changamoto ya ubora kwa waamuzi wetu, na hili limekuwa likithibitishwa mara kwa
mara na malalamiko mengi ya wadau wa soka hapa nchini, na hata kupitia adhabu
zitolewazo na bodi inayosimamia uendeshwaji wa ligi kuu (TPLB).
Na baada ya kukiri tatizo hilo tujiulize tunawezaje kulipunguza kama sio kuliondoa kabisa, kama ni kuendesha kozi za mafunzo, kuboresha mazingira ya kazi, kuongeza vifungu vya adhabu kwa waamuzi watakaokiuka miiko ya kazi zao au hata kuangalia upya mchakato wa kutoa vibali vya kazi kwa waamuzi hao.
Naamini ili kuweza kufika huko
tunahitaji kufanya maamuzi tu, na wala haiwezi kuwa kitu kigumu. Kama mwamuzi,
Georges Gatogato wa Burundi ameweza kuchaguliwa na CAF kusimama katika michezo
ya CHAN, naamini hata waamuzi wetu, Ramadhani Kayoko na Hery Sasii wanaweza.
Uchambuzi wa Lunyamila kupitia gazeti la Championi Jumatatu.
0 COMMENTS:
Post a Comment