NYOTA wa zamani wa Yanga, Bernard Morrison wakati ule alipokuwa kwenye ubora wake ndani ya Yanga alikuwa anafanya maamuzi ambayo anayajua yeye mwenyewe na hakukuwa na adhabu juu yake zinazochukuliwa na hakuna ambaye alikuwa anajali.
Ilikuwa anaweza kuacha kwenda kwenye mazoezi kwa sababu zake binafsi na mwisho wa siku akaendelea kuwa na uhakika wa kuanza kikosi cha kwanza.
Ilikuwa ni zama za aliyekuwa Kocha Mkuu, Luc Eymael ambaye alikuwa anatambua kwamba Morrison ni mchezaji mzuri ila anakwama kuwa na nidhamu bora.
Ilifika wakati aligoma kusafiri kwa basi wakati timu ilipokwenda Bukoba kucheza mchezo wa ligi kutokana na Eymael kuhitaji huduma yake mwisho wa siku alikwea pipa na kwenda kucheza mchezo huo.
Rekodi zinaonyesha kwamba kwenye mchezo huo wa ligi, Morrison alifunga na kutuma salamu kwa watani zao wa jadi, Simba kwa kuwa walikuwa na mchezo wa Kombe la Shirikisho ambao ulikuwa mbele yao.
Ni kweli aliwafunga Simba kwa bao la faulo akiwa nje ya 18 kwenye Kariakoo dabi na ulikuwa ni mchezo wa ligi ila bado alikuwa anabebwa na Eymael kwa kuwa alikuwa anampenda na anatimiza majukumu yake.
Niliwahi kuongea na Eymael kuhusu Morrison aliniambia kwamba hakuna ambaye hajui kuhusu Morrison hasa kwenye nidhamu ila anamuamini kwa kuwa ni mchezaji mzuri.
Ikawa hivyo kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho wakati ubao ukisoma Simba 4-1 Yanga baada ya Morrison kufanyiwa mabadiliko alisepa mazima na akatoka uwanjani jumlajumla.
Alipanda bodaboda na kusepa baada ya hapo ikawa ni mvutano kuhusu mkataba wake na mwisho akajiunga Simba huku bado akiwa kwenye mvutano na mabosi wake wa Yanga wakieleza kuwa nyota huyo ana mkataba nao.
Weka kando hayo ya Morrison ambaye ni raia wa Ghana sasa ghafla mambo yamekuwa tofauti kwa huyu Mrundi, Said Ntibanzokiza.
Kuanza kwake benchi kwenye mchezo dhidi ya Gwambina inaonesha wazi kwamba alikasirika na alikuwa anaamini kwamba yeye ni lazima aanze kikosi cha kwanza.
Huenda yapo ambayo mimi siyajui ila Yanga wanajua hapo kama kuna kitu nyuma ni lazima kifanyiwe kazi maana hiki ni kama kivuli cha Morrison.
Sawa nakubali kila mchezaji anahitaji kuanza kikosi cha kwanza lakini suala la mwalimu kufanya maamuzi linapaswa liheshimiwe.
Upana wa kikosi na mbinu za mwalimu zinampa fursa ya kufanya vile anavyohitaji ila kuonekana mchezaji anakasirika na kueleza kuwa ni sehemu ya mchezo naona ni yaleyale ya Morrison tena kufanya vile ambayo anajiskia.
Duniani kote hakuna mchezaji mkubwa kuliko timu hivyo hata kama ameomba msamaha Saido inabidi atambue kwamba kwa kitendo alichokifanya kwa mchezaji wa kigeni sio cha mpira ni kitendo kinachoshusha hadhi yake.
Muhimu kwa wachezaji wazawa pamoja na wale wanaochipukia kuwa na nidhamu na kuheshimu maamuzi ya kila mmoja, nina amini kwamba Yanga wataongea naye na watamaliza zile tofauti ambazo zipo kwani nimemsikia Senzo Mbatha akiweka wazi kwamba watazungumza naye.
Senzo akizungumza nae juu ya nidham, nae pia atamwambia mbona nawe uliondoka Simba bila ya kuaga au kukabidhi, jee hiyo ni nidham?
ReplyDeleteSaido ajiulize kuwa... 1)je, mechi zote alizoanza timu ilishinda? 2) Alipoingia kutokea benchi alifungnga goli la ushindi au alikuta timu inaongoza? Aheshimu maamuzi ya kocha asilete dharau
ReplyDelete