“TUNAWAPIGA mapema.” Hiyo ni kauli ya Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes raia wa Ufaransa kuelekea mchezo wa leo Jumanne dhidi ya Al Merrikh ya Sudan, hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Simba watawakosa wachezaji wawili tegemeo wa kikosi cha kwanza, Taddeo Lwanga na Pascal Wawa kutokana na sababu ya kuwa na kadi mbili za njano.
Licha ya kuwakosa wachezaji hao, lakini Gomes, alisema: “Ukiangalia kuna mchezaji kama Peter Muduhwa ambaye ni mzuri na anacheza beki wa kati, lakini hakuwa anapata nafasi ya kucheza kutokana na uimara na uelewano walionao Wawa na Onyango (Joash).
“Katika eneo hilo kuna Kennedy (Juma) na Ame (Ibrahim) ambao walikuwa wakicheza katika baadhi ya mechi kwa maana hiyo kuna ambao anaweza kuingia katika eneo hilo la beki wa kati.“
Kwenye kiungo mkabaji tunaweza kubadili mfumo wa kucheza, lakini katika mechi iliyopita ya ligi alicheza (Mkude) Jonas ambaye alifanya vizuri.
“Kuna Nyoni (Erasto) ambaye anacheza katika eneo hilo la beki wakati au kiungo mkabaji na nafasi nyingine yupo fiti na katika kipindi hiki tutaangalia namna ya kufanya baada ya kukosekana kwao.
”REKODI ZINAWABANA AL MERRIKH
Ingawa wengi wanaona Simba wana kibarua kigumu mbele ya Al Merrikh ya Sudan leo Jumanne, lakini shughuli hiyo inaweza kuwa nyepesi kwao kutokana na rekodi za wapinzani wao kuwa mbovu wanapocheza ugenini.
Rekodi zinawabana Al Merrikh hasa wanapocheza ugenini ambapo wanaonekana kuwa ‘wachovu’ kutokana na kupoteza mechi katika misimu mitano tofauti waliyocheza katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Al Merrikh wakiwa ugenini, hawana makali sana ambapo wamepoteza mechi tano mfululizo za ligi hiyo katika hatua mbalimbali ambazo walifika.
Al Merrikh ambao kwa sasa wanafundishwa na Kocha Lee Clark raia wa England, mechi za ugenini walizopoteza ni dhidi ya Al Ahly msimu huu wa 2020-21 kwa mabao 3-0 hatua ya makundi, kisha msimu wa 2019-20 walichapwa na JS Kabylie ya Algeria 1-0 hatua ya awali na msimu wa 2018–19 walipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Vipers ya Uganda.
Rekodi ya kupoteza ugenini haijaishia hapo, kwani mwaka 2018 walibamizwa mabao 3-0 na Township Rollers ya Botswana, wapinzani wao Etoile du Sahel walipewa ushindi wa mabao 3-0 na pointi tatu, kisha mwaka 2016 ndiyo pekee ambao waliambulia pointi walipotoka suluhu na ES Sétif.
Wakati Al Merrikh wakiwa na rekodi hiyo mbaya ya kupoteza ugenini, Simba wamekuwa na historia ya kupata matokeo mazuri katika uwanja wa nyumbani.
Kwa msimu huu pekee katika mechi tatu, wameshinda mbili dhidi ya Al Ahly (hatua ya makundi) 1-0, wakiwachapa 4-0 FC Platinum hatua ya mtoano na suluhu walipocheza na Plateau United.
Lakini tangu msimu wa 2018-19, Simba hawajawahi kupoteza uwanjani hapo wakicheza mechi tisa, wakishinda saba mbele ya AS Vita (2-1), Ahly mara mbili zote kwa bao 1-0, Mbabane Swallows (4-1), Nkana FC (3-1), FC Platinum (4-0) na JS Saoura (3-0).
Huku wakitoka sare dhidi ya UD do Songo (1-1) na 0-0 dhidi ya Plateau.
KAULI ZA MAKOCHA
Gomes alisema: “Lazima tushinde mchezo wetu wa kesho (leo) na tutashinda mapema tu kwani malengo yetu ni kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hii mikubwa Afrika, tulikuwa tuna siku tano nzuri za maandalizi ya mchezo huu.
“Katika mchezo huu tutaingia kwa mbinu tofauti na mchezo uliopita tuliocheza na Al Merrikh nyumbani kwao Sudan, hivyo tutacheza kwa kushambulia muda wote.
“Kukosekana kwa mashabiki katika mchezo huu kutatuathiri na kwangu nimeumia, kwani tulikuwa tumezoea kucheza na mashabiki na kupata matokeo mazuri, hivyo kukosekana kwao ni tatizo.
”Kwa upande wa Lee Clark, alisema: “Timu yangu ipo vizuri baada ya kufanya mandalizi ya kuhakikisha tunapata ushindi kesho (leo) baada ya kutoka suluhu nyumbani.“Morali ya timu ipo juu kuelekea pambano hilo ambalo muhimu kwetu kupata ushindi.”
Naye Nahodha wa Simba, John Bocco, alisema: “Maandalizi tuliyoyafanya yanatosha kwetu kupata matokeo mazuri, kikubwa nafurahia morali iliyopo kwa wachezaji wenzangu.
“Kikubwa tutaingia uwanjani kutafuta pointi tatu ili tutimize malengo yetu ya kufuzu robo fainali, tuwaombe mashabiki waendelee kutuombea dua, tutawawakilisha vizuri.”Simba ndiyo vinara wa Kundi A katika michuano hiyo wakiwa na pointi saba, wakifuatiwa na AS Vita na Al Ahly ambao kila mmoja ana nne, huku Al Merrikh wakikusanya pointi moja wakiburuza mkia.
Nawatakia simba ushindi mwema
ReplyDeleteKadi ni tatu waandishi mnakwama wapi?
ReplyDelete