March 16, 2021


 

KOCHA Cedric Kaze ameiacha Yanga ikiwa kileleni mwa Ligi Kuu bara baada ya kukusanya pointi 50 kibindoni.

Wanaoikimbiza Yanga kwa kasi ya kimondo ni watani wao wa jadi Simba ambao wana pointi 46 lakini hawajacheza mechi tatu nyuma ya Yanga.

Maana yake, Simba wana nafasi kubwa ya kuivuka Yanga na kukaa kileleni mwa ligi hiyo baada ya mechi hizo.

 

Inategemea Simba watazicheza vipi mechi hizo za kiporo ambazo zinaweza kuwa faida au hasara pia. 

 

Kwa Yanga hata kama watakuwa wanajaribu kuficha au kutaka mambo yaonekane ni kawaida lakini ukweli ni kwamba wana presha kubwa kutokana na Simba kuonekana sasa watakwenda kileleni.

 Inaonekana Simba wana nafasi kubwa ya kukwea kilele cha Ligi Kuu Bara na hofu inaongezeka kwamba kama Simba watafanya vizuri katika mechi hizo tatu, itawezekana vipi kuwang’oa tena kileleni hapo.

 

Mwisho kinachoongeza hofu ni namna ambavyo Yanga wamekaa kileleni kwa muda mrefu, takribani mzunguko wote wa kwanza lakini leo wanaondoka tena dhidi ya Simba ambayo inaonekana iko vizuri zaidi.

Suala la itakuwaje limechukua nafasi kubwa sana kwa kuwa Simba ndio mabingwa mara tatu mfululizo wa Ligi Kuu Bara. Kwamba wakipaa na kushika usukani, kuwang’oa ni shughuli nzito.

 Tayari Yanga ili kuona kwamba wanarekebisha mwendo wao ili waweze kwenda vizuri, wamemtoa kocha wao Kaze, maana yake wanataka kwenda mwendo sahihi ambao wanaamini utakuwa na tija zaidi.

 Kwa uchunguzi wao wameamini Kaze ndiye alikuwa tatizo kwa kushindwa kwenda kwa mwendo wanaoutaka, hivyo wamefanya marekebisho ya muda ya benchi la ufundi wakimpa mzalendo, Juma Mwambusi ambaye Yanga si mgeni na alishawahi kufanya kazi na Kaze.

Wakati Mwambusi anaendelea na kazi, Yanga wanaendelea na mchakato wa kumpata kocha mpya ambaye ataungana na Mwambusi kuendeleza gurudumu la kuifanya Yanga iendelee kufanya vyema.

 

Huku Yanga ikiendelea na michakato yote hii, kinachotakiwa sasa ni mashabiki nao kuonyesha heshima na kuupa nafasi uongozi wao uendelee kuifanya kazi yao kwa nafasi ili waweze kufikia kila ambacho wanakiamini.

 

 Kama gumzo litaendelea kuwa Kaze katika kipindi hiki ni kuzidi kuongeza matatizo kwa kuwa hakuna tena nafasi ya kumrudisha kocha huyo katika kikosi chao.

 

Badala yake, kwa sasa ni kuangalia mbele na Yanga ina nafasi gani ya kufanya vizuri kwa ajili ya baadaye. Ikiwezekana kama ni suala la ushauri basi uongozi upewe ushauri ambao unaweza kuwa na nafasi ya kusaidia kwenda mbele.

 

Kuendelea kumjadili Kaze ni kuiondoa Yanga njiani kwa kuwa sasa si kitu namba moja kwao, kinaendelea kubaki kama sehemu ya hadithi au historia ya timu hiyo kwa kuwa kocha huyo Mrundi naye ana mchango wake.

 

Vizuri Yanga wakaendelea kumheshimu lakini lazima waamini kwamba hakuna kocha ambaye anaweza kuja Yanga na akaendelea kubaki milele katika klabu hiyo.

 

 Wamepita wengi tu ambao wamekuwa na mchango na Yanga na leo hawapo. Mafanikio ya Yanga, mfano yale ya kuwa waliochukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nyingi zaidi unajumuisha makocha wengi ambao hadi sasa hawapo. Labda Mwambusi ambaye aliwahi kuwa kocha msaidizi wa Hans van der Pluijm.


Maana yake waliokuwepo, pia waliondoka. Hivyo kuondoka kwa Kaze, inawezekana uongozi ulikuwa na haraka au vinginevyo lakini bado mashabiki wa wanachama wanalazimika kubaki na uongozi wao ili kuendeleza maisha na harakati za klabu yao.

 

 

 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic