LIGI Kuu Tanzania Bara inazidi kukata mbunga hasa kwa mzunguko wa pili ambapo kumekuwa na matukio mengi mazuri na mabaya ndani ya uwanja.
Wachezaji wengi wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kusaka ushindi ndani ya uwanja. Wanaoenkana kuegeuza uwanja kuwa ulingo kama ambavyo mabondia wanafanya.
Waachane na tabia ya kugeuka kuwa mabondia kwa kupigana ama kuchezeana vibaya ndani ya uwanja.
Maamuzi yao ndani ya uwanja yamekuwa yakiwagharimu wachezaji wenzao hasa pale wanapoumia katika harakati za kusaka ushindi.
Katika hili ni muhimu kwa kila mchezaji kuwa mlinzi wa
mchezaji mwenzake kwa kuwa hali haijawa salama kwa nyakati hizi ukianza
mzunguko wa kwanza na huu wa pili.
Jambo moja la msingi la kufanya kwa wachezaji ni kujali
mpinzani wake na kuamini kwamba mpira sio vita bali ni burudani.
Ile burudani inapopotea na kuanza kuwa ni vita ndani ya
uwanja hapo tunashuhudia balaa kubwa. Imekuwa kawaida kwa sasa ndani ya uwanja
kushuhudia buti za maana pamoja na viwiko kwa wachezaji.
Hali hii ni mbaya hasa kwa afya za wachezaji wetu ambao kazi
yao ni mpira. Kati ya vitu ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya mchezaji ni
maumivu anayopata akiwa kazini kwa kuumizwa.
Wapo ambao mpaka leo hawakukubali kurudi uwanjani kwa
kuhofia kuumizwa pia wapo ambao mpaka muda huu wanatibu majeraha ambayo waliyapata.
Ipo wazi kwamba mchezo wa mpira ni mchezo wa kutumia nguvu
ila ifike mahali kwamba nguvu itumike pale inapostahili.
Wapo wale ambao wanachukua sheria mkononi na kutumia ubabe
hili halipo sawa ni muhimu wachezaji kubadilika na kucheza kwa ustaarabu ndani
ya uwanja.
Kwa sasa kumekuwa na maumivu mengi kwenye soka hasa kutokana
na kuripotiwa baadhi ya matukio ambayo hayaleti picha nzuri. Muhimu kwa
wachezaji kuwa makini ndani ya uwanja muda wote
Endapo inaweza kutokea tukio baya ambalo labda mwamuzi
hajaona ama wachezaji hawajaona itakuwa ni hatari kwa timu nzima pamoja na
mchezaji mwenyewe.
Hivyo jambo la msingi wachezaji wote wanapaswa wajue kwamba
mlinzi wa mchezaji mwingine ni mchezaji mwenyewe uwanjani.
Kama linatokea tatizo anapaswa atoe huduma kwanza kabla ya
kuangalia matokeo ambayo anayapa kipaumbele kwani uhai wa mchezaji ni bora muda
wote kuliko matokeo yenyewe.
Itakuwa ni wakati mzuri pia kwa timu zote kujifunza kuwa na
'Fair Play' uwanjani ili kutoa mwanya kwa wachezaji kuwa na maamuzi sahihi
kuhusu afya za wachezaji.
Ikitokea hivyo itawajengea uwezo wachezaji kujali na kuwa na
maamuzi yenye busara wawapo uwanjni kwenye mashindano muda wote.
Kwa kufanya hivyo pia kutaokoa maisha ya mchezaji ambaye
amepatwa na matatizo akiwa ndani ya uwanja bila kujali yupo mazingira gani
ilimradi naye pia ni mchezaji.
Soka sio mchezo wa maumivu bali ni mchezo wa uungwana kwa kila
mmoja ndio maana wachezaji wamekuwa wakipeana mikono ikiwa na maana kwamba wote
ni kitu kimoja.
Kumbuka pia hata hivi karibuni Bernard Morrison wa Simba pamoja na Juma Nyoso wa Ruvu Shooting walikutwa na adhabu ya kufungiwa mechi tatu kwa sababu ya kupigana uwanjani.
Ukiweka kando wachezaji kujali afya za wengine wimbo
mwingine ni kwa waamuzi ambao wanapewa jukumu la kusimamia sheria 17 nao
wamekuwa wakionekana kuboronga.
Ligi bora inaendeshwa na waamuzi makini duniani hakuna timu
ambayo inaweza kuwa bora kama itakuwa inabebwa ama kufanya vitendo ambavyo
vinatoa viashiria vya kubebwa hakuna.
Hivyo waamuzi waache kuchezesha wakichanganya mapenzi yao ya
klabu ama maamuzi yao binafsi sio sawa kwa ajili ya afya ya soka.
Hili ni doa ambalo linatibua ligi msimu huu na linarejesha
nyuma ile morali ya wachezaji pamoja na timu kusaka ushindi.
Kila mmoja atimize majukumu yake kwa wakati na kuanza
kujipanga ni sasa. Nina imani kupitia ripoti pamoja na yale ambayo yamejitokeza
itakuwa ni darasa ili kuwa bora kwa wakati ujao.
0 COMMENTS:
Post a Comment